Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Francis Kumba Ndulane

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Bajeti yetu ya Serikali. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu kuchangia. Pia, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia amani, utulivu, umoja na upendo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya udadisi katika Wimbo wetu wa Taifa nikagundua kwamba, tumemwomba Mwenyezi Mungu mara kumi alete baraka katika Taifa hili. Kwa hiyo, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupokea maombi yetu na kuliwezesha Taifa letu liendelee kuwa na baraka na maendeleo. Pia, ninasema tu kwa wale wachache wenye nia mbaya ya kutaka kuvuruga umoja, amani na utulivu kwa uweza wa Mwenyezi Mungu wetu na manabii wake waliompendeza tangu kale, washindwe na walegee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa, ambayo ameifanya kwenye jimbo imeonekana hata na nchi nzima. Kwa ujumla tumeshuhudia miradi mingi ya kimkakati; miradi ya maendeleo katika sekta zote imefanyika na kuwezesha kutimiza dhamira aliyokuwanayo, ambayo aliitoa kwenye hotuba yake ya tarehe 19 Machi, 2021 wakati alipoapishwa kushika hatamu ya uongozi wa nchi yetu, lakini pia, alirudia maneno yaleyale wakati alipofika hapa Bungeni kwa mara ya kwanza kulihutubia Bunge, Siku ya tarehe 22 Aprili, 2021. Kwa hiyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kusimamia vizuri kutoa fedha nyingi na kuzielekeza katika miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza na kuwashukuru rafiki zangu, schoolmates wangu, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Manaibu wao pamoja na watumishi waliopo katika Wizara hizo kwa kutuletea bajeti nzuri, ambayo ina reflect maono ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia, nitakuwa mchache wa fadhila nisipompongeza RC wangu, dada yangu, Mheshimiwa Zainab Telack.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, amefanya kazi kubwa sana katika Mkoa wa Lindi kusimamia miradi mbalimbali inayoelekezwa huko, sanasana kwenye eneo la kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji, lakini pia, kupandisha kiwango cha elimu. Kwa kweli, tumefanya vizuri sana katika miaka hii ya karibuni na sasa tunashuhudia matunda ambayo yamewekezwa na Mheshimiwa Rais wetu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo hiyo sekta ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchache wa fadhila pia nisipowapongeza na kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kilwa Kaskazini katika kata zote 13 kwa kuniunga mkono katika mambo mbalimbali ambayo yaliainishwa katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, lakini pia, yaliyokuwa yanatatiza katika jimbo letu. Ninawashukuru sana wananchi wa Kata ya Kipatimu, Chumo, Kibata, Kandawale, Namayuni, Mingumbi, Tingi, Somanga, Kinjumbi, Miteja, Mitole, Njinjo na Miguruwe. Ninamwomba Mwenyezi Mungu anijalie afya njema ili niendelee kuwatumikia katika kipindi kijacho cha miaka mitano wananchi wa Jimbo langu la Kilwa Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata mambo mengi sana kupitia bajeti ambazo zimewekezwa, ambazo zina reflect dhamira njema, ambayo anayo Rais wetu katika Jimbo la Kilwa Kaskazini. Tumepata zahanati zaidi ya nane, vituo vya afya zaidi ya vitatu na kingine kimeletewa fedha juzi katika Kata ya Kandawale, shilingi milioni 250. Tumepata shule za sekondari tatu, za msingi sita na pia, miradi ya maji zaidi ya vijiji 14 imetekelezwa. Tumepata madarasa ya kutosha, matundu ya vyoo ya kutosha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na vifaa tiba vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, minara ya simu zaidi ya 16 imewekwa katika Jimbo la Kilwa Kaskazini, maboti ya uvuvi, mpango wa matumizi bora ya ardhi umefanyika katika zaidi ya vijiji 44 na unaendelea. Pia awamu ya mwisho ambayo imetolewa Mwezi Januari tumepata mikopo zaidi ya shilingi bilioni 1.3, kwa ajili ya wanawake vijana na kundi la wahitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kuliko yote ni tulipopatwa na janga la mafuriko Serikali imeleta zaidi ya shilingi bilioni 119 na 47%, sawa na shilingi bilioni 56, imekwenda katika Jimbo letu la Kilwa Kaskazini kujenga miundombinu mipya wezeshi katika maeneo hayo ya barabara. Kwa hiyo, namshukuru tena Mheshimiwa Rais na ninamuombea kwa Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, ili tuweze kumpa tena kipindi cha miaka mitano. Tumejiandaa Wanakilwa Kaskazini na Wanakilwa kwa ujumla kuweza kumpa ushindi wa