Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niungane na wenzangu kuweza kuunga mkono bajeti hii nzuri. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea bajeti nzuri ya trilioni 56.4 ukilinganisha na bajeti ya 2024/2025 ya trilioni 50. Maana yake nini? Ametupatia bajeti nzuri ambayo sasa tunayo imani inakwenda kufanya kazi nzuri katika kuwaletea maendeleo Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninampongeza Waziri Mwigulu na Waziri mwenzake Profesa, pamoja na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kweli tumeona mabadiliko ni makubwa sana. Mawaziri na Naibu Mawaziri wenu tunawapongeza sana. Vilevile sekta mbalimbali ambazo wanaziongoza ikiwemo TRA na nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwapongeze Mawaziri hawa kwa sababu kodi wanayokusanya TRA, mfumo ambao upo sasa, huko nyuma mfumo wa kukusanya kodi kwa wafanyabiashara ulikuwa ni wa nginjenginje, mshikemshike, kodi ilikuwa ni kama za kunyang’anya wafanyabiashara, lakini leo kodi inayokusanywa ni kodi iliyotulia, wanafanya mazungumzo na wafanyabiashara. Tunampongeza sana Waziri wa sekta na Kamishna Mkuu anayesimamia suala hili la kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumuiya ya Wafanyabiashara walikaa, wakaleta changamoto nyingi walizoeleza zinazoleta vikwazo katika biashara zao, tunampongeza Rais alimtuma Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa pamoja na Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango wakakae na hawa watu, tunawapongeza baadhi ya hoja wamezishughulikia, tunawapongeza sana. Ombi letu ni kwamba, hoja zilizobaki sasa na zenyewe ziweze kushughulikiwa ili shughuli za biashara ziweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nitamke moja ambayo ni hii kwamba wageni walikuwa wanafanya biashara ambazo wazawa tunaweza kufanya. Jambo hili lilikuwa siyo sawa na sasa wameliondoa; kwa hiyo, tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa kwenye hela hizi ambazo bajeti hii ipo mbele yetu. Ombi langu kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na mwenzake; kwenye maeneo yetu tuna maboma mengi sana ambayo kila halmashauri walisema yaletwe. Tunaomba fedha hizi sasa tutakapokuwa tumepitisha tarehe 24 ya kupiga kura (kura tutapiga ndiyo hakuna lingine) ili ziende sasa zikafanye kazi ya kutatua changamoto ya maboma haya ambayo yamejengwa yakiwemo ya Jimbo la Makambako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Makambako lina maboma ya zahanati, maboma ya majengo ya shule na mengineyo. Sasa ombi ambalo ninakuomba kuna kituo cha afya ambacho nilisema siku ile hapa kwenye swali ambacho kimejengwa kule Kitandililo, kimejengwa kule Mahongole pale kwenye Kijiji cha Mahongole kwamba haya yalishajengwa, walishatupa fedha na zilizobaki ni kumalizia. Waliagiza Mkurugenzi alete makisio na yameshaletwa Hazina; tunaomba fedha hizi ziende kwa wakati ili zikamalizie majengo haya ambayo tayari yameshaanza kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna hela ambazo walishatupa, shilingi milioni 583 fedha za kujenga shule ya ufundi na fedha zilizobaki bado hawajatupatia. Siku ile kwenye swali hapa Mheshimiwa Waziri alisema sasa wanajiandaa kupeleka fedha hizi za shule za ufundi ambazo zimepelekwa ninadhani kila baadhi ya halmashauri. Tunaomba sasa ziende ili zikakamilishe shule hizi za ufundi ziweze kufanya kazi ile iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo Kituo kingine cha Afya pale Usetule. Ninaomba na chenyewe hiki fedha ziende ili zikaweze kutatua. Kipo kingine tena kituo cha afya kipo pale Kata ya Kivavi na eneo linalojengwa linaitwa Kivavi. Kwa kweli niombe sana fedha hizi ziweze kwenda zikafanye kazi hiyo ya kutatua changamoto za wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile zipo fidia kwenye Jimbo la Makambako kuhusu suala la umeme wa upepo. Wawekezaji wa suala la umeme wa upepo kama imeshindikana basi Serikali itoe kauli ili maeneo haya yarudishwe kwa wananchi kwa sababu limechukua sasa ni miaka 18, (miaka 18 wananchi hawajalipwa fidia). Sasa kama