Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii nami nimshukuru Mungu kwa kuniwezesha jioni ya leo kuweza kuchangia hotuba za Waheshimiwa Mawaziri hawa vijana wawili; Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha, katika mustakabali mzima wa bajeti yetu ambayo tunaendelea nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika maeneo matatu. Kwanza ni kuishukuru Serikali kwa kile ambacho imefanya katika maeneo yangu ambayo ninawakilisha. Pili, nitapenda kutoa changamoto kadhaa ambazo tunaziona, lakini mwisho nitawashauri Waheshimiwa Mawaziri hawa vijana katika kuhakikisha basi tunakwenda mbele vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia Serikali hii ya Awamu ya Sita ilivyofanya kazi nzuri kwa kipindi chake chote. Katika elimu, shule nyingi katika maeneo yetu ya vijijini zimejengwa na zingine ni mpya kabisa. Hakukuwa na uwezekano wa wanafunzi wa wakulima na wafugaji kupata elimu, lakini leo hakuna changamoto hii tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu tumejenga shule mpya 30 katika kipindi cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia. Maana yake ni sifa za kipekee mno kuwahi kutokea. Mwaka 2020 tulikuwa na shule 40 tu katika Jimbo zima la Manyoni Magharibi ambapo sasa ni Jimbo la Itigi, Halmashauri ya Itigi lakini kwa miaka minne tumejenga shule zaidi ya 30. Wananchi wa Itigi wamenituma humu nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, lakini na waliomshauri katika hili wakiwemo Mawaziri hao vijana katika kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika afya, tumejenga zahanati katika maeneo yetu, tumejenga vituo vya afya na leo tunajenga hospitali ya wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji hivyo hivyo; vijiji vyetu vingi vinaenda kupata huduma za maji japo ziko changamoto za hapa na pale. Kama nilivyosema, nalo nitakuja kulichangia lakini miundombinu, tunaunganishwa Mkoa wa Singida na Mkoa wa Mbeya kwa barabara za lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi alisimama kidogo na changamoto hizi zilishaelezwa, tunaamini tunapoenda mwishoni hapa basi makandarasi huyo atapewa pesa ili arudi kumalizia kipande hiki cha kilomita 56.6 ambazo tunaamini zikishafunguka tayari central corridor kwa upande wa Singida kuunganisha na southern corridor na northern corridor upande wa Mkoa wa Simiyu na Mara na sisi tutakuwa tumefaidika kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nishati vijijini, tumeshuhudia vijiji vyote nami kwenye jimbo langu vikipatiwa umeme na sasa wanakwenda vitongojini, lakini kama nilivyosema, kuna changamoto chache ambazo tunaomba tuwaambie ili wakazifanyie kazi. Katika vijiji vyetu, Mheshimiwa Rais wetu alitangaza Royal Tour na sisi watu wa Itigi tunapakana na mapori ya akiba ya Muhesi na Rungwa. Kwa kiasi kikubwa kumekuwa na manufaa makubwa, lakini zipo changamoto za wanyama wakali na waharibifu ambao wanapita kwenye maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba ni corridor za Wanyama, lakini uhalisia ni kwamba inawezekana hawa wanyama inawezekana wameongezeka kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, tunaomba juhudi za makusudi zifanyike ili kuwanusuru wananchi hawa ambao wengine wanauawa na wengine wanaliwa mazao yao kutokana na wanyama hawa kuwa wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha katika ukurasa wake wa 47, amezungumzia kilimo ambacho kimeongezeka kwa kiasi kikubwa. Tulikuwa na tani 17,148,290 mwaka wa fedha 2021/2022, lakini mwaka wa fedha 2023/2024 ziliongezeka kufikia tani 22,803,316. Maana yake ni nini? Kwamba uwekezaji wa Serikali katika sekta ya kilimo unaonyesha kuwa na manufaa makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ya kilimo kadri inavyoongezeka basi tunategemea kwa muda mfupi ujao iweze kuakisi lakini ongezeko hili la kujitosheleza kwa chakula hiki kwa 128% kwa nchi kama Tanzania ambayo ni hub ya chakula, bado tunatamani kuona inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko hapa tulipo. Kwa sababu ongezeko la bajeti yetu kwa upande wa kilimo ni kwa zaidi ya 300%. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa madini nako kuna ongezeko kidogo. Tulikuwa na asilimia sita nukta nane tu sasa tumefika kwa 10%. Bado natamani kuona tunakwenda mbele zaidi kwa sababu bajeti ya upande wa madini nayo imeongezeka kwa zaidi ya 600%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kiasi fulani tunawaomba Waheshimiwa Mawaziri hawa vijana ambao wameaminiwa na Mheshimiwa Rais waweze kuikwamua nchi hii kupitia maeneo haya ambayo ni rasilimali za nchi yetu. Tunajua uwezo wako mkubwa wa kusimamia, lakini tunafahamu namna ambavyo wanapaswa kuongeza jitihada na ubunifu mkubwa zaidi kuisaidia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo jambo mahsusi sana, katika nchi yetu tuna Gesi ya CNG, lakini kuna mchakato unaoendelea wa LNG ambao ninaamini mchakato huu utatutoa katika manunuzi makubwa ya mafuta ya petroli. Ununuzi wa mafuta ya petroli unagharimu kiasi kikubwa sana cha mapato yetu kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaweza kulimaliza hili kwa sababu gesi iko ndani, hata kama kuna changamoto zozote na wale wanaowekeza, lakini ninahakika kwa sababu jambo litakuwa ndani itakuwa ni rahisi sana, hatutakuwa na uagizaji mkubwa wa mafuta ya petroli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia inahama kutoka kwenye mafuta kwenda kwenye vyombo vinavyotumia umeme. Sisi tunapoendelea ku-delay, tutakuja kuachwa kwa sababu dunia sasa mataifa yanayoendelea yanatengeneza vyombo vya umeme ikiwemo magari, lakini na vyombo mbalimbali vya matumizi ya nyumbani na matumizi ya miundombinu vinatumia umeme. Kwa hiyo, basi tutoke hapo tulipo tuweze kusogea haraka ili tukimbizane na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Nickel, watu wa Wizara ya Madini wakimbie na hili. Nickel ndiyo inayotengeneza betri hizi ambazo zinatumika kwenye magari ya kisasa na kichanganyio kingine ni cobalt. Inawezekana hatuna cobalt ya kutosha kwa hapa Tanzania, lakini nchi jirani zinazotuzunguka cobalt iko nyingi sana na uhitaji wa cobalt ni kiasi kidogo sana na cobalt kwenye matumizi haya hata gharama zake siyo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapo-delay kuingia katika LNG, tunapo-delay kuingia kwenye matumizi ya kutengeneza betri za umeme, tutajikuta tunaendelea kuwa wategemezi wa mafuta wakati ambapo dunia inakimbia na inatoka huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kuishauri Serikali yangu. Kule vijijini kwetu kunapokuwa na miradi hii ambayo inafanyika na miradi ya Serikali ukiwemo ujenzi mbalimbali wa Barabara, lakini na miradi ambayo inatekelezwa na Serikali. Basi vijana wetu walioko kule vijijini waweze kuhusika kwenye kazi zile za nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na changamoto sana za ajira za nguvu kwa sababu watu wetu wamekuwa wanadhani labda nazo zinahitaji mchakato mkubwa. Tumeona kwenye bomba la mafuta, ajira hizi zimehusishwa kwenye vijiji. Ninaomba mfano huu uende katika maeneo mengine ili wananchi wetu waweze kupata hizi ajira za nguvu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilikuwa na machache sana ya kuchangia katika eneo hili, lakini pia kuna jambo ambalo ardhi zilizotwaliwa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa (SGR). Wananchi wale katika eneo langu la Itigi hawajalipwa baadhi yao. Ninaomba basi mchakato huu nao uende haraka ili wananchi waliopisha ujenzi wa miundombinu hii waweze kulipwa ili wajue Serikali yao sasa nao inawajali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)