Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika hii Bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Mipango. Nichukue nafasi hii kwanza kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna alivyoweza kutujaalia na sasa tunaenda kufika mwisho wa awamu yetu katika hiki kipindi cha miaka yetu mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi ninawashukuru sana Wananchi wa Jimbo langu la Musoma Mjini kwa ushirikiano mkubwa walionipatia. La pili, ninaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kazi kubwa aliyofanya katika hii awamu yake hasa katika Huduma za Jamii kwa namna alivyoweza kuleta maendeleo makubwa katika Nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tu nimetoka Musoma, nilienda tu kufanya kazi moja ya kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao, lakini jambo moja kubwa ambalo wananchi wameridhika nalo ni kwa namna walivyoweza kupata huduma za kijamii kwa kiasi kikubwa sana. Kwa maana kwamba, fedha nyingi mama yetu amepeleka kwenye upande wa elimu, ameweza kupeleka fedha nyingi shule zimejengwa na vijana wetu wameendelea kupata elimu pasipokuwa na malipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huduma ya afya kazi kubwa sana imefanyika, vituo vingi vya afya vimejengwa, hospitali zimejengwa na huduma za afya zimeendelea kuboreshwa. Pia hata ungegusa katika sekta ya maji, kama kwangu pale Musoma Mjini habari ya maji tulishasahau kama tuna tatizo la maji tena. Hata ungegusa upande wa umeme na leo ukiangalia tuna umeme ambao wa ziada sasa na tunazalisha megawati zaidi ya 4,000 lakini matumizi yetu tunatumia tuseme kama 50%. Kwa hiyo, hapo pote panaonekana kwamba ni kwa kiasi gani Serikali yetu ya Awamu ya Sita imepeleka fedha nyingi kabisa hasa katika huduma za jamii na watu wetu wameendelea kufaidi matunda ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo mafanikio makubwa zipo changamoto ambazo bado zinatusumbua kama nchi na bado zinawasumbua watu wetu. Kusema ukweli katika hili sasa ni ushauri wangu kwamba hebu tuangalie namna kujikita katika kutatua hizi changamoto. Changamoto kubwa tuliyonayo inayowasumbua watu wetu ni changamoto ya ajira, pamoja na mafanikio yote haya tuliyoyapata, lakini ajira bado ni changamoto kubwa sana. Ukienda kule mijini, ukienda vijijini vijana wengi hawana ajira, kwa hiyo wapo tu mtaani wanaendelea kurandaranda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninajaribu kuangalia hapa katika hotuba ya Waziri wa Fedha ameonesha kwamba ni kweli Serikali imefikia lengo lake, kiasi cha ajira kimefikia lengo na kuvuka kidogo, lakini tunasema bado watu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka ni wengi zaidi kuliko ajira yenyewe inayopatikana. Ndiyo maana pamoja na furaha ambazo watu wanazo katika huduma za jamii zilizoboreshwa, lakini suala la ajira sasa ninashauri kabisa kwamba hebu tuone namna gani sasa tutaelekeza huko nguvu zetu kubwa. Hata katika hii bajeti sijaona mikakati mahsusi ambayo itaendelea kupunguza tatizo la ajira kwa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia viwanda vingi vimekufa, hivi viwanda vilikufa hasa pale Serikali ilipojitoa kwenye biashara ikaachia sekta binafsi, kama pale kwangu Musoma sasa sina kiwanda hata kimoja. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ninakuomba na hili nimekuwa nikikuambia kila mara kwamba wale wananchi wangu wa Musoma hata kile kiwanda kilipobinafsishwa kulikuwa na mafao ya wale watumishi waliokuwa wa Kiwanda cha MUTEX, sasa hili nimekuwa kila leo nikilisema na kama Serikali mmekuwa mkiahidi kwamba baada ya muda wale watu watapata haki zao, sasa wale watu wanaendelea kutaabika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba wale watu walitoka katika mikoa mbalimbali, sasa wengine hata wameshindwa kurudi makwao, sasa wanazeekea hapo, wanafia hapo lakini kila siku, leo wanaenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, kesho wanakuja kwa Mbunge, keshokutwa wanaenda kwa Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kuomba basi waweze kupata haki zao ili waweze kuendelea na maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba tu Mheshimiwa Waziri atakaposimama ni vizuri sasa unipe kauli ya mwisho hivi ninavyoenda Jimboni, basi nijue kwamba ninakwenda kuwaambia nini, kwa sababu miaka mitano yote nimekuwa nikiomba haya mafao yao, lakini mpaka leo sijafanikiwa chochote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ninaomba katika hilo aweze kulipa kipaumbele kutuambia kama watapata chochote na kama hawapati, basi ni vizuri tukawaambia na wakaweza kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, sasa