Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kupata nafasi jioni hii ya kuweza kuchangia hoja iliyopo mezani. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai wa kusimama kwenye Bunge lako Tukufu kwa siku ya leo. Pili, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utashi wake na hiari ya makusudi ya kuhakikisha kwamba bajeti hii inatengenezwa vizuri kwa niaba ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa ninaunga mkono hoja iliyopo mezani kwa asilimia mia moja, lakini la pili, ninawapongeza Mawaziri wote wawili na watumishi waliopo chini yao wote kwa kutengeneza bajeti nzuri yenye mtazamo wa kuchechemua uchumi wa nchi yetu na kuhakikisha kwamba maendeleo yanatokana na bajeti iliyopangwa kwa wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaelekea sana kwenye ushauri upande wa kilimo. Kwanza tunashukuru sana bajeti hii kwa kumwangalia mkulima kwa kumweka kipaumbele. Moja ni kuondoa kodi kwenye viuatilifu ambavyo vinatumika kwa wakulima wetu. Hili jambo tutaliona ni dogo, lakini ni kubwa sana kwa wakulima wetu kwa sababu hivi viuatilifu ndivyo vinavyowafanya wakulima waweze kupambana na wadudu mbalimbali ambao wanaathiri mazao yetu ili kupata mazao zaidi. Kupunguzwa kwa kodi hii kutasababisha mkulima kuwa na purchasing power kubwa ya kupata hivi viuatilifu hatimaye kufanya matumizi yawe makubwa zaidi na kumfanya avune zaidi na Serikali kuvuna zaidi kutokana na kodi na tozo mbalimbali zinazotokana na mazao ambayo wakulima wanazalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo kwa kweli ni faraja kubwa na ni hiari ya Mheshimiwa Rais wetu, sambamba na hii ni pamoja na kuendelea kutoa ruzuku kwenye mbolea kwa wakulima. Hili jambo bado ni kubwa linaendelea kuhakikisha kwamba uzalishaji unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee tumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa sisi wananchi tunaotoka kwenye ukanda ule unaozalisha korosho. Tunamshukuru sana kwa hiari yake na kuamua kutoa export levy kwenye zao la korosho kwa 100%, tunashukuru sana. Kwa sababu hiyo ndiyo maana mpaka sasa tumeona uzalishaji wa korosho umetoka tani 323,000 mpaka kufika tani 528,000 ambayo ni zaidi ya 60% ya ongezeko lililotokana na uwezo wa Serikali kuwahudumia wakulima wetu kwa kuwapa pembejeo za sulphur na maji bure. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, Mungu aendelee kumpa maisha marefu ili aendelee kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa ushauri kwenye mazao mengine ya biashara, kwa mfano ilivyo kahawa, tumbaku na mazao mengine kama kokoa, waige mfano wa korosho. Tulivyoanzisha export levy 2009, ninadhani kama 2008 kama 2009 ilikuwa ni mahususi kwa ajili ya kuchechemua uzalishaji wa korosho pamoja na kuwezesha kuanzisha viwanda vya ubanguaji kwenye nchi yetu ili korosho iweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili jambo limeonesha kuleta mafanikio kwa sasa kwa sababu uzalishaji umeongezeka na dhamira ya Serikali kuanzisha kongamano la korosho katika Halmashauri ya Nanyamba ni dalili ya kutosha kabisa kuonesha kwamba export levy imeleta matunda makubwa kwa wakulima wa korosho. Kwa hiyo, si dhambi kwenye mazao mengine wakaingiza mtindo huu au wa namna yoyote ile ya kuhakikisha kwamba na wenzetu hawa wanakwenda kwenye export levy itakayosaidia kuzalisha zaidi kwa sababu sehemu ya export levy kwa 100% inaenda kusaidia wakulima wenyewe kwa ajili ya kusaidia mashamba yao pamoja na wataalam kwenye eneo linalohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuiga hilo suala la export levy si dhambi nao wenzetu wakaendelea kuiga huu mtindo wa stakabadhi ghalani. Ninaomba nikufahamishe, kwenye maeneo yote yanayolima korosho, yanayotumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwenye ufuta na mbaazi sasa hivi hatutamani kurudi nyuma kwenye mfumo ule wa zamani. Imeonesha mafanikio makubwa hasa kwenye upande wa kupanda bei na pili kwa halmashauri zetu za wilaya kwa kupata mapato ya uhakika zaidi kuliko ilivyo kwenye mfumo wa kiholela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali, kama halmashauri hizi za maeneo haya zinafaidika sana kwenye Mfumo huu wa Stakabadhi ya Ghalani