Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya. Niwashukuru na wenzangu humu wote tuliomo katika Bunge hili Tukufu, wamekaa na kutulia ili kusikiliza mpango unaoendelea sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwamba bajeti hii ni bajeti yetu ya mwisho kwa kipindi hiki. Tukimaliza kufunga kwa sasa hivi kutakuwa hakuna bajeti tena. Kwa hiyo, kwanza nachukua fursa hii ya kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wangu wote waliomo humu ndani. Ninawashukuru sana kwa kukaa pamoja, kwa kutulia na kuweza kufanya kazi kwa pamoja. Ninashukuru sana na tuendelee kukaa nao pamoja ili tuweze kujenga mustakabali wetu wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri wangu wa Fedha pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa wanazozifanya katika Serikali yetu hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wanafanya kazi kubwa na leo hii wapo mezani ili kupitisha Bajeti yao ya Mpango katika Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Rais wangu Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake anazozifanya, anafanya kazi kubwa ambazo kazi hizo zinaonekana Tanzania nzima pamoja na Serikali zake nyingine. Kwa hiyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea sasa ili na mimi sasa hivi niweze kuishauri Serikali yangu. Nimeliona jambo kubwa katika Jiji hili la Dodoma: Jiji la Dodoma hivi sasa limekuwa linakua kwa kila hatua, kwa kila wakati, kwa kila saa. Kwa kipindi cha mwaka 1990 na 2014 sivyo ilivyo sasa hivi Dodoma. Sasa hivi imekua sana. Kwa hiyo, katika kutazama kwangu, ushauri wangu nimesema niulete katika mpango ili iangalie nayo Serikali yangu. Je, hili nitakalolisema wataweza kulifanya kwa sababu Serikali yetu ina miradi mikubwa mingi sana. Miradi hiyo inaendelea kufanya kazi lakini na sasa hivi ninataka nilitie mkazo hili ili liweze kufanyika katika Jiji letu hili la Dodoma na hii pia ni mradi huu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dodoma hivi sasa limekuwa kubwa na kuna msongamano wa barabara na magari. Yaani sisi tukitoka hapa sasa hivi Bungeni, kama watatoka Waheshimiwa Mawaziri wao mwanzo, basi uhakikishe nyumbani unaweza ukafika saa mbili, tatu kutokana na msongamano ulioko huko nje barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ninamwomba Mheshimiwa Waziri wangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu pamoja na Naibu wake walichukue hili suala, tuweze kujengewa barabara ya juu ile flyover kama inawezekana iwe kama Dar es Salaam kwa sababu hili jiji kubwa na kila siku linakua. Je, tukijengewa hii barabara huku (flyover) tukapita kule juu na wengine wakapita chini, basi ule msongamano unakuwa mdogo. Hauwi mkubwa kama ulivyo hivi sasa. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali yangu hili suala na Serikali yangu sikivu kama inawezekana nalo pia lifanyiwe kazi katika Jiji la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ninachangia kuhusu Mkoa wangu wa Kusini Unguja. Mkoa wa Kusini Unguja ni mkoa wenye wilaya mbili. Mkoa ule umejaa utalii baina ya Kati na Kusini lakini mie nitazungumzia kuhusu suala la askari walioko kule Kusini Unguja hasa hususan kuhusu zile nyumba. Nyumba za Polisi zimeanza kujengwa hiki kipindi cha mwaka wa pili bado hazijamalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipiga kelele kuhusu vituo lakini vituo tayari vimemalizika na hivi sasa vinafanya kazi vizuri lakini nyumba zao askari Kusini Unguja zinajengwa kwa kusuasua na hatujui lini nyumba zile zitaweza kumalizika. Ninaishauri Serikali, zile nyumba zimalizwe haraka ili wale askari wetu waweze kupata sehemu sahihi ya kuweza kukaa ili wafanye kazi vizuri na ukizingatia Mkoa wa Kusini ni mkoa wa watalii, lakini ikiwa wanakaa kule bado wakati wa utalii unapopamba moto, wako kule basi watazidi kujenga usalama katika kile kijiji chetu cha kule Kusini Unguja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo mawili. Sina mambo makubwa sana isipokuwa hayo. Ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nawapongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu ingawa wanazungumza huko, lakini ninajua wamesikia. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)