Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba nichukuwe nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na uhai leo hii tumeweza kusimama hapa kuchangia Wizara yetu ya Kilimo.
Pili, nichukuwe nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya ya kuhakikisha Watanzania ambao sehemu kubwa ya maisha yetu yanategemea kwenye kilimo.
Tatu, nichukue nafasi hii kupongeza Wizara, ndugu yangu Mheshimiwa Bashe, Mheshimiwa Silinde pamoja na Katibu Mkuu na timu nzima. Kwa kweli ninataka niwathibitishie kwamba wamefanya kazi kubwa sana. Kazi waliyoifanya kwenye sekta ya kilimo; hii Wizara ndiyo tulikuwa tunaona kuwa ni ile Wizara ambayo tunaona kwetu kwamba ilishindikana. Sasa tangu mwaka 2021 mpaka sasa mapinduzi yaliyofanyika kwenye hii Wizara ni mapinduzi ambayo hatukuyatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitawatolea mifano michache tu na ninachukua sample ya jimbo langu na wilaya yangu ya Kaliua. Hadi mwaka 2021 sisi ni wakulima wakubwa wa tumbaku, na Wilaya ya Kaliua ndiyo inayoongoza kwa uzalishaji wa tumbaku katika nchi yetu ya Tanzania, tunazalisha takriban kilo milioni 30.2. Tumbaku hii nyingi na ndiyo tunayoitegemea wananchi wa Tabora, wananchi wa Kaliua na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini ambacho tumefanya? Kabla ya mwaka 2021 tulikuwa tunapewa ukomo wa kulima kwamba wewe mkulima wa tumbaku mwisho wako wa kuzalisha ni kilo 1,000; mwisho wako wa kuzalisha ni kilo 2,000 na mwisho wako wa kulima ni kiasi fulani. Unakuwa na maeneo makubwa lakini umepewa ukomo kwamba huwezi uka-access kulima kadri ya mtaji wako, huwezi uka-access kulima kadri ya uwezo ulio nao. Sasa haya yote yamekwenda kuwa historia na ndiyo maana ninasimama kifua mbele kama Mbunge, kama mwakilishi wa Jimbo la Kaliua kuwaambia Watanzania kwamba mapinduzi yaliyofanyika kwenye sekta ya kilimo hususani kwenye zao la tumbaku ni makubwa sana ambapo Mheshimiwa Waziri anatakiwa kupewa makofi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ukiachana na ukomo, upatikanaji wa mbolea, huko nyuma ilikuwa inafikia msimu unaanza tayari tumetoka kwenye mabedi, tumekwenda kwenye masuala ya tumbaku imeshapanda ndipo mbolea inakuja huku tumbaku ikiwa imekwishaanza kuharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, jambo hilo sasa limekuwa ni historia, kwa sababu mpaka sasa mbolea inayoendelea kuanzia msimu wa mwaka huu mwezi wa nane, wa tisa na kuendelea tumeambiwa mbolea ipo. Hivyo niwathibitishie wakulima kwamba wakae mkao wa kutulia, mbolea ipo, walime tani yao. Kile kizuizi cha kulima kwamba watalima na nini biashara hiyo imeshakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni kuhusu bei ya tumbaku; hapa kwenye bei ya tumbaku ilikuwa historia. Sasa ninakuthibitishia kwamba jana nilikuwa ninapokea simu za wananchi wa Usinge, Kazaroho, Igwisi na Zugimlole wameuza tumbaku, wameuza hadi dola tatu. Dola tatu tunaongelea takribani shilingi 7,000. Hii kitu imekuwa ni common kwao, kwa nini? Ni kwa sababu Mheshimiwa Bashe, Waziri wetu mchapakazi ameweza kufungua channel za kuhakikisha kwamba kampuni za kutosha za tumbaku zinafanya kazi nzuri sana kule Kaliua, zinafanya kazi nzuri sana kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri aendelee kushirikiana nao kuhakikisha kwamba masoko yanayoendelea sasa hivi wauze katika bei ambazo ni nzuri kama walivyoanza ili kuhakikisha sisi tunapokwenda kule, Mama Samia anapozunguka ni makofi, ni kura za kutosha, CCM inasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningetaka kupongeza kwenye kilimo cha tumbaku reference ambayo mimi Kaliua nimesimama kum-support