Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi, lakini pia ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii ya jioni hii ya leo ya kuweza kupata nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya katika Taifa letu. Tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu amjalie afya njema ili inapofika Oktoba 25, wananchi waweze kumwamini tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwa kazi kubwa ambazo ameendelea kuzifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya jambo kubwa la kihistoria ambalo limekaa pale Bunda kwa muda mrefu ambapo aliidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 50 kuwalipa wananchi wetu wa Kata ya Nyatwali ambao baadhi yao wameshaondoka na baadhi yao bado hawajaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo pia, bado kuna changamoto ndogondogo ambazo bado wananchi wetu wanazidai kwenye Serikali. Niwaombe watu wa Serikali kabla ya kumaliza bajeti hii waweze kuwalipa wale wananchi wetu waondoke katika eneo lile ili waweze kwenda kuanza maisha yao sehemu nyingine. Kwa hiyo tunawashukuru na watu wa Wizara ya Fedha kwa kufanya jambo hili ili wananchi wetu hawa waweze kupata maisha yao katika eneo lingine.


Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninapenda niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Bunda Mjini kwa namna ambavyo waliniamini miaka mitano na ninaamini kupitia Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tumefanya kazi kubwa na kuubadilisha mji wetu wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kwani si kama tulivyoingia, lakini leo mji ule umebadilika na unaonekana ni mji wa kisasa. Pia, shughuli za maendeleo zinakwenda kwa speed. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe tu wananchi wetu wa Jimbo la Bunda Mjini itakapofika 25 ya mwezi wa 10 waweze kuendelea kuiamini Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Chama chetu Cha Mapinduzi. Mimi pia mwenyewe bado nitakuwa tayari kama Mungu akinijalia uzima kuendelea kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajadili Bajeti ya Wizara ya Fedha. Hivyo, tunajadili Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa muunganiko wa Wizara zote ambazo tumeshazijadili (Wizara ya Fedha na Wizara zingine zote ambazo zimepita) ili haya yote ambayo tumeyazungumza hapa zaidi ya miezi mitatu tuyamalizie hapa kwenye Wizara ya Fedha. Pia, Wizara ya Fedha ili iyafanye haya mambo yote yaweze kufanyika vizuri, lazima kupatikane pesa na hizo pesa mahali pa kupatikana lazima zitoke kwa wananchi wetu wale wanaofanya shughuli mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu kwa wananchi wenzangu, Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania wote kila mmoja kwa nafasi yake; kwa sababu bajeti yetu inategemea makusanyo yetu tujitoe wale wanaofanya biashara kila mmoja kwenye nafasi yake ili aweze kulipa mapato kwenye Serikali. Hii ni kwa sababu bila kufanya hivyo wananchi hawawezi kudai barabara wala maji, vituo vya afya, shule za misingi na sekondari na mambo mengine kama watakuwa hawawezi kulipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima watu walipe kodi. Bahati nzuri tunaendelea kuishukuru Serikali kwa sababu imeendelea kutengeneza mazingira mazuri ya ulipaji kodi kama hivyo ambavyo inaendelea kupunguza kero mbalimbali za wafanyabiashara ili wafanyabiashara waweze kulipa kodi kwa hiari zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na vizuizi vyote ambavyo vinaondolewa kwa ajili ya kuleta kero kwa wafanyabiashara, lazima sisi kama wafanyabiashara tujue kwamba kulipa kodi ni suala la lazima. Tunalipa kodi ili kuiletea nchi yetu maendeleo. Nje na kodi, haya yote ambayo tunazungumza hapa hakuna kinachoweza kufanyika na hatuwezi kupata maendeleo kwenye nchi yetu yasiyotokana na sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata zikiwa ni fedha za misaada tunazipata, hizo baadaye zinalipwa na zinalipwa kutokana na kazi zetu ambazo sisi wenyewe wananchi wa Tanzania tunazifanya. Kwa hiyo, niiombe Wizara ya Fedha iendelee kuboresha miundombinu ya utozaji kodi kwa wananchi na wafanyabiashara mbalimbali ili kwamba wananchi waweze kulipa kodi zao vizuri kwa ajili ya manufaa ya nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kero mbalimbali ambazo zilikuwa zinawapata wafanyabiashara za kufungiwa biashara zao ni kweli kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha jambo hili limekuwa likifanyika. Mamlaka ndogo za halmashauri au za kata, jambo dogo tu kwa mfanyabiashara wanaweza kwenda wakafunga biashara na unaona kama ni jambo ambalo wangeweza kuzungumza wakaelewana na maisha yakaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu pia wanapofunga biashara ya mtu wanamfanya pia asipate nguvu ya kulipa hicho ambacho wao walienda kukidai. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, kwa jambo hili ambalo amelisisitiza hapa kwenye hotuba yako tunaiomba sana Serikali ilisimamie vizuri. Ninaamini Watanzania leo wameelimika kwa kiasi kikubwa na wana uelewa mzuri sana kwa ajili ya kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninataka kuzungumza jambo la hizi control number ambazo tunatumiwa kwenye mifumo ya Serikali na sisi tunazitumia kwa ajili ya kufanya malipo kwenye Serikali. Kuna mahali ambapo panaonyesha bado control number hizi inawezekana zikatolewa ukafanya malipo lakini malipo yale yasifike mahali husika. Sasa kwa jambo hili likionekana ni kweli na likaendelea kuwepo linaweza kuja kuleta madeni makubwa sana kwa wafanyabiashara wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana watalaam wetu wa Serikali ambao wao ndiyo wanasimamia mifumo hii waisimamie vizuri. Tulipe malipo ya Serikali kupitia hizo control number za Serikali, lakini na malipo hayo yenyewe yafike Serikalini pia ili kwa baadaye lisije likageuka kuwa tatizo kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni jambo la vyuo hivi vya ufundi na shule za amali ambazo Serikali imetoa fedha na zimejengwa karibu katika kila halmashauri. Jambo hili Serikali ikilisimamia vizuri vijana wetu wengi wakapata uwezo wa kufanya kazi na wakawa wamefundishwa; kwa sababu zile shule kwa mfano shule ya amali ambayo imejengwa pale Bunda Mjini, hata kama wale wanafunzi watafundishwa kwenye maeneo yale watafundishwa vitu ambavyo pia vinaendana na jiografia ya maisha yao na pale wanapoishi na vitu ambavyo wanaweza wakavitumia wao wenyewe. Kwa hiyo niiombe sana Serikali iendelee kuboresha shule hizi na vyuo vyetu vya ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu likipata watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa kiasi kikubwa ndiyo njia pekee ambayo tunaweza tukaisaidia nchi yetu kwa kufanya walipakodi waongezeke zaidi kuliko wale walipakodi wachache waliopo ambao wanapewa mzigo mkubwa wa kulipa kodi. Kwa hiyo kupitia shule hizi na vyuo vyetu vya ufundi kama Serikali itasimama vizuri na jambo hili, ikawajengea vijana wetu uwezo wa kufanya kazi vizuri kama vile ambavyo tuliona jambo hili la pikipiki lilipojitokeza pamoja na kwamba unaona vijana wetu wanavyochangamka nalo ni jambo ambalo linawasaidia kwa sababu pia limepunguza sehemu kubwa ya tatizo la ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wote wale ambao wanaendesha pikipiki leo au bajaji na vitu vingine wasingekuwa na kazi hiyo wakategemea kwenda kuomba kazi Serikalini, Serikali isingekuwa na uwezo wa kuwaajiri watu wote hao; isingewezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuiombe sana Serikali iendelee kuboresha vyuo hivi vya ufundi na shule hizi za amali ili ziweze kuwafundisha vijana wetu kujitegemea na kuwajengea uwezo wa kuweza kufanya kazi zao za mikono ambazo zinaweza zikawafanya pia na wao wawe sehemu ya kuchangia pato kwenye nchi yao na Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili likisimamiwa vizuri kwa sababu, leo ukija kuangalia kwa mfano, bajeti yetu ya trilioni 56 fedha ambazo zinakusanywa katika nchi yetu ni takribani trilioni 30, trilioni 26 ni ambazo tunategemea kupata kutoka maeneo mbalimbali. Kwa hiyo tukiwaongezea watu uwezo wa kufanya kazi, wakajiajiri wao wenyewe, wakafanya kazi zao wenyewe, watakuwa ni sehemu ya kupunguza tatizo la nchi yetu kutegemea misaada kutoka nje. Jambo hili ni muhimu na ni ambalo Serikali inapaswa kulisimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuiomba Serikali. Kuna miradi mbalimbali ambayo imeanzishwa katika Halmashauri ya Mji wa Bunda; tuna vituo vya afya Kata ya Waliku, tuna kituo cha afya tumepata katika Kata ile ya Guta, tuna Hospitali yetu ya Halmashauri ya Mji wa Bunda, vyote hivi bado havijakamilika vizuri, bado tunaomba fedha kutoka Serikalini, ili Hospitali hii ya Halmashauri ya Mji wa Bunda iweze kukamilika vizuri, iweze kutoa huduma kuwasaidia wananchi wetu na vituo vyetu vile vya afya ambapo kimoja kipo Kata ya Waliku na chenyewe kimepata majengo, lakini bado hakijakamilika. Tunaiomba Serikali ifanye kila linalowezekana itoe fedha, ili vituo hivi vya afya viweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na barabara za mitaa ambazo kwa kiasi kikubwa leo zinapitika, vilevile changamoto bado zipo. Tunaiomba Serikali pia, iweze kutoa fedha, ili kuhakikisha kwamba, barabara hizi zinaweza kupitika kwa wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilikuwa na hayo. Ninakushukuru kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)