kwa sababu hivi viwanda ambavyo vingi karibu vyote vimekufa bahati nzuri ile miundombinu kwa maana ya yale ma-godown yaliyokuwa ya vile viwanda bado yapo, sasa tunadhani tukiendelea tu kusema tusubirie mwekezaji aje, tumkabidhi vile viwanda, kwanza teknolojia imeshabadilika, leo viwanda ambavyo vinafanya kazi kulingana na teknolojia iliyokuja ni vile viwanda tu vidogovidogo. Kwa hiyo, ni vizuri tungeyabaini hizi godown zilizopo kwa maana sasa hivi tuseme ni godown na scrap yaliyoko mule kwa maana vile tena vimeshapitwa na wakati kulingana na teknolojia siyo viwanda tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa hivi tuhesabu tu kwamba tuna godown na yale godown sasa tuone namna ambavyo tunaweza kuwashawishi na kuwaleta wawekezaji wapya wanaoweza kuja na teknolojia za kisasa ili hizo godown ziweze kutumika katika viwanda vidogovidogo ambavyo vinaweza vikawapatia vijana wetu ajira. Tukiendelea tu kung’ang’ania tu tunasema kwamba anayekuja tunampa kiwanda na zile machine zilizomo ninadhani haiwezi kusaidia sana kwa sababu zile machine zote zimeweza kupitwa na wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwa sababu sisi kazi yetu ni ushauri na kwangu nilichotaka kukishauri au nilichoona nishauri kwenye upande huo ili tuweze kupunguza tatizo la ajira. Kwanza tunakubaliana kwamba, kwenye upande wa kilimo walau tija imeongezeka na kwa sababu tija imeongezeka basi walau kilimo kimeendelea kuchukua baadhi ya vijana wetu, lakini bado kulingana na vijana walivyo wengi hao walichukuliwa kwenye upande wa kilimo na katika baadhi ya maeneo mengine kama mifugo na uvuvi ni kwamba ile gap bado ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa ninadhani ile BBT ambayo ilikuwa inalenga tu kwenye kilimo hebu tuone namna ya kuipanua. Nami kama ni ushauri wangu sasa ningeweza kushauri kwamba, badala ya BBT ikae huku Wizarani halafu ikae kwa mfano kwenye Wizara ya Kilimo ni kwa nini tusiishushe sasa BBT, kwanza iwe katika kila mkoa, ikishakuwa katika kila mkoa kule tuwape wale Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya tuwaongezee kazi nyingine kwa maana kazi yao kubwa waliyonayo pamoja na shughuli nyingine, lakini wana jukumu la kufanya kazi ya ulinzi na usalama. Sasa ninadhani kuna haja ya kuwaongezea hilo jukumu la kuona namna wanavyoweza kuongeza ajira kupitia hii BBT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoweza kukifanya ni vizuri basi kila Mkoa wakakaa, wakabuni kwamba ni namna gani wanaweza kutumia fursa zilizopo katika namna ya kuongeza ajira. Kwanza ungeniuliza leo ningesema JKT iwe katika kila mkoa, ikishakuwa kila mkoa hawa Wakuu wa Mikoa hawa kwa sababu ni Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama tuone namna tunavyoweza kuunganisha. Kwa sababu kati ya shida moja ambayo mara nyingi tunaiona, yaani unakuta kwa kawaida mtu, mfano, njaa ikiingia tunasema Serikali ni lazima ihusike, lakini unapokuta sasa watu wanazurura, wanazembea kufanya kazi, Serikali haijihusishi katika kuwabana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ndiyo kama hayo kwamba, hata zile ajira zinazoweza kupatikana kama hatuna namna ya kuwabana yaani tutafute hizo ajira, tuzi-plan katika mikoa, lakini tuone namna ya kuzisimamia. Tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo itaendelea kupunguza hii gap iliyopo ya vijana wengi ambao wanakaa mtaani, wanarandaranda, lakini vilevile ni kwa sababu hiyo ya kukosa ajira. Kwa hiyo, niendelee tu kushauri kwamba, hii BBT tukiisogeza kule mkoani inaweza ikafanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nililishauri sambamba na hilo katika kuongeza ajira, kuna maeneo ambayo kulikuwa na fursa, lakini kama Serikali kusema ukweli wamezembea na baada ya kuwa wamezembea sasa ile athari inarudi kwa wananchi. Mfano, kwetu ambao tupo kandokando ya Ziwa, kuna hili suala la uvuvi haramu. Suala la uvuvi haramu kusema ukweli ndiyo limetupatia umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukulie mfano Kanda ya Ziwa; pale Musoma kwenyewe tulikuwa na viwanda visivyopungua vitano vya samaki, vile vyote vilikuwa vinatoa ajira kubwa kwa sababu wale wavuvi waliokuwa wanaenda kuvua walikuwa wanapata ajira, wale wachuuzi waliokuwa wananunua walikuwa wanapata ajira, wale waliokuwa wanafanya kwenye viwanda vile vya kuchakata samaki walikuwa wanapata ajira, kwa hiyo ulikuwa unakuta mzunguko wa fedha ulikuwa mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ikafika mahali kusema ukweli ni lazima tukubali ikazembea zembea hivi, vile viwanda vyote vimekufa. Leo ukienda Musoma viwanda vyote havifanyi kazi, ukienda Mwanza kuna kiwanda