mwekezaji wa suala la umeme wa upepo limeshindikana, basi tutamke kwamba imeshindikana tuwarudishie wananchi ili itakapofika muda Serikali inahitaji, watafanya mazungumzo upya kuliko hivyo sasa imekaa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupongeze hili suala la bodaboda na bajaji. Katika Mji wa Makambako tuna bodaboda nyingi, tuna bajaji nyingi zinasaidia sana wananchi. Suala hili ambalo limepitishwa hapa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu tunapongeza sana kwa kweli kwa dhati kabisa na wananchi jambo hili wamelifurahia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine hapa ninaomba niliseme. Nchi hii ni yetu sote. Tunapoona tunapokwenda wapo watu sasa wameanza kuleta viashiria ambavyo vinaweza kuvunja amani katika nchi hii. Mheshimiwa Rais amesimamia jambo hili vizuri sana. Hivyo tuombe taasisi inayohusika na baadhi ya watu kupitia mitandao mbalimbali wameanza kuchora picha mbaya kwa Mheshimiwa Rais (wanamchora kama vikatuni) nilisema siku ile hapa nilipochangia kipindi kilichopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inayohusika ishughulikie jambo hili. Mheshimiwa Rais wetu anaheshimika sana ndani ya nchi na nje ya nchi kwa mambo makubwa anayoyafanya ya kusimamia kuhakikisha nchi hii inakuwa ya amani. Kwa hiyo, niombe sana jambo hili Wizara inayohusika iweze kusimamia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo hapa vilevile ambalo biashara mbalimbali ambazo zinafanywa na wageni ambao nimesema hapa sisi wenyewe tunaweza kuzifanya. Jambo hili Watanzania walio wengi wana uwezo mkubwa wa kufanya. Kikubwa ni ninyi kutuwezesha kupitia benki za kukopa kwa riba nafuu ili tuweze kufanya kazi ambazo wanaweza wakafanya wageni. Sisi wenyewe tuna uwezo; wataalam tutaajiri na wapo wasomi wengi tutaajiri. Kwa hiyo jambo hili lisimamiwe kwa uzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho; ukanda wetu wa Kusini pale Makambako tumejengewa Kiwanda cha IDOFFI. Kuna mashine au mitambo ambayo ilishaletwa pale kwa ajili ya kutengeneza vidonge na syrup. Mashine hizi ni hela za Serikali za mabilioni zipo pale, majengo yapo haijafunguliwa. Alipokuja Mheshimiwa Makamu wa Rais kuangalia kile kiwanda na kuzindua tulimwonesha na aliagiza. Mpaka leo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu wakae na Mheshimiwa Waziri wa Afya, tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hiki hakifunguliwi, majengo yapo, mitambo ipo na fedha; wamekwama nini? Kamati ya Bunge ilipokuja iliona suala hili na waliagiza pia mwaka jana, mwaka juzi mpaka leo ipo. Kwa hiyo nimwombe sana watu wa ukanda huo tunategemea sana kiwanda hiki kifunguliwe ili wapate ajira vijana ambao watakuwa si wataalam wanaotokana na eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho wenzangu wamesema hapa. Unajua mtu akifanya vizuri ni lazima umpongeze. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Profesa tangu wameingia kila mmoja kwenye Wizara yake tumeona mabadiliko. Tunawaombea waendelee, Wizarani mambo yanakwenda vizuri na shughuli zinakwenda vizuri; tunawapongeza sana, sana, sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaombea kwenye majimbo yao, wananchi wa majimbo yao; Waheshimiwa Naibu Mawaziri na Waheshimiwa Mawaziri, watu wakawachague wawarudishe tena. Wamewatumikia Watanzania vizuri wakiwepo na Watanzania wa Jimbo la Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia...

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wake umeisha huyu, anamalizia tu. Malizia Mheshimiwa.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Makambako kwa kuniamini na kuendelea kuniamini. Pia, jana na juzi nimepita kwao kwenda kuwaambia mambo yaliyotekelezwa kwa bajeti hii ambayo inaishia mwezi huu Juni. Sasa ninawaomba waendelee kuniamini, nipo vizuri. Nitahakikisha ninakwenda kuwatumikia kwa bajeti hii ambayo tunakwenda. Ninawashukuruni na Mungu awabariki sana wananchi wangu ninawapenda sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, ahsante sana.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)