Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nimshukuru Mwenyezi Mungu na mimi kupata wasaa wa kuchangia, kama Mjumbe wa Kamati ndani ya Wizara hii. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninampongeza nikiwa na sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilivyoanza Bunge nilianzia Kamati ya Kilimo, tulikuta bajeti ni shilingi bilioni 294, wakati huo Mheshimiwa Bashe alikuwa ni Naibu Waziri. Sasa tunawauliza mtafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ukiniuliza sifa za Mheshimiwa Bashe, nitakuambia ni usikivu, uthubutu na ujasiri na ukiniuliza tena, nitakuambia ni uthubutu, usikivu na ujasiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alitupa moyo akasema haitachukua muda bajeti yetu itakuwa imeongezeka na ndio zilikuwa kelele zetu na leo tunaongelea bajeti ya shilingi trilioni 1.2. Haya ni maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini amempata kijana, Mheshimiwa Bashe ambaye ameweza kuyashikilia akiwa na msaidizi wake, Mheshimiwa Silinde na wana timu yao inayoongozwa na Ndugu Gerald Mweli, imejipanga na wamejipanga sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niwaambie, Mheshimiwa Bashe inawezekana unachofanya kwa vijana wa Tanzania hawajakielewa. Kamati ni mashahidi, tulivyoenda kwenye semina ya tamthilia ya mbegu, vijana walitoa ushuhuda, ukiwa kanisani unaweza ukasema ushuhuda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakasema vijana tuingie kwenye kilimo kwa sababu ni wakati ambao Mungu ametupatia Mheshimiwa Hussein Bashe kutusaidia sisi vijana kwenye kilimo; sasa tusisubiri ameshatoka ndipo tunamsifia, leo anatakiwa apate sifa zake. Maono ya Mheshimiwa Rais ameyatekeleza kwa kusaidiwa na wasaidizi wake. Ukimwangalia Mheshimiwa Silinde yeye yupo kimya kimya, lakini akikwambia anakwenda mahali atatekeleza na anatekeleza kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niongelee umwagiliaji na uchimbaji wa scheme. Ameongea Mheshimiwa Kimei, kama hatukupeleka hela kwa usahihi na inavyotakiwa kwenye umwagiliaji tutawaonea wataalam walio kwenye umwagiliaji. Scheme ile ukishaianzisha unatakiwa uimalize, ukiiacha katikati kama ikija mvua ile scheme itaondoa halafu utaona kama mtaalam amekula fedha, kumbe hajala fedha, ni sisi hatupeleki fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe Wizara ya Fedha wapeleke fedha kama zilivyopangwa kilimo. Passion ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kilimo. Ili kilimo kiende hizi scheme zijengwe zimalizike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichogundua kwenye umwagiliaji ni ushirikishwaji wa wananchi mahali ambapo hizo scheme zipo. Nitatoa mfano wa scheme ya Ilanyinda ambayo ipo Mkoa wa Shinyanga. Tulifika kwa Mkuu wa Mkoa taarifa aliyotupatia ndiyo ambayo Mkurugenzi anayotupatia na ndiyo ambayo Mheshimiwa Waziri aliyokuja nayo kwenye Kamati. Uhakika huu ninaupata wapi? Tulipofika kwenye scheme wanamfahamu Mkuu wa Mkoa utadhani ndiye Waziri wa Kilimo, ni kwa sababu kila wakati anakwenda kukagua mradi huo, lakini tuliyekuta anasimamia ule mradi ni Mwenyekiti wa Kitongoji, ndiye anawasimamia wale vibarua wa kila siku.