kimoja tu ndiyo kinafanya kazi, ukienda Bukoba hakuna kiwanda kinafanya kazi. Kwa hiyo hawa wote waliokuwa wanapata riziki hiyo sasa hivi wako tu mtaani wanarandaranda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachotaka kukishauri sasa na hiki nilishashauri mara nyingi nikasema, hebu tufike mahali tuunde mamlaka inayoweza kuangalia Maziwa pamoja na Bahari. Tukishaunda zile mamlaka zitatusaidia kulinda, kwa sababu haya tumeyaona, leo unapozungumza kwa mfano Mamlaka ya Ngorongoro unaona kabisa kwamba, yaani hao ndiyo wanasababisha mpaka ile Ngorongoro inaendelea kuwepo. Kwa hiyo ziko mamlaka kama hizi zote leo ukitaja yoyote ilimradi ni mamlaka ni kwamba kazi ya kwanza inajitahidi ku-protect kile ilichonacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapokuja kwenye habari ya Ziwa ambapo ndiyo kuna uchumi mkubwa wale samaki hawana mwangalizi, kwa hiyo watu wanavua tu hovyo hovyo. Ziwa kwa sababu limeunga katika nchi, kwa mfano lile Ziwa Victoria ziko nchi zisizopungua tatu tuna-share pale. Kwa sababu hakuna mamlaka hata namna ya kudhibiti kwamba hili ni la upande huu, hili ni la upande huu na yenyewe haipo, kwa hiyo, suala la uvuvi haramu linaendelea kutupatia taabu kubwa na kwa kufanya hivyo ndiyo maana watu wetu wanaendelea kuwa maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa na hili suala la mamlaka ninakumbuka hata Waziri aliyekuwepo alikubali kwamba yuko tayari sasa kwa ajili ya kuileta hiyo sheria ili tuweze kuipitisha, lakini mpaka leo wala hakuna anayeizungumzia. Kwa hiyo maana yake ni kwamba, Serikali ni kama inakwepa jukumu lake badala isimamie ule uvuvi haramu uishe sasa imeendelea kuwa na hali hiyo kwa hiyo matokeo yake shida zimeendelea kutuandama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la Balozi zetu. Tunatambua kwamba, mojawapo ya zile Balozi zetu wanaangalia Diplomasia ya mahusiano, vilevile kazi kubwa nyingine wanayopaswa kuangalia ni namna ambavyo watu wetu wanaweza wakapata fursa zinazopatikana katika nchi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuamini wako Watanzania wengi wanazo fedha, wangependa kuona fursa zinazopatikana ili waweze kufaidika nazo, lakini kwa bahati mbaya sana ni kwamba, kwa sababu unakuta Watanzania wengi ambao wana fedha angependa kwenda kwenye nchi zingine kwa mfano kama India, kama China, lakini anashindwa aanzie wapi. Kwa hiyo, kwa sababu anashindwa aanzie wapi unakuta tu akienda anaenda kufanya biashara ya trading ile ya kwenda, ataenda pale Guangzhou atanunua mali, atakuja hapa anauza biashara imefanyaje, imeisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mabalozi wetu, ofisi zetu za Ubalozi zingekuwa active wakawa, kwa mfano wale watu wa Business kile Kitengo cha Business Attache kikafanya kazi vizuri, maana yake ni kwamba kama Balozi wetu wa India angeweza kuwa anatueleza fursa zinazopatikana India na akaangalia ili watu wetu kila anapokuja huku anasema na anaweza kupata nafasi ya kukaa nao, lakini hata watu wetu wakienda kule waweze kupokelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalisema hivyo kwa sababu gani, kwa nafasi yangu kama mjasiliamali nimezunguka nchi nyingi na kila ninapoenda nimekuwa ninaenda hata katika Balozi, yaani ukifika pale unamwambia Balozi unakuja, ukifika pale anachoweza kufanya ni kukukaribisha, atakusikiliza halafu, yaani atakupa msaada mdogo sana. Kwa hiyo, ninadhani hilo nalo ni changamoto kubwa tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi hapa mimi nilienda hapa jirani tu hapa Comoro, nilipoenda pale Comoro kwa bahati nzuri kwa sababu kwa bahati mbaya ile nchi hawajui Kiingereza na hawajui Kiswahili, wanajua Kifaransa na hiyo lugha yao ya Kikomoro. Kwa hiyo, nililazimika kabla ya kwenda nimtafute Balozi, baada ya kuwa nimempata Balozi ninashukuru sana kwanza kwa mapokezi aliyonipatia, siyo hilo tu, nilipofika kule alinipa usaidizi wote na baada ya kunipatia ule usaidizi, umenifanya nikaangalia fursa zilizopo kule na sasa nikaona kumbe kama Mabalozi wote wangekuwa wanafanya hivyo, maana yake ni kwamba katika kukuza uchumi wa nchi yetu, Watanzania wangeweza kufaidika kupitia hizo Balozi zetu zilizoko katika nchi mbalimbali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE (MHE. COSATO D. CHUMI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Muda wake ulikuwa umeisha alikuwa anamalizia. Mheshimiwa malizia point ya mwisho.
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nichukue nafasi hii kusema kwamba, tunadhani kuna haja ya Balozi zetu nazo zikiwa active zitasaidia sana katika kupunguza hili tatizo la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)