kishindo. Mwenyezi Mungu amjalie sana mama huyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ya kushauri. Jambo la kwanza, ninaomba miradi ya maji iendelezwe, hasa katika vyanzo vikubwa vya mito. Sisi bahati nzuri Mikoa ya Kusini hatuna ziwa, ukiondoa kule Ruvuma, lakini tuna mito mingi inayotiririsha maji mengi yanayokwenda baharini; Mto Ruvuma, Mto Lukuledi, Mto Ruhuhu, Mto Rufiji na ipo mito ya msimu zaidi ya mitatu, Mto Mbwemkuru, Mto Matandu na Mto Hanga, ninafikiri Serikali sasa ijikite katika kuona namna ambavyo itaboresha miundombinu hiyo ya maji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarajia Serikali iweke mabwawa katika mito hii, ambayo ni seasonal, kwa sababu itasaidia kwanza itapunguza mafuriko ambayo tumeyaona mara kwa mara, lakini pili, kupata malisho ya mifugo. Pia, itasaidia kupata maji, kwa ajili ya mifugo pamoja na kupata maji safia na salama, kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninaomba miradi yetu ya BBT Serikali iiangalie katika maeneo ambayo mazao yake hayavunwi kwa wingi, yale ya kimkakati ambayo yatakwenda kutatua matatizo ya msingi tuliyonayo. Tumeona miradi mingi imeelekezwa kulima pilipili hoho, kabichi, vitunguu; mimi ninafikiri kwa sababu, hizi bidhaa zinapatikana kwa wingi na nyingine nyingi tunauza nje ya nchi tuwekeze, labda kwa mfano kwenye zao la kimkakati ambalo tutapata uzalishaji wa mafuta kwa sababu, mpaka leo tunatumia fedha nyingi za kigeni kwenda kununua mafuta kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto, kwa mfano ya wakulima na wafugaji katika Mikoa ya Kusini, hasa Mkoa wa Lindi na wilaya zake. Ninafikiri katika eneo hilo Miradi ya BBT ilenge katika kutatua changamoto za msingi, kama hii ya migogoro ya wakulima na wafugaji. Kwa hiyo, ninafikiri tukienda hivyo basi maisha ya wananchi wetu yatakuwa mazuri, lakini pia, uchumi utaimarika na mambo mengine yatakwenda sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali iongeze nguvu katika barabara za vijijini. Barabara nyingi za vijijini, hasa katika Wilaya ya Kilwa, Wilaya ya Rufiji na majimbo yote mawili ya Kilwa Kusini na Kaskazini, Liwale, Nachingwea na kwingineko zilikumbwa na tufani ya Mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya. Tunaishukuru Serikali, kama nilivyosema mwanzo, Mkoa mzima wa Lindi umeleta shilingi bilioni 119, miradi inaendelea na jana nilikuwa jimboni, baadhi ya makalavati yameanza kukamilika kwa hiyo, ni hivi karibuni tutapata tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kule kwenye barabara za vijijini, ambako huko ndiko mazao ya korosho, ufuta na mengine yanatoka yapate kusafirishwa kirahisi kufika kwa walaji, kwenye masoko, ninafikiri bado kunahitajika fedha nyingi ziongezwe. Hii ni, ili kuhakikisha uchumi wa wananchi wetu unaendelea kuimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, Serikali imekuwa ikitumia nguvu kubwa sana inayotokana na mapato yake ya ndani kuendesha miradi ya kimkakati na yenye vigezo vya kibiashara. Katika eneo hili tunayo taasisi yetu iliyoundwa, ambayo inahusika na miradi ya ubia au PPPC (Public Private Partnership Centre); ninafikiri kitengo au taasisi hii iwezeshwe vya kutosha, ili itoe msaada mkubwa kwa mtaji wa kuendesha hii miradi. Matokeo yake ni Serikali itapunguziwa mzigo wa kibajeti katika kuhudumia hii miradi, lakini pia, tutapata teknolojia kutoka kwa hawa wawekezaji kwenye hiyo miradi ya ubia, tutapa ufanisi mkubwa na pia, ubunifu wa kutosha wa kuendeleza hiyo miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba, miradi ikishirikisha watu binafsi maana yake ni tutatanua wigo wa watu binafsi kuweza kushiriki katika shughuli za maendeleo na hivyo, wananchi kukua kiuchumi, kama mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Kwa hiyo, ninaomba Serikali iangalie hata ile SGR, aliyozungumza rafiki yangu hapa Mheshimiwa Mpakate, inaweza ikaingia katika utaratibu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ifanye bidii ipate wawekezaji wabia tuweze kujenga kwa haraka hata ile ambayo bado haijaingizwa kwenye mpango, ya kutoka Dar es Salaam kupitia Lindi mpaka Mtwara nayo iweze kujengwa bila shida. Kuna Nchi kama Korea, Malaysia zimepiga hatua kubwa sana kwa kutumia hii miradi ya PPP kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu Tukufu isimamie jambo hili, ili kuhakikisha kwamba, utekelezaji wa miradi siyo tu unatekelezwa kwa mtaji wa Serikali, bali pia, unashirikisha watu binafsi chini ya utaratibu wa PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)