Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kavejuru Eliadory Felix

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na mimi kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia kwenye hoja hii ya Wizara ya Kilimo. Mimi pia niungane na wasemaji walionitangulia kuwapa pongezi sana sana Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe na Naibu wake Mheshimiwa David Ernest Silinde, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu. Nimpe pongezi kubwa sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya dhati ya kuamua kufanya mapinduzi ya kilimo hapa nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu unakwenda kujikita kwenye hotuba, ukurasa ule wa 152 na nilikuwa ninajaribu kuulinganisha na ukurasa wa 129, hasa nikizingatia bajeti ya mwaka 2025 ambayo hasa imelenga kwenye ukuaji wa sekta ya kilimo kwa upande wa mazao ya kilimo kufikia asilimia tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeliangalia jedwali lile namba tano la ukurasa 152, kwanza nitoe pongezi kubwa sana kwa wakulima wa mazao ya biashara, hawa wamekuwa na mchango mkubwa sana wa kutuingizia fedha nyingi za kigeni, niwapongeze wakulima wa korosho, pamba, pareto, kahawa, tumbaku, chai, mkonge, sukari na kakao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo bado kuna jitihada inayohitajika kwenye mazao haya ya biashara. Yapo mazao matatu ambayo nimeyaangalia kwenye jedwali hilo, nikiangalia malengo yake ni madogo sana. Zao la kwanza nimeangalia zao la kahawa, lengo la bajeti ya mwaka 2025/2026 ni kutoka sasa kwenye uvunaji wa kahawa ambao tulipata tani 86,366; kwa kakao kutoka tani 13,652 kufikia tani 15,000, na zao la pareto kutoka tani 3,327 kufikia tani 5,000. Ninaomba nitolee mfano tu kwenye zao la kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo nchi ambazo uchumi wake umebebwa na kahawa, kidunia nchi ya kwanza ni Brazil, ya pili ni Vietnam na ya tatu ni Colombia. Ukija kwenye Bara la Afrika, pamoja na kwamba sisi Tanzania ni nchi ya tatu, lakini nchi inayoongoza katika uzalishaji wa kahawa ni Ethiopia. Ethiopia sasa hivi kwa mwaka inazalisha tani 472,000. Nchi ya pili ni Uganda ambao wamefanya mapinduzi makubwa sana. Kwa mwaka 2021 Uganda walikuwa wanazalisha kahawa tani 242,000 lakini kwa msimu uliopita wameweza kupata uzalishaji wa tani 384,000. Sisi tumepiga hatua, tumetoka kwenye 51 tumefika 81. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ninashangaa, sasa tunataka 81 tunataka kuongeza tu tofauti hiyo ya 85,000 ni kama 4,000. Mbona ni kidogo ilihali hili ni zao muhimu linalotuingizia fedha za kigeni? Isitoshe linalimwa katika mikoa 16 hapa nchini. Ukilinganisha eneo ambalo linafaa kwa ajili ya kilimo hapa kwetu Tanzania ni kubwa mara tatu zaidi ya eneo ambalo linalimwa zao la kahawa nchini Colombia. Hata eneo ambalo linazalishwa kwa kahawa nchini Ethiopia ambayo ndiyo nchi namba moja katika Bara la Afrika ni dogo ukilinganisha na ardhi yetu ambayo inafaa kwa ajili ya kilimo cha kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Serikali iangalie kwa dhati kwa sababu hili ni zao ambalo linatuingizia fedha nyingi. Sasa hivi soko lake limeendelea kupanuka na bei yake ipo juu, linatuingizia fedha za kigeni. Kunahitajika mkakati mahsusi sasa wa kutoka kwenye hizi tani ambazo zipo chini ya 100,000 twende angalau hata kwenye 200,000. Majirani zetu ambao ni wanne wa Kenya kwa kipindi kile cha mwaka 2021/2022 walikuwa na uzalishaji wa tani 34,000; lakini sasa hivi wapo wanatukaribia, na wana malengo ya kuvuka zaidi ya hii 85 ambayo sisi tumepanga.

Kwa hiyo, ninaomba jitihada mahsusi iwekwe kwenye mazao haya ya biashara hususan biashara ambayo tayari inalimwa kwenye mikoa 16. Itatoa ajira nyingi sana na itawanyanyua maskini wengi na kupunguza umaskini uliokithiri katika jamii zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeomba kwamba pamoja na jitihada na ruzuku ambayo imekwishaendelea kutolewa basi ruzuku kubwa ya Serikali ilenge na jitihada kubwa ziende kutolewa ikiwa ni pamoja na pembejeo na kilimo kwenye mazao haya ya biashara ili tuendelee kupata fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niishukuru Wizara, nimeona kwenye bajeti hii inayokwenda kujengewa nyumba nne kwenye Kituo cha TACRI cha Mayaya. Ninawapongeza watumishi wote wa TACRI katika Kituo cha Mayaya, wanafanya kazi kubwa sana. Msimu uliopita wamezalisha miche mingi ya kahawa na yote ilichukuliwa na wakulima kwa muda mfupi. Ninaomba waongezewe bajeti yao ili wazalishe miche mingi ya kahawa na iliyo bora. Sasa hivi wakulima wa kilimo cha kahawa nchini kote wamehamasika kulima kilimo hiki. Kwa hiyo, tunaomba jitihada ziongezeke kwa ajili ya kuongeza miche bora, ikiwa ni pamoja na pembejeo za kilimo zije kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ambapo ni kukumbushia tu, ni kilimo cha tangawizi. Katika Jimbo langu la Buhigwe kwenye bajeti mbili zilizopita Wizara iliahidi kutujengea miundombinu ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umeisha tafadhali.

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaunga mkono hoja. (Makofi)