Mheshimiwa Waziri na kumpongeza ni hapa, wakati Mheshimiwa Rais anaingia mwaka 2021 tulikuta bajeti kwa mfano ya Kaliua ilikuwa ni shilingi bilioni 3.2. Sasa ninaongea bajeti ya mapato ya ndani ya Kaliua imekwenda hadi shilingi bilioni 8.9, hebu mpigieni makofi Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, ukipandisha own source ikapanda kwa kiwango hiki cha shilingi bilioni 8.9 tafsiri yake ni kwamba ndiyo maana mnaona sisi Kaliua tunao hata uwezo wa kujenga vituo vya afya kwa fedha ya ndani. Kwenye jimbo langu vinajengwa vituo vya afya viwili, kwenye jimbo la mwenzangu Ulyankulu kule vinajengwa, haya ni mapato ya ndani. Hii yote ni faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo kampuni zimefanya vizuri zaidi, zimeweza hata zenyewe kutoa CSR na kujenga vituo vya afya na ndiyo maana tunawaambia kwamba kwa kweli sekta ya kilimo imepata mwenyewe. Kama ni upele, Kaka Bashe yeye ndiye mkunaji wa upele anayestahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninasimama hapa, leo watashangaa Kwezi mbona anapongeza sana, ndugu zangu ninataka niwathibitishie kwamba hii BBT sio kitu cha mchezo, hii ni sehemu kubwa sana ya ajira. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, DC wangu Ndugu Gerald Mongela amepokea matrekta ya kutosha Kaliua. Tulitenga hekari 16,000; kwa kilimo tuna hekari 6,500 na 10,000 ni kwa ajili ya mifugo. Vijana kule wapo tayari, wapo tayari kwa maelekezo na pia wapo tayari kufanya kazi. Sisi kama mnavyotujua, mzigo mzito tunao na tunapiga kazi, hatuna cha kuchelewa nacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ambalo nilitaka niliongelee; hili jambo ni ombi; ombi langu kubwa ni kwamba kuna kitu hapa zile AMCOS. Mimi kule kwangu anajua kabisa jimbo lile lina watu takribani 400,000 na wengi ni wakulima 90% wameniomba AMCOS takribani 14; na hii ni kwa sababu gani! Unakuta kwamba vijana wetu wamemaliza darasa la saba, wengine wamemaliza form four na wengine wamemaliza form six. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba unaweza ukaangalia ili kutusaidia AMCOS Kaliua. Hiyo ni special request ya kwangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningeweza kukupongeza ni suala la Benki ya Ushirika. Kwa kweli hapa umevunja record. Ninakuomba hata wakija wale wakulima binafsi wenye uwezo hakikisheni mmeweka programu nzuri sana kuhakikisha hawa wakulima tayari wana uwezo wa kukopa kupitia vyama vyao vya ushirika, kupitia vikundi mbalimbali, lakini hata mmoja mmoja kwa sababu ni wanaushirika wanaotambulika na wana uwezo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaweza kumalizia hapa ni jambo kubwa sana ambalo nitapenda kuliongelea. Ninaziomba sasa kampuni za tumbaku, kwa kweli Mheshimiwa Bashe ninaomba zaidi wajikite na wenyewe kuwekeza katika maeneo yetu. Maana yake kama maghala yanavyojengwa sasa hivi, wanaendelea kukuza uchumi wa maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Engineer Ezra pale ameomba akasema liko moja. Mimi kwangu yako mengi, lakini ninatamani sana hata twende kwenye kujenga kiwanda cha tumbaku ili tuwapunguzie gharama za kusafirisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alikuwa na idea nzuri sana, tunajua Morogoro mambo ni mazuri, lakini in future hebu jaribu kuangalia kwenye Mkoa wetu wa Tabora tunaweza tukaenda kiasi gani kwa sababu tumbaku ndiyo iko pale na mambo mazuri yako pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa ambalo nilitaka kusisitiza ni ruzuku. Ninakushukuru kwa ruzuku, wananchi wanaendelea kulipwa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja kwa 100%. Ahsanteni sana. (Makofi)