kurahisisha upatikanaji wa ushuru wao kutoka kwenye mazao haya na kodi mbalimbali za Serikali. Kuna mazao ambayo wenzetu yamekuwa kama mazao ya biashara kama ilivyo Rukwa, Sumbawanga, Songea na Mbinga, zao la mahindi. Zao hili limekuwa ni zao la kibiashara kwao kwa sababu linasababisha wao kuwa na kipato kikubwa kutokana na mahindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mfumo wa kununua NFRA umeonesha udhaifu wa hali ya juu. Moja ya udhaifu wa mfumo ule sasa hivi wakulima ndiyo wanauza mahindi kwa watu wa katikati. Kwa hiyo, bei anayoitoa NFRA kwa wanaouza mahindi kwao wanapata watu wa kati, wakati wanapeleka fedha maana yake mkulima hana mazao kwenye maghala yake, mazao yote yapo kwa wafanyabiashara wa kati. Kwa hiyo, faida ile ya kilo shilingi 700 mpaka 800 kwenye upande wa mahindi inakwenda kwa wafanyabiashara wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali, lengo la Serikali ni kuwasaidia wakulima, basi hii Mifumo ya Stakabadhi Ghalani kwenye maeneo yale yenye mazao mahususi yanayowasaidia wakulima kama mazao ya kibiashara ni vyema basi stakabadhi ghalani ikaelekea kusaidia wakulima wetu ambao watapata bei ile nzuri ya moja kwa moja kutoka kwa wanunuzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si jambo rahisi kama mlivyoona wakati wa miaka ya nyuma, tunalumbana hapa kwenye ufuta, kwenye maeneo mengine lakini leo wanachekelea; kwenye kokoa leo wanachekelea; kwenye kahawa leo wakulima wanachekelea; basi ile itatusaidia na hao wa mahindi, maharage na mazao mengine ambayo yanalimwa kwa wingi kwenye maeneo haya wakapata bei nzuri; na wakulima wale wakaendelea katika kuhakikisha maisha yao yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwenye kilimo ni suala la umwagiliaji. Tunashukuru bajeti ya umwagiliaji imeongezeka, lakini tumwombe Waziri wa Fedha, tuna mipango mizuri, Mheshimiwa Bashe ana mabwawa chungu mzima hapa, ameyataja kuna miradi zaidi ya 900 ya umwagiliaji, shida pesa haiendi kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umwagiliaji ni muhimu sana, tukiuanza mradi leo ukaishia katikati, mvua ikinyesha maana yake zitakapokuja hela unaanza upya, kitu ambacho kinarudisha nyuma miradi hii ya umwagiliaji. Inakuwa kila siku tunapeleka hela lakini miradi haiendelei. Kwa hiyo, tunaomba Waziri wa Fedha, wewe ni msikivu, unamsaidia sana mama kuhakikisha kwamba tunataka kuendelea kuzalisha zaidi, sasa tunaomba fedha za umwagiliaji ziende kama zilivyokusudiwa kwa sababu lengo la umwagiliaji ni kuhakikisha kwamba mkulima analima mwaka mzima na kuzalisha zaidi bila kutegemea mvua na ili Serikali iweze kupata fedha na mapato zaidi kutokana na tozo na kodi mbalimbali zinazotokana na biashara ya mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa siitendei haki Wilaya ya Tunduru na Jimbo la Tunduru Kusini kwa ujumla pamoja na Wilaya zote na Mikoa ya Kusini. Kuna suala la ujenzi wa SGR. Kwenye mipango hii, bado tunakuwa na kizungumkuti cha kutengeneza SGR kutoka Mtwara – Tunduru - Mbamba Bay pamoja na matawi yake Nchuchuma na Liganga. Wakati tayari Serikali imeonesha dhamira yake ya kuanzisha Mradi ule wa Liganga na Mchuchuma kwa kuanza kulipa fidia kwa waathirika, tunaomba sana, miradi hii ni pacha ili iende sawasawa lazima iendene sambamba na ujenzi wa reli ya SGR kutoka Mtwara - Tunduru mpaka Mbamba Bay ili iweze kusaidia, itakapokamilika itasaidia Mradi wa Liganga na Mchuchuma kusafirisha zile bidhaa kwa urahisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, hii mipango yetu tuamue kama tulivyoamua kwenye SGR reli ya kati, kama tulivyoamua kwenye standard gauge na kama tulivyoamua kwenye Daraja hili la Magufuli tuamue na kusini tujenge ile ili iweze kuchechemua uchumi wa kanda ya kusini. Tuamue kabisa kimsingi, tufumbe macho, Mchuchuma na Liganga isiwe historia ianze kufanya kazi ili wananchi wapande hii ya kusini wafaidike na biashara hii ya makaa ya mawe na mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninalisisitiza kwenye habari ya Benki ya Ushirika yetu ambayo imeanzishwa. Ninaomba sana, tumeanzisha kwa hela ndogo sana, lakini tutakavyoanza kujenga matawi tuangalie maeneo ambayo uzalishaji na vikundi