Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. Kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa commitment hii kubwa anayozidi kuifanya, maana mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo. Tumeona ongezeko la fedha kutoka shilingi bilioni 297, leo ninaongelea shilingi trilioni 1.242; ni hela nyingi sana ambazo zimewekezwa. Kwa hiyo, tuzidi kupongeza na kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi kipekee zimuendee Waziri - Mheshimiwa Bashe, Mheshimiwa Silinde - Naibu Waziri, Katibu Mkuu – Ndugu Gerald na wasaidizi wengine. Ninasema mpewe pongezi kwa sababu unapoona Mheshimiwa Rais anaruhusu fedha hizi ziende kwa wingi huko maana yake ni ana confidence na ninyi. Wizara zipo nyingi na kila Wizara ni muhimu, lakini kwa haya ambayo mnayafanya, mipango mizuri na usimamizi mzuri, ndio maana mnaona pesa zinatiririka, na hasa Wanakamati pia tumekuwa tunapambana kujua kama kuna mkwamo wowote tupige kelele, lakini Mheshimiwa Bashe, mara nyingi umetuhakikishia upo mstari wa mbele hata ku-push kutoka Wizara ya Fedha na mambo yanaenda. Kwa hiyo, tuwapongeze sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nikirejea sasa katika hotuba ukurasa wa 128 wa hotuba yake Mheshimiwa Waziri, ametaja vipaumbele sita ambavyo atavitekeleza kwa kutumia mikakati 30. Sasa mimi nilikuwa ninatafuta yale yanayonihusu kwa sababu unajua mambo yapo mengi. Hii Wizara tunatamani hata sometimes iwe na siku tano au sita, maana ni Wizara ya wakulima, ni Wizara ya nchi nzima, lakini kwa sababu tunakimbia na hizi dakika saba, nane, sometimes huwezi kufika sehemu unapotaka kuongea na ndio maana watu wetu huko watashangaa mbona hukusema hili! Muda hautoshi tupo limited. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia ukurasa wa 132 kwenye kipaumbele chako namba tatu, umesema kuimarisha usalama wa chakula na lishe. Sasa mkakati ambao nilikuwa nimeuona ni uwekezaji kwenye miundombinu ya uhifadhi wa chakula mpaka kufikia tani 3,000,000 kwa mwaka 2030. Mheshimiwa Bashe na kipaumbele namba nne pia, kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji, mauzo ya nje ya nchi na mkakati ambao ninaurejea ni kujenga miundombinu ya masoko ya mazao ya kilimo, kwa ajili ya wakulima katika halmashauri mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maelekezo ambayo umeyapokea, kipekee nikushuru wewe mwenyewe binafsi Mheshimiwa, ulini-assure kwamba tulete maandiko, kwa ajili ya ujenzi wa soko la mazao ya kilimo katika Wilaya ya Biharamulo, eneo la Lusahunga. Pia ukanihakikishia ujenzi wa maghala ya chakula katika eneo la Lusahunga pale kwa sababu ni junction inayo-serve Kigoma, Rwanda na Burundi na inayo-serve watu wanaoenda Uganda. Kwa hiyo, nikushukuru sana na salamu hizi za shukrani ninaahidi, kwa niaba ya Wana-Biharamulo, mtazipokea mwezi Oktoba mwaka huu wa 2025. Sisi hatuna maneno mengi, tunaenda kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine pia Mheshimiwa Waziri for the first time, hata sisi leo watu wa Kagera na hasa sisi wa Biharamulo, nimeona kwenye bajeti yako, ukurasa wa 203 umeongelea ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji, huko una mabwawa 114. Tuna Bwawa letu la Mwiruzi pale limetajwa, linalojengwa kwa meter cubic 13,000,000 za ujazo au lita za ujazo 13,000,000,000. Ni bwawa kubwa sana na linaenda kuwangilia kwenye skimu ya umwagiliaji, ile skimu 42 umetuweka tena Wilaya ya Biharamulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna skimu ya umwagiliaji ya hekta 13,000 eneo la Mwiruzi, kwa hiyo, tuzidi kushukuru na ndio maana tunasema mambo ni mengi, lakini tungeweza kuyasambaza yote hapa yasingetosha, yote hii ni shukrani kwa sababu hata sisi for the first time tunaenda kupata mradi wa umwagiliaji, skimu kubwa katika Wilaya ya Biharamulo na licha ya skimu tunapata bwawa kubwa lenye ujazo wa lita 13,000,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala nilitaka niliongelee pia hapa suala la kahawa, sisi tunaotoka Mkoa wa Kagera tunaelewa. Mheshimiwa Rais alivyoingia mwaka 2021 kahawa kwa Mkoa wa Kagera ilikuwa na tozo 49, kupitia juhudi za Mheshimiwa Waziri na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tozo zimefutwa kutoka 49 zikabaki saba. Ndio maana kwa Mkoa wa Kagera by 2021, mimi ninaongelea kwangu Biharamulo bei ya kahawa ilikuwa inauzwa kati ya shilingi 1,200 mpaka shilingi 1,400. Kwa mwaka jana ambao tumemaliza tumeuza kahawa kilo moja kwa shilingi 5,400 robusta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siyo kitu kidogo, unaweza ukaona kazi kubwa iliyofanyika. Tuzidi kupongeza bidiii kubwa sana iliyofanywa na Serikali, kwa ajili ya kuwainua wakulima wa kahawa kwa Mkoa wa Kagera na hususani Biharamulo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumekuwa tunapokea miche ya ruzuku ila Mheshimiwa Waziri, Biharamulo tumeenda mbali zaidi, maana Wilaya ile ni kubwa. Kwa hiyo, tumetengeneza vitalu vinne sasa hivi katika kanda tofauti tofauti ili wananchi waweze kupata hii ruzuku ya miche ya kawaha kulekule waliko. Ninapoongea sasa tuna vitalu vya miche 1,150,000 ambayo tutaigawa katika mwaka huu 2025, lakini ikiwa katika maeneo manne tofauti ili huduma tuweze kuisogeza karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee Mheshimiwa Waziri nikushukuru kwa habari ya wakulima wa tumbaku. Ninakumbuka kipindi kile ulinihakikishia kwamba unapambana, kwa ajili ya ruzuku ya watu wa tumbaku. Haikuwa rahisi, maana uliwekewa vikwazo kwamba ni zao la biashara, tukapata vikwazo vikubwa sana, lakini kwa bidii yako umepambana mpaka sasa hata sisi wakulima wa tumbaku tumeanza kupata ruzuku ya tumbaku. Yote hii ni kwamba mnapigana msiwasahau wakulima wa zao lolote lile kwa sababu bado wanaingiza fedha za kigeni, wanazidi kutuletea heshima katika nchi. Kwa hiyo, nikushukuru sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nikushukuru kwa ahadi ya ujenzi wa ghala la kuuzia tumbaku katika Kata ya Kalenge, maana tumehangaika sana kwa muda mrefu. Tulikuwa tunaenda kuuzia tumbaku Kahama, unatoa tumbaku Biharamulo, lakini wewe mwenyewe umetoa maelekezo kwa watu wa Bodi ya Tumbaku na wameshaniona, tunatafuta eneo ili waje wajenge ghala lile kwa ajili ya kuuzia tumbaku katika Wilaya ya Biharamulo na hususani Mkoa wa Kagera, tumbaku yetu isitoke nje. Yote haya ninashukuru na ninazidi ku-appreciate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu nikutie moyo kwa kitu kimoja; kilimo siyo betting, unajua ukienda kwenye betting ukiwa na shilingi 1,000 unaweza ukaingia na ukatoka na shilingi 1,000,000. Ndugu zangu kilimo ni mchakato, ndio maana tumekuwa tunaambiwa kuna upembuzi yakinifu, kuna usanifu hapo, uanze kulima, ukimaliza uvune, upeleke sokoni. Kuna maneno mengi sana yanasemwa hususani kwenye miradi hii ya BBT. Mimi nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri, wewe fanya kazi, wananchi wanaona matokeo, kamati imeona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anayeenda kulima kwenye mashamba, wengi tunaona mazao yakiwa yametoka, lakini tungekuwa tunaona misitu kabla ya kukatwa ndio tungejua kilimo ni process. Kwa hiyo, tukutie moyo, ufanye kazi tupo nyuma yako, tunachohitaji ni matokeo haya tutayaona baada ya muda. Huwezi kwenda kulima ukaona matokeo leo, matokeo tutayaona baada ya muda kwa sababu kilimo ni process. Tulianza na shilingi bilioni 297 leo tupo shilingi trilioni 1.2.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha. Tafadhali hitimisha.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia, dakika moja; leo tupo shilingi trilioni 1.2 kwa hiyo, haya ndio tunayoyasema, ulianza taratibu, sasa unazidi kupanda, unavyozidi kupanda ndipo tutakapokuja kuona matokeo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)