Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti ya Kilimo. Kwanza, kabisa ninaomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uzima na uhai hatimaye tuko hapa tunachangia maendeleo ya kilimo katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kupitia kilimo. Amefanya kazi kubwa sana, lakini ninaomba nimpongeze Waziri Bashe pamoja na Naibu Waziri. Ninaomba nimpongeze Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na ninaomba niwapongeze watendaji wote wa Wizara ya Kilimo pamoja na taasisi zote zinazohusika na Wizara ya Kilimo kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Bashe kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kupitia Wizara ya Kilimo; ameonesha taswira mpya kabisa katika Wizara ya Kilimo. Vilevile amefanya kazi kubwa na nzuri ambayo hata leo wakulima wa Tanzania wamebadilisha maisha yao kupitia majukumu mazito, kuona matatizo yao na kuyabeba kama ya kwake yeye binafsi. Ninaomba nikupongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya kwanza tulikuwa tunakusumbua sana kupitia mazao yetu ya kibiashara kama tumbaku na pamba, lakini ulitazama kwa mtazamo chanya. Ukahakikisha, ukaanza kufuatilia zao moja baada ya lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka Mheshimiwa Bashe hakuna zao lililokuwa linasumbua kama tumbaku. Wakulima wa tumbaku walikuwa duni. Waliokuwa wanalima zao la tumbaku walikuwa maskini, lakini toka ulivyoingia Mheshimiwa Bashe umebadilisha taswira ya wakulima wa tumbaku. Leo hii wakulima wa tumbaku nao wako katika historia ya kilimo chao ambacho wanacho katika maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umwagiliaji; Mheshimiwa Bashe ninaomba nikupongeze na nikushukuru sana. Ulikuja kwenye Jimbo langu na uliniahidi katika umwagiliaji kwenye Jimbo la Nsimbo utaweka mabadiliko makubwa sana na uliahidi kuwa utatoa shilingi bilioni 50, ninakushukuru. Ninaomba nikupongeze na mkandarasi Mchina alianza kazi katika Skimu ya Umwagiliaji ya Usense. Vilevile, ulisema utajenga nyumba kwa ajili ya yule ambaye ataisimamia skimu ile, ambaye ni afisa kilimo na kumletea gari. Hata hivyo, kwa bahati mbaya mpaka sasa hivi ule mradi umesimama kabisa. Sasa sielewi matokeo yake yakoje, lakini ninaomba nikushukuru sana kwa sababu ulifika lakini una nia njema na wakulima wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishukuru Mheshimiwa Rais ameleta ruzuku kwa wakulima. Ruzuku ile wakulima wa pamba na wakulima wa tumbaku walikuwa hawana ruzuku kabisa, lakini sasa hivi wakulima wa tumbaku wamepata ruzuku na wenyewe sasa hivi wananeemeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuwarejeshea wakulima ruzuku ile ya mwaka jana. Ile bakshishi yao umeanza kuwalipa, lakini mpaka sasa hivi kuna watu ambao wameanza kulipwa, lakini mpaka sasa hivi kuna wengine hawajaanza kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niipongeze Benki ya NBC, wao wameanza kulipa zile AMCOS zao ambazo wako nazo, lakini bado CRDB hawajaanza kuwalipa wale wakulima katika AMCOS zile nyingine. Ninaomba Mheshimiwa Bashe sasa hivi wakulima wana matumaini makubwa sana na wewe, wanakupenda kwa sababu umebadilisha maisha yao. Wakulima wa Tanzania wanakupenda, umebadilisha maisha yao kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaomba hawa ambao bado (Benki ya CRDB), basi iongeze speed iwalipe ili na wenyewe AMCOS nyingine ziweze kupata manufaa yale yanayotakiwa na kupata stahili yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu stakabadhi ghalani; ndani ya Mkoa wetu wa Katavi hususan Jimbo la Nsimbo tunalima ufuta na wananchi wa Halmashauri ya Nsimbo walikuwa bado hawajazoea kuingia kwenye stakabadhi ghalani. Hata hivyo, ninaomba niishukuru Serikali kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. Tunaona kupitia mikoa mingine ya Mtwara, Lindi na sehemu mbalimbali kupitia stakabadhi ghalani manufaa makubwa ambayo wanayapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaomba mwaka huu Mkoa wa Katavi tuingie kwenye stakabadhi ghalani na wananchi bado hawajazoea, hili jambo ni geni kwao. Nilikuwa ninaomba sana twende kwenye elimu kwa mwaka huu. Tuwape elimu ya stakabadhi ghalani kwa sababu walikuwa hawajawahi kufanya kupitia zao la ufuta. Ninaomba tuwafundishe kwanza, tuwaelekeze mwaka huu halafu mwakani sasa tuingie kwenye stakabadhi ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake sasa hivi imekuwa ni mgongano kwa sababu hawajui, hawajazoea, wameshazoea kuuza kiholela na sisi tunapenda kwa sababu unaona sasa hivi hapa kuna Waheshimiwa Wabunge wamesema waliongia kwenye stakabadhi ghalani kupitia ufuta wameuza kwa bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaomba, tunatamani na wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kupata mafanikio ya ufuta na mwaka huu 2025 wamelima sana ufuta, lakini jambo hili la stakabadhi ghalani limewakuta tayari wameshazoea mtazamo mwingine na wanatakiwa waingie kwenye mtazamo mwingine. Nilikuwa ninaomba sana tuingie kwenye elimu...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Mheshimiwa Bashe ninaomba nikupongeze sana kwa kazi kubwa uliyofanya kupitia sekta ya kilimo, hongera sana. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wetu wa Katavi atapata kura 100%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)