Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa rehema, ametulinda, lakini pia amenilinda mimi kama mwakilishi wa Wanakilolo kwa kipindi cha miaka mitano hii ya Bunge la Kumi na Mbili. Shukurani hizi ni kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ninajua mchango huu ninautoa kwa sababu ndio uchangiaji wa mwisho kwa Bunge la Kumi na Mbili. Kwa hiyo, sitapata tena fursa ya kuchangia mpaka Bunge lijalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kushukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa sana ambayo ameyafanya katika nchi yetu. Si katika nchi yetu kwamba Kilolo haijaguswa pia kwa sababu amewagusa Wanairinga, lakini pia Wanakilolo kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo miradi mikubwa ambayo imetugusa sisi Watanzania wote, kama miradi ya umeme vijijini ambapo vijiji vyote vya nchi hii vikiwemo vijiji vyote vya Wilaya ya Kilolo na Jimbo la Kilolo vimepata umeme. Ipo miradi mikubwa kama ya SGR ambayo kwa sasa inawagusa Watanzania wengi sana ambao wanatumia usafiri huo, lakini pia wananufaika kutokana na uchumi uliokua kutokana na miradi mikubwa ambayo nchi hii imefanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si miradi hiyo tu iko miradi mingi pia ambayo imegusa kila maeneo. Kwa mfano barabara za lami zinazojengwa kwenye maeneo mbalimbali; hata Wilaya ya Kilolo ambayo ilikuwa haijaunganishwa na barabara za lami sasa imeunganishwa na barabara za lami tunavyozungumza. Hii ni kazi kubwa sana iliyofanyika katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu mbalimbali pia ambazo hazikuwa na sekondari, sekondari zimejengwa na kuna miradi mingi ya maji inayoendelea. Wakati wote tunapozunguka tunaona jinsi ambavyo Watanzania kwa ujumla wana moyo wa shukurani kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua mchango mkubwa sana wa Waziri wa Fedha pamoja na Wizara yake katika kuhakikisha kuwa haya yote yanafanikiwa. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuhakikisha kwamba mpangilio wa fedha unawagusa Watanzania, hasa kwa miradi ile ambayo nimeitaja na mingine mingi ambayo inaendelea kufanyika katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi ambayo yamefanyika kwa Wilaya ya Kilolo nikisema nitaje orodha kwa kweli ni nyingi sana na kwa hiyo, itoshoshe kusema kuwa kipindi hiki cha miaka mitano kimekuwa kipindi cha mabadiliko na Watanzania wameona, wananchi wameona na wanajua nini cha kufanya katika kuendelea kuipa nafasi Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuwatumikia Watanzania. Ninafahamu kuwa kauli mbiu zitapita, lakini Kauli Mbiu ya Oktoba Tunatiki itakuwa na nguvu zaidi kuliko kauli mbiu nyingine zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia na kusoma bajeti hii vizuri na ninavyo vitu kadhaa vya kupongeza, lakini pia vya kuwekea msisitizo kwenye bajeti hii. Katika kipindi hiki pia nimepata fursa ya kuwa Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI wakati Kamati hii ilipokuwa iko pekee yake na hili suala la Aids Trust Fund lilianza kujadiliwa wakati huo. Nichukue fursa hii kumpongeza yeye, pia kuishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa sisi kama Watanzania kujitegemea katika kuwa na mifuko ya fedha zetu wenyewe zinazoweza kutufanya tuwe na mfuko wa fedha ambazo Watanzania wanaopata shida ya maradhi wanakuwa na chanzo ya kwetu sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la kuanzisha vyanzo vya mapato kwa ajili ya Aids Trust Fund pia kwa ajili ya bima ya afya kwa wote ni wazo la msingi sana na kwa kweli linapaswa liungwe mkono na Watanzania, lakini na Wabunge wote, ili sisi Bunge hili la Kumi na Mbili tuweke historia ya kuwa chanzo cha kuendeleza utaratibu wetu wa kutafuta namna bora