Kwa hiyo, wale watakuwa na uchungu wa kuutunza ule mradi kwa sababu wameshirikishwa. Hii tuombe na Wizara nyingine zenye miradi ziige mfano huu wa kushirikisha wananchi walio eneo hili ili kuweza kulinda kilichopo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee mikoa potential ambayo tunatakiwa tuiangalie kwa macho mawili kwenye kilimo. Kuna Mkoa wa Morogoro, kiti chako kilitupa ruhusa kama Kamati ya Kilimo tukaweka kambi kama siku tano Mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro kila zao linaota. Kuna Mkuu wa Mkoa tusipompa maua yake ni kumwonea, Mheshimiwa Adam Malima, amekuja na formula kwa vijana. Kama tukiifanya Tanzania na Mheshimiwa Bashe ukiichukua hii vijana wote hakuna atakayelia lia na ajira zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishuhudia kugawa miche ya karafuu kwa vijana walio darasa la kwanza kila kijana miche 10, na Mheshimiwa Naibu Waziri tulikuwa wote. Sasa mimi kwa hesabu yangu ndogo, sikusoma PCM, nikapiga hesabu kwa miche hiyo 10 kwa kijana ambaye amepewa yupo darasa la kwanza, mkarafuu unaanza kutoa maua na mazao ukiwa na miaka minne, mkarafuu mmoja unatoa kilo 15 na bei ya karafuu sasa hivi ni shilingi 30,000. Sasa kijana huyu wakati anafika darasa la sita atakuwa na uwezo wa kutengeneza shilingi 4,500,000. Anapofika form six atakuwa anatengeneza shilingi milioni 22 kwa mche mmoja. Sasa tuchukulie form six naye ameanza kupanda huku, alipokuwa form one akaanza kupanda mwenyewe, mpaka anafika chuo kikuu ana miche 100. Miche 100 kwa kilo 15 atakuwa anatengeneza milioni 45 ni kijana gani atataka umuajiri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo waliosema kwamba mali ipo shambani, ipo shambani kweli. Kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri alichukuwe hili, tuanze huu utaratibu kwa vijana walio shule za msingi kuwapa mazao ambayo yanaota sehemu ile, itakuwa ni BBT nyingine, huku anasoma huku anatengeneza hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nitumie muda huu kumwomba Mheshimiwa Waziri, mimi nimeanza, nimechukua vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam wapo 20, na amenisaidia Mheshimiwa Mbunge wa Mvomero, nimepitia kwa RAS, pale Mvomero kuna ekari tano za kupanda kakao. Sasa mimi nitamfuata kabla Bunge halijaahirishwa ili anisaidie vijana hao wapate fedha waende kulima kakao. Baada ya miaka minne wale vijana watakuwa wanavuna na bei ya kakao kilo moja ni shilingi 29,000. Hao vijana baada ya muda watakuwa ni wasemaji wakubwa wa kilimo, tutakuwa tumepunguza vibaka Dar es Salaam. Wapo tayari kuweka kambi Mvomero kwenda kulima. Mimi nimwombe alichukuwe hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kusema hayo ndiyo narudia kumpa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu awe na amani, hawa vijana wote ndio wanaokwenda kumpiga kura, akina mama wote ndio wanaokwenda kumpigia kura. Kwa suala alilokumbuka la wakulima wa Tanzania ambayo ni 70%, sisi tuliokuwa maskini wakulima wa Tanzania leo tunakuwa matajiri kwa ajili yake. Yeye Mheshimiwa Bashe anaendelea kutekeleza maono hayo. Tumeona kila mikoa tunayotembea, tumeona hizo scheme za umwagiliaji na tumeona sasa anakuja kuvumbua zile mbegu za asili ambazo amesema kwamba kabla Bunge halijavujwa zitakuwa zimesajiliwa TARI ili sasa mtu aamue, akienda sokoni akute mbegu ya asili, akute hizi za kisasa aamue analima nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale akina mama wa Karatu walimpa ushuhuda siku ile kwamba mbegu ya asili ya mahindi kwenye hekta moja unaweza ukavuna magunia 45; mbegu ya asili ambayo inavumilia ukame, haihitaji mbolea sana, ni mbolea ya asili ya samadi. Hebu turudi kwenye vitu vyetu vya asili, hebu twende tukatumie mbegu za asili. Aliziona zilikuwa pale, aliona mahindi yalivyokuwa pale, unga wake tumenunua, ni mtamu kuliko unga unaotoka kwenye mahindi ya kawaida haya ya sembe. Sasa twende tufanye hivyo, kilimo kibadilike lakini kwa kukumbuka na mbegu zetu za asili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niendelee kuwapongeza kwa vifaa walivyoleta…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha tafadhali.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Oooh, ninaunga mkono hoja. (Makofi)