Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii jioni ya leo kuweza kuchangia kwenye Wizara hii ya Fedha na Wizara ya Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia leo hii tukakutana wazima. Pili, nikupongeze wewe tokea asubuhi upo kwenye Kiti kwa ajili ya kusimamia utaratibu. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Mipango kwa uwasilishaji mzuri wiki iliyopita wa taarifa hii ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana pia Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Leo hii kabla sijazungumza yote ninaomba niunge mkono wa asilimia mia moja taarifa hii ili kuweza kumpa nguvu Mheshimiwa Waziri. Kutoka na mawazo ya Mheshimiwa Rais haya leo hapa tunayajadili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa mno kwa kipindi chake hiki ambacho tayari amepokea kijiti. Ipo baadhi ya miradi mbalimbali ambayo kwa akili ya kawaida Watanzania walikuwa wanafikiri kama Mheshimiwa Rais anaweza kuyatekeleza. Leo hii tunaona na tunashuhudia miradi mikubwa ya kielelezo ambayo ameiacha mtangulizi wake, Mheshimiwa Rais ameikamilisha. Kesho pia tutashuhudia huko Mwanza Mheshimiwa Rais nako anakwenda kukamilisha lile daraja kubwa ambalo Watanzania wa Mwanza, Geita na maeneo mengine jirani wanaenda kushuhudia na kuweka historia kubwa ya mama alivyokamilisha miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ninatokea upande wa pili wa Zanzibar Mheshimiwa Rais pia nimpongeze sana kwa kazi nzuri ambayo tayari amefanya. Hatujawahi kushuhudia kwa namna ambavyo Mheshimiwa Rais, Mama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuuenzi Muungano huu, lakini pia kushuhudia ile fedha ambayo inakwenda Zanzibar kama ya Muungano kwenye magawio anaisimamia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi na yeye pia kwa kusimamia vizuri zile fedha ambazo tayari zinaenda vizuri kwa ajili ya kuchochea maendeleo kwa upande wa Zanzibar. Tumeshuhudia miradi mbalimbali; hivi karibuni tu tuliingia kwenye janga kubwa la COVID tulipokea fedha nyingi sana, lakini kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo Mheshimiwa Rais kuna fedha baadhi ya nusu zaidi ya bilioni 230 nayo ilikwenda kule Zanzibar ikatekelezwa miradi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Zanzibar ninavyo vijiji zaidi ya vitatu, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Zanzibar pamoja na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna walivyoshirikiana kwa pamoja kwenye fedha zile za COVID kwenda kujenga madarasa ya shule na pia kujenga miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo miradi ya hospitali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo pia miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwa mfano kama ujenzi wa Airport ya kisasa ambayo inategemewa kujengwa kule Kisiwani Pemba, yote hayo ni mikakati pamoja na ushirikiano mazuri ya Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dkt. Hussein Mwinyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashuhudia vile vile kuna ujenzi mkubwa wa Barabara ya Tunguu mpaka Makunduchi, nayo pia inatengenezwa kwa kushirikiana kwa Marais wetu hawa wawili. Pia, tunashuhudia ujenzi wa Barabara ya Chakechake - Wete nayo pia ni ushirikiano ya Marais wetu wawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia pia Nchi yetu ya Tanzania kwa namna ambavyo Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan aliyobeba ajenda ya nishati safi ambayo tunasema mitungi ya gesi, kwa namna ambavyo siyo huku tu Tanzania Bara mpaka kule Zanzibar nishati hiyo inatumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimesema niunge mkono taarifa hii kwa sababu tunafahamu kwamba tunampa mandate mama ya kwenda kufanya kazi. Kwa hiyo, nikasema nimuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo miradi ya kimaendeleo kwa upande wa pili pia Zanzibar inaenda kufanya kazi Zanzibar yanaenda kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hilo sasa niende kwenye mchango wangu kuja kwenye sekta ya kilimo. Juzi hapa tumemsikia Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo kilimo chetu cha Tanzania kilivyopiga hatua, kutoka 2022 tulikuwa tunaambiwa tupo kwenye 2.5%, lakini kwa sasa hivi mpaka tunazungumza 2025 tupo kwenye hatua ya 4-point na kadhalika kwenye kilimo. Hii yote inaonesha kwamba namna gani tulivyopiga hatua. Tunaambiwa tuna wastani wa chakula wa takribani 128%, yote inaonesha kwamba tumevuka mpaka kwa namna ambavyo tulivyokuwa na reserve ya kutosha ya chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri Mheshimiwa Bashe, tumekuwa tukimpongeza hapa siku zote kwa namna ambavyo alivyokuwa na mipango ambayo inatekelezeka. Wizara hii huko nyuma hata bajeti yake ikipangwa ilikuwa inapangiwa bajeti ya fedha za kawaida, lakini tumeshuhudia mwaka huu Wizara yetu ya Kilimo imepangiwa fedha nyingi. Hii yote inaonesha imani kubwa ya Mheshimiwa Bashe, lakini imani kubwa na dira ya Mheshimiwa Rais ya kutaka kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hilo pia, kwenye kilimo tunaambiwa tunafanya vizuri zaidi, lakini bado hatujaangalia kutanua zaidi kwa ajili ya kusambaza vyakula vyetu nje ya nchi, yapo baadhi ya mazao machache ambayo tayari tunafanya exportation, lakini nishauri kupitia Wizara yetu ya Fedha pamoja na Mipango, sasa hivi lazima twende kwenye modality nyingine ya kilimo. Wapo wawekezaji mbalimbali duniani sasa hivi wanatumia mfumo wa EPC+Finance, hii ni miradi mizuri sana ambayo inatekelezwa na wenzetu, wanakuja ndani ya nchi, Serikali inawapa fedha wanatekeleza miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao kama wao wanasimamia in term of engineering, procurement pamoja na masuala ya construction. Tukiwapa fedha wao watakuwa wanatengeneza miradi lakini vijana wetu ndio watakaopata ajira, lakini pia ardhi yetu ndio watakayoitumia. Pia, tukiwapa fedha maana yake tutakuwa tuna guarantee ya fedha zetu kwa namna gani ambayo tunaweza tukarejesha kwa kipindi kifupi, hii itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ipo Miradi kama BBT, hili tumewaachia ndugu zetu vijana wetu wa Kitanzania ndio wanatekeleza, lakini miradi kama hii ambayo tayari inatekelezwa na wenzetu kutoka nje, lakini miradi ikishatekelezwa fedha inayopatikana itabakia ndani ya nchi lakini tutakuwa tuna uhakika wa masoko ya nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba sana Wizara ya Fedha, hebu tuliangalie hii. Tumekuwa wagumu sana, tumekuwa wavivu kwenye eneo hili la kuweza kufikiria. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba kakae na Mheshimiwa Bashe, ninadhani miradi kama hii inatekelezeka. Zipo baadhi ya Nchi kwa mfano wenzetu Zambia, wanatekeleza miradi kama hii, lakini hata ukienda hapo Uganda pia wanatekeleza miradi kama hii. Wageni wanasimamia miradi kama hii lakini fedha inayopatikana inabakia ndani ya nchi na tunakuwa tuna guarantee ya fedha zetu ambazo tayari tumeziwekeza kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje kwenye eneo la pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais amekuwa msikivu sana kwa wafanyabiasha hususan wadogowadogo (machinga) juzi tumesikia hapa Mheshimiwa Rais ameridhia na ametoa mandate kwamba kutenganisha biashara za wazawa pamoja na wageni, hili ni jambo la kupongezwa sana kwa Mheshimiwa Rais. Tumeshuhudia kila siku kariakoo kwenye majiji wananchi wanalalamika kuonekana kazi ambazo zinaweza zikafanyika na wazawa lakini wageni wanafanya hizi kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kusikia kilio hiki, lakini pia kuielekeza Wizara kuweza kutathmini sasa hivi biashara gani wanaweza wakafanya wazawa na biashara gani wanaweza wakafanya wageni. Hili ni jambo zuri sana na lazima Mheshimiwa Rais apigiwe makofi mengi kwa namna ambavyo alivyowafikiria vijana wetu wa Kitanzania. Hii imechochea uchumi wetu katika nchi, lakini pia imewasaidia vijana wetu ambao tayari wanafanya kazi, wanafanya biashara ndogondogo, hawa vijana wetu ambao tunawaita machinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, tumekuwa tukilalamika sana hususan sisi Wabunge ambao tayari tunatokea Zanzibar kuhusiana na hizi tozo za forodha hususan za bandarini. Kumekuwepo na kama njama fulani za watu wa tax hawa customer’s duties wa bandarini either airport. Kwa mfano, airport pale, utawakuta hawa watu wa tax wanasubiria ndege. Zinapokuja ndege za Uturuki, zinapokuja ndege za China au Dubai utawakuta wenzetu hawa watu wa taxi ndio wanaowaagizia wafanyabiasha, kwa hiyo hakuna transparency kabisa katika ku-charge kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale airport kuna kachumba maalum, ukifika unakadiriwa; hii nipe kiasi kadhaa, hii nipe kiasi kadhaa. Kwa hiyo, ninaiomba sana Wizara yako Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, hakuna transparency katika utozaji wa kodi hususan kwa bidhaa ambazo zinatoka nje ya nchi; na mfano huohuo ukienda pale bandarini hakuna modality ya bidhaa ambazo unatoka nazo Zanzibar unakuja nazo labda Tanzania Bara, hakuna price kabisa. Ukienda pale mfanyabiashara unakadiriwa kwa namna ambavyo wanavyojisikia wao wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, haya malalamiko na changamoto kama hizi zinaweza zikatatulika, tusimsubiri tu mpaka Mheshimiwa Rais ndipo akemee na asemee haya mambo. Haya mambo yapo, tunaomba Wizara husika isimamie transparency tunaitaka hususan kwenye maeneo hayo katika nchi yetu. Kwa upande wa Zanzibar kuja Tanzania Bara na kwa upande wa Airport.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nikushukuru sana kwa kunipatia fursa hii na ninaunga mkono hoja iliyokuwepo mezani. (Makofi)