ya kujitegemea badala ya kuendelea kuegemea kwa wafadhili ambayo inaweza kutufanya watumwa hasa nyakati ambazo tunahitaji kufanya maamuzi yetu sisi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni la kupongeza sana na kwa kweli mimi moja kati ya vipengele vya bajeti ambavyo nimeviona ambayo vinaonesha umakini wa Serikali hii ya Awamu ya Sita ni pale ambapo kuna maeneo mengi yanayoonesha kwamba nchi yetu ina dhamira ya dhati ya kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hilo tu, hata kujitegemea kwa bajeti katika uchaguzi ni kielelezo cha uhuru wa Watanzania, ni kielelezo cha kwamba Watanzania wameamua kufanya demokrasia ya kwao wenyewe ambayo itaonesha uhuru wa kugombea, uhuru wa kuchaguana bila kuwa na msukumo kutoka mahali pengine popote. Jambo hili ni jambo la msingi sana na nina hakika ni jambo ambalo ni la kupigiwa mfano kwa maamuzi bora kama haya. Tumshukuru sana Mheshimiwa Rais na pia tumpongeze sana Waziri wa Fedha pamoja na timu yake kwa ajili ya maamuzi makubwa kama haya ambayo yana mustakabali mzuri kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo machache ambayo pengine ni vizuri kuangalia ni kuona jinsi gani tunaweza kuifanya nchi yetu ikue kiuchumi. Hili linagusa zaidi sekta ya mipango. Sekta ya mipango imefanikiwa sana kwenye baadhi ya vipaumbele, ninataka nitoe mfano jinsi ambavyo sekta ya mipango imefanikiwa kwenye suala zima la kupeleka umeme vijijini na tukafanikiwa kwa 100% kwenye vijiji vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uchumi wa nchi hii uweze kukuwa ipo sekta moja ya muhimu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Mipango aweze kuliangalia suala hili kwa kuangalia jinsi gani tunaweza ku-copy mpango wa REA kwenda TARURA kwa ajili ya barabara vijijini. Kama tutakuwa na mpango unaofanana na REA ambao umefanikiwa kupeleka vijiji vyote, wakati huu tunapoweka mpango wa miaka mitano ijayo kuhakikisha kwamba kwa mpango huo huo tunao mpango ambao unahakikisha hakuna barabara katika nchi hii kwenye kijiji chochote ambayo haipitiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini, inawezekana? Inawezekana kwa sababu gharama za kupeleka barabara vijijini maeneo mengi inaweza kuwa ndogo kuliko gharama tulizotumia kupeleka umeme. Kama tumefanikiwa kupeleka umeme kwenye vijiji vyote mimi sioni kikwazo cha kuweka mpango madhubuti wa kuhakikisha kwamba barabara kwenye vijiji vyote zinakuwa ni za angalau changarawe na nyingine za lami. Tunaweza tukaamua kwamba kusiwe na sehemu ambayo hata kama ni kipindi cha mvua kiasi gani barabara haitapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wafanye kazi, tathmini ifanyike na baada ya hapo mpango wa miaka mitano ijayo uakisi suala hili na ambalo litakuwa ukombozi hasa kwenye maeneo ambayo hayapitiki kwa muda mrefu. Nikitolea mfano, hata Wilaya ya Kilolo ambayo changamoto kubwa sasa iliyobaki katika uzalishaji mali ni suala zima la barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa mfano huo tu, lakini kwenye nchi yetu yako maeneo mengi sana ambayo unaona jinsi ukuaji wa uchumi unafanyika. Kwenye kilimo uwekezaji umeshafanyika fedha nyingi zimewekezwa kwenye umeme, umeme upo, kwenye sekta ya maji tumefanya vizuri tumepeleka maji kwa kiasi cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uchumi unakua lakini sekta ya usafirishaji inakwamishwa hasa kwenye eneo la barabara ambalo mimi nina hakika watakapokaa na kuchakata na kuliwekea hesabu vizuri jinsi gani ya kukwamua eneo hilo watakuwa wamefanya jambo ambalo nina hakika kwamba litaleta tija kwenye nchi yetu. Niwaombe sana, kama litazingatiwa maana yake ni kwamba haliwezi kwenda kama kawaida. Umeme ulienda REA haikuwa kama kawaida, ilikuwa ni project maalum