vya ushirika vipo vingi sana ili iweze kusaidia kukua kwa haraka benki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa mfano kwenye kanda hii ya korosho. Ni zaidi ya trilioni moja, benki zetu zinapitishwa kwa ajili ya wakulima na vyama vya ushirika kwa ajili ya malipo mbalimbali ya mazao. Sasa jambo hili kama litakuwa sambamba na kufungua matawi kwenye Mkoa wa Ruvuma ambapo sisi kuna vyama vitatu vipo strong, vinajitahidi, vinakwenda vizuri, TAMCU, SUNAMCU na MBIFACU ambavyo vinashughulika sana na wakulima kwenye kahawa, mahindi, ufuta, mbaazi pamoja na korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Mtwara napo uzalishaji wa korosho umekuwa ni mkubwa sana, wana haki ya kupeleka Tawi hili la Benki ya Ushirika ili likawasaidie wanaushirika wenzetu wa Tandahimba, Newala, Masasi, Mtwara pamoja na Nanyumbu sambamba na vyama vya Mkoa wa Iringa, Lindi na Mkoa wa Pwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hilo jambo la ushirika mimi kama mwanaushirika ambaye nimefanya kazi zaidi ya miaka 10 kwenye ushirika ni ndoto ya muda mrefu, ni zaidi ya miaka 10 benki hii imeasisiwa, lakini ninashukuru kwa kuanza rasmi kwa benki hii. Tunaomba dhamira ya kuwasaidia wakulima iende sambamba na kufungua matawi kwenye maeneo ambayo wanaushirika wapo wengi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni suala la wafugaji holela. Katika maeneo yanayoathirika sana na ufugaji holela ni pamoja na Jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru kwa ujumla pamoja na Kusini, Namtumbo na maeneo mengi ambayo zamani hatukuzoea kuona ng’ombe, kwa hiyo ng’ombe wamekuwa wengi sana. Kwetu Tunduru tulitenga vitalu, hebu tusaidieni kuwahudumia wafugaji hawa kwa kuwapelekea miundombinu kwa ajili ya maji pamoja na majosho kwa ajili ya kuhudumia mifugo yao. Tukiwa tayari kabisa kuwasaidia kwa mtindo huu wataacha ule ufugaji holela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumetenga vitalu zaidi ya 252. Tunapozungumza saizi, vile vitalu wameviacha, wanaenda kwenye mabonde ambako wakulima sasa wanalima, wanategemea kwa ajili ya mazao yao na sasa hivi wanavuna mipunga na mazao mengine, lakini hawa wenzetu sasa kwa kukosa miundombinu kwenye maeneo yale tuliyowatengea, basi wanakimbia wanaenda kwenye maeneo ambayo yana mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa suala la kuwasaidia hawa wafugaji kuhakikisha wanapata miundombinu na kuwafundisha ufugaji wa kisasa badala ya ufugaji wa kuhamahama. Serikali itoe kipaumbele ili kuhakikisha kwamba wafugaji hawa wanakaa sehemu kwa amani kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ni ujenzi wa maghala kwenye vijiji vyetu. Tunazungumza vizuri uzalishaji umeongezeka, lakini nimesoma taarifa hiyo mwaka mzima, miaka mitano hii tumejenga maghala 46 na vihenge 20 na nchi hii ni kubwa sana. Katika biashara ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kutumia TMX suala la ubora wa mazao unaendana sambamba na suala la sehemu ya kuhifadhia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumo wa Stakabadhi Ghalani unasema, mkulima atachukua mazao yake, atapeleka ghalani, atahifadhi kusubiri mteja wa kununua zao lake kwa namna ilivyo, Serikali iliamua kutumia vyama vya ushirika ili kurahisisha mfumo huu kwa sababu wakulima walio wengi uwezo wao ni mdogo. Wanavuna kilo 20, kilo 30, kilo moja, ni wachache ambao wanafika tani na zaidi ya tani, kilo 500. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuhifadhi yeye kama yeye kupeleka ghalani peke yake ni shida. Njia pekee ya kuhakikisha kwamba huu mfumo unaenda vizuri na ubora unakwenda sawasawa, tuwekeni mpango maalum kabisa wa kujenga maghala kwenye vijiji vyetu ili kuhifadhi mazao hayo kule kule wakulima ambako wanazalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria inataka mfumo wa stakabadhi, ghala likiwa na uwezo wa kuhifadhi tani 200 tu, sheria inaruhusu kuendesha mfumo wa stakabadhi ghalani. Hebu tuamue na hili tuhakikishe kwamba tunakuwa na maghala ya kisasa kwenye vijiji vyetu ili mfumo huu waone wananchi wa kawaida jinsi unavyowajali uchumi wa mazao yao kwenye maeneo ambayo wanaishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)