Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Kilimo. Kwanza, ninampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais mwenye upendo na mama wa kipekee ambaye ameonesha nia yake ya dhati kabisa kumkomboa mkulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipoona kwa mara ya kwanza tu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amepandisha bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 297 kwenda shilingi trilioni 1.2, tuligundua Mheshimiwa Rais Samia ameamua. Maamuzi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza bajeti kwenye kilimo yamepeleka tabasamu kubwa kwa Watanzania na kwa wakulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Samia alitufurahisha wakulima alipopeleka askari wawili wa mwamvuli ambao ni Mheshimiwa Hussein Bashe na Ndugu yangu Mheshimiwa Silinde. Mlipotumwa kwenda kama frontline foot soldiers kwenda kutatua obstacles zilizoko kwenye kilimo na hakika mmejua kuwafurahisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani, wananchi wangu wa Ngara na wale wa Mkoa wa Kagera, mmegusa penyewe. Mheshimiwa Bashe na Mheshimiwa Silinde, tunawashukuru sana kwa kuongeza bei ya kahawa. Mwaka 2021 kahawa ya maganda kwa kilo moja ya Robusta iliuzwa shilingi 1,200. Msimu huu ulioisha, kilo moja tumeuza shilingi 6,700. Haya ni mapinduzi makubwa kabisa kwenye kilimo. Tunawapongeza sana Mheshimiwa Bashe na mwenzako na watumishi wote wa Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri mliyoifanya. Aidha, tunawapongeza kwa mageuzi makubwa mliyoyafanya kwenye zao hili la kahawa. Kwanza, kubadilisha mfumo wa kuuza kahawa kutoka kununua kiholela holela kupitia Vyama vya Ushirika na kahawa kuanza kuuzwa minadani. Hapa mliupiga mwingi. Mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, minada mliyotuletea baada ya kuwa tulileta maombi imemwezesha mkulima kuuza kahawa yake kwa mtu mwenye pesa nyingi ambaye anakuwa ameleta bid kubwa. Mheshimiwa Bashe hongereni sana kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru kwa kuondoa tozo zaidi 49 ambazo zilikuwa zinamuumiza mkulima na kubakisha tozo saba ambazo tozo hizo sasa anatozwa mfanyabiashara wa kahawa na siyo mkulima. Hii imetoa nafuu kubwa sana kwa wakulima wa kahawa. Ahsanteni sana kwa kazi nzuri mliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nielekeze mchango wangu kwenye baadhi ya vitu muhimu ambavyo Wizara imewahi kuahidi na inatakiwa ivifanye. Hapo nyuma nimekuwa nikiomba Wizara itusaidie kuileta NFRA, ifanye price stabilization kwenye zao la mahindi ndani ya Wilaya ya Ngara na Mkoa wa Kagera. Mmetuahidi kwamba mwezi wa tano, wa sita huu NFRA walitakiwa kuwa Ngara, unfortunately hatujawaona. Ni ombi langu kwako Mheshimiwa Hussein Bashe na wenzako mtusaidie jambo hili liweze kutimia, price stabilization ifanyike, wakulima waache kuuza mahindi kwa bei ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mpango mzuri sana wa Wizara ya Kilimo kuhakikisha inaanzisha irrigation scheme kubwa. Scheme hizi zitaweza ku-serve mashamba makubwa ya kahawa na mazao mengine maeneo mbalimbali nchini, lakini kumbukeni changamoto kubwa ya wakulima ipo kwa wakulima wadogo wadogo na wakulima wa kati wanaovuna kuanzia tani 10 mpaka tani 100. Ninaomba nilete ombi kwako Mheshimiwa Bashe. Njoo na ubunifu wa ruzuku ya kuwezesha kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji kwa wakulima wa kahawa wanaozalisha tani 10 mpaka tani 100 kwa msimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya wakulima wa kahawa kwa sasa ni sisimizi wanaokula mizizi ya kahawa nyakati za kiangazi wakitafuta maji na ndicho chanzo cha kahawa nchini kukauka na kupunguza uzalishaji. Bila kuwapa irrigation, mini-irrigation scheme, mashamba yataendelea kukauka. Ninaomba sambamba na kugawa mbegu ya ruzuku, wakulima wanaozalisha vizuri waweze kusaidiwa katika eneo hili. (Makofi)

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua hiyo ni kengele ya kwanza na ninajitahidi kwenda na muda wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani kwenye upande wa miche ya kahawa. Ninaipongeza Wizara kupanga kugawa miche milioni 20 ya kahawa katika msimu huu. Mahitaji ya Wana-Ngara ni miche milioni 10 ndani ya kipindi cha miaka mitano. Wananchi wa Ngara wanaomba pale tulipoweka vitalu vya miche ya kahawa pembeni yake tuweke na vitalu miche ya parachichi. Wanapochukua miche ya kahawa, wachukue na ya parachichi. Anapomaliza kuuza kahawa, anapotumia fedha kabla haijaisha parachichi iwe imekomaa na aanze kuuza na aendelee kupata pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba utusaidie miundombinu iliyowekwa kwa ajili ya kuotesha miche ya kahawa kwenye viriba au vitalu, hiyo hiyo itumike kuotesha miche ya parachichi pembeni kandokando ya vitalu vya miche ya kahawa. Tutapiga njiwa wawili kwa jiwe moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masoko ya kimkakati ambayo Wizara iko inayajenga maeneo mbalimbali nchini ikiwepo Ngara. Nimeona ukurasa wa 107 wa Hotuba ya Mheshimiwa Bashe iliyojaa matumaini wa Watanzania imeonesha kwamba lile Soko la Kabanga limefika 50%. Sitaki kubishana na zile takwimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya ya Ngara amekwenda kutembelea pale amekuta mambo siyo mazuri sana, ninajaribu kutumia lugha nzuri. Kamati ya Siasa imeenda wiki iliyopita imekuta kazi siyo nzuri sana. Mheshimiwa Bashe nimeanza kusema wewe ni frontline foot soldier ambaye umeondoa obstacles nyingi kwenye Wizara ya Kilimo, hili haliwezi kukushinda. Ninaomba utusaidie kufuatilia masoko haya kwa sababu Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanashindwa kufuatilia vizuri kutokana na setup na usimamizi unaotoka Wizarani moja kwa moja kwenda kule. Ninaomba utusaidie eneo hili ili masoko haya yaweze kukamilika kabisa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Bashe kwa kazi nzuri. Hotuba yake imejaa matumaini makubwa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)