na ndio maana ilifanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utengenezaji wa barabara vijijini isiwe kama kawaida, iwe na mpango maalum na project maalum ambayo inahakikisha kwamba kuna ukombozi wa barabara kufikika maeneo yote ya nchi yetu ili Watanzania sasa waweze kuunganishwa na kufurahia usafirishaji wa mazao wanayoyazalisha kutokana na ruzuku za mbolea zilizowekwa, lakini pia na uzalishaji wanaofanya kutokana na umeme uliofika kwenye maeneo yao na maji ambayo tunaenda kwenye kuweka hizi za kwenye umwagiliaji. Ni lazima tufikiri namna bora ya kuimarisha miundombinu ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni namna gani tunavyoweza kukabiliana na changamoto ya mazingira pamoja na kuanza kufikiria kuweka kipaumbele kwenye motisha za watu wanaolima mazao ya misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya karibuni uvunaji wa miti ni mkubwa kuliko upandaji wa misitu. Maana yake ni kwamba, katika kipindi cha miaka michache ijayo nchi yetu itaingia kwenye changamoto ya kukosa mazao ya misitu, hasa mbao. Kwa sababu kwenye maeneo ambayo mazao hayo yanalimwa sasa watu wanahama kutoka kwenye kulima miti na kulima mazao mengine. Kwa mfano, Wilaya nyingine wanaanza kulima maparachichi na kadhalika. Nchi yetu hii ina uhitaji mkubwa sana wa mbao. Kwa hiyo, itafika wakati aidha bei ya mbao itapanda sana au utofauti na hiyo ambayo inaathiri uchumi kwenye sekta ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili hilo lisitokee maana yake kwenye mipango inayokuja ya miaka mitano ijayo ni lazima kuona Serikali inaweka motisha gani kwa wakulima wa mazao ya miti. Isipowekwa motisha yoyote maana yake ni kwamba wakulima wa mazao haya ambayo ni ya kusubiri muda mrefu bila kuvuna watapungua. Wakishapungua maana yake ni kwamba kutakuwa na kwanza athari za kimazingira ambazo zitaathiri kilimo cha kawaida kwenye maeneo lakini pili, tutakuwa na athari za kiuchumi hasa kwenye sekta ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni jinsi ambavyo Serikali yetu imefanya vyema katika bei za mazao mbalimbali. Mazao mengi ya kilimo huko siku za nyuma yalikuwa na shida sana kwenye bei, lakini tunakoenda unaona jinsi bei za mazao zinazidi kuongezeka, hasa mazao ya kilimo. Hata hivyo, katika uongezekaji huu wa bei za mazao iko changamoto ya vipimo. Ningependa kulizungumzia hili kwa sababu sasa hivi vipimo viko vya aina nyingi. Nikizungumzia kilimo kama cha vitunguu ambacho najua Mheshimiwa Waziri wa Fedha anafahamu, hata kule kwao wanalima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni walikuwa wanasema lumbesa, wakaikataza, sasa siku hizi wameleta neti. Neti maana yake ni kwamba haijai lakini inapanuka, yaani ule unene wa mfuko unakuwa mkubwa lakini juu ule ujazo unabaki vilevile. Hii imekuwa ni changamoto kiasi kwamba unajiuliza, je, Wakala wa Vipimo wenyewe hawajaliona hili na kama wameona ni nini wanachoweza kufanya? Kwa sababu hili linawakandamiza sana wananchi, wale wananchi ambao ni wa kawaida ilihali Serikali, wakati Mheshimiwa Rais anaendelea kutoa ruzuku ili Watanzania wapate bei nzuri (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati jambo linawafanya Watanzania wanafurahia sana kunakuja na changamoto ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu ambao wanataka kuwadidimiza wakulima. Jambo hili ni vizuri kwenye hatua zinazofuata kwenye siku zijazo kuliangalia ili liweze kuondoka. Likiondoka maana yake ni kwamba lazima tuweke utaratibu wa vipimo unaompa tija mkulima. Maana yake mkulima ambapo hajapata kipimo ambacho ni sahihi inamletea changamoto kwenye bei kwa sababu anauza kingi kwa bei ndogo na kwa hiyo ile tija inakuwa kidogo. Hilo ningependa kusema kwamba ni jambo ambalo tunatