Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa fursa hii. Nianze tu kwa kujiunga na wenzangu kumshukuru na kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mkakati anaousimamia kwenye sekta hii ya kilimo ambao sasa umeanza kuonesha matumaini na neema kwa wakulima na kuonesha kwamba kujenga uchumi shirikishi ambao unashirikisha watu wengi wakiwemo wakulima wetu inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba maono yake haya yalianza pale alipoweza kumuona Mheshimiwa Bashe, Mheshimiwa Silinde pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara akawapa jukumu la kuendeleza sekta hii ambayo wamekuja na ubunifu mkubwa. Kwenye sekta hii siyo rahisi kubuni sana kwa sababu miaka mingi tumesema kilimo ni siasa, lakini nani aliweza kufikisha hiyo siasa mahala pake, kama siyo Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, timu yake kwenye Wizara pamoja na taasisi wanazozisimamia ambazo kusema kweli tumeanza kusikia mambo ya kutoa mbegu, kwenda usambazaji wa mbolea na kadhalika na reform kwenye ushirika unaanza kuonekana. Kwa hiyo, ninasema kwamba sisi Watanzania ambao tunajumuika kwenye sekta hii, kwa pamoja lazima tumsifu na tumshukuru sana kwa kazi anazochapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii the whole thing ambacho mimi kinanisikitisha kidogo ni kwamba release ya funds, fedha zilizotolewa mpaka mwezi Aprili kama kweli nimesikia vizuri kwenye hii hotuba ni 53%. Haitoshelezi kwa kazi inayofanyika na ndio ninaamini kwamba bado kuna miradi imezubaa zubaa huko kwa sababu hela haijaenda mahali pake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sababu moja inaweza ikawa pengine tume-over stretch kwamba implementation capacity kwenye Wizara haiwezi kwenda na fedha nyingi kiasi hicho na hautatarajia kwa sababu shilingi trilioni 1.2 mahali ambapo kulikuwa na shilingi bilioni 294 inawezekana ikawa kwamba ni lazima wajipange vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nilikimbilia kusema kwamba kwenye Wizara hii tatizo kubwa ni mifumo na taasisi, institution building ndani ya Wizara na sekta kwa ujumla kwamba nitamfikishiaje mkulima mdogo pale kijijini mbolea, efficiently? Nitamfikishiaje pembejeo? Nitamfikishiaje, kama ni huduma, hata ya trekta ili aweze ku-expand? Mtamfikishiaje mbegu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kitu kilikuwa kipo, hii institution building. Huu mfumo ulikuwepo, lakini huu mfumo ulikufa baada ya cooperatives kufifia. Hii movement ya ushirika ilidhoofika na baada ya kudhoofika, basi ikawa imeua ile chain ambayo ilikuwepo. Tulikuwa tumeunda, miaka ya nyuma huko na tulivyokuwa wadogo tulikuwa tunaona jinsi ambavyo mabwana shamba, huduma ya ugani, ilikuwa inakwenda kupitia ushirika na inasimamiwa kupitia ushirika. Sasa hakuna hicho kitu, kimekufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninataka kusema kwamba kitu kinachoua ushirika siyo sheria, siyo kanuni, ni watu. Sasa kama watu wanakamatwa wamefanya uzembe huko halafu hawaadhibiwi inavyostahili, wanaendeleza kuua ushirika na mimi ninakuomba Mheshimiwa Bashe ninaamini kwamba Mheshimiwa Rais ataku-back up kwamba mtu akifanya kosa kwenye kuendesha ushirika, kama wale kule kwetu Vunjo, walishindwa kulipa fedha za wakulima wa kahawa wakakaa nazo, kwanza walizimeza halafu hawakuwalipa na wakawa hawako hata wawazi kwamba hiyo hela imeenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu kama wale wafungwe. Ni kuwafunga, hata hamna mambo ya faini kwa sababu mpaka leo hii Mheshimiwa Waziri ulisema.

Hee, ni dakika tano tano! Basi, kama ni tano tano, ninaona mambo mabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ninafikiri takwimu ambazo ametoa Mheshimiwa Bashe kuhusiana na uzalishaji ulivyoongezeka, ukiangalia na jinsi ambavyo kweli kwenye NBS Mtakwimu Mkuu wa Serikali anavyosema agriculture ina-grow kwa 4.1 percent, siamini kama ni kweli. Naamini lazima tuoanishe mahali fulani, kuna mahali ambapo watu wa takwimu hawajapata mambo haya yanayoendelea kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba pamoja na hivyo, ukiangalia jinsi fedha ilivyotiririka, mabwawa yanayojengwa ni mengi mno kwa wakati mmoja, huwezi kujenga yote kwa wakati mmoja, inakuwa kwamba lazima utakuwa unalaza damu mahali. Kwa hiyo, hela inalala pale, halafu humalizi, chukua machache maliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna bwawa moja ambalo nilizungumza juzi, Mheshimiwa Silinde akalijibu vizuri sana kwenye swali langu, Bwawa la Urenga. Bwawa la Urenga pale ni natural, hata halihitaji kuchimba, maji yanakuja yanasimama pale, yanachotwa, halafu linanywesha. Lile bwawa linasaidia watu zaidi ya 27,000 na eka zinazoweza kunyweshwa kwa kupitia bwawa hilo ni eka 15,000 is a low hanging fruit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwamba Mheshimiwa Silinde alivyotembelea kwa kutumwa na Mheshimiwa Waziri, aliona, akashangaa, akasema kuna potential. Sasa yeye hakuona ile potential kwa sababu hajajua watu wanaoitegemea; watu wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Kirua Vunjo Kusini, Kata ya Kahe Mashariki yaani ni watu wengi. Sasa hivi mazao yao yamedumaa kwa sababu lile bwawa halipo, liliharibika kidogo na linahitajika kurekebishwa na alituahidi kwamba limeingia kwenye bajeti. Ninakuomba sana Mheshimiwa Bashe, uliliacha hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakushukuru pia kwamba Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji naye ameanza kukarabati mifereji, mingine inatoka kwenye bwawa hilo hilo. Kwa hiyo, ameanza ukarabati, ni kitu ambacho kusema kweli kinaleta matumaini na neema kwa Wana-Vunjo. Ninaomba muendelee na kazi hiyo, ninaamini kwamba tutafika vizuri. Pia tujue kwamba kwa Wana-Vunjo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa. Muda wako umeisha, hitimisha hoja yako Mheshimiwa, tafadhali.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusema BBT tu kwamba mnyororo wa thamani wa mazao, kama ndizi na nini, aendelee kutusaidia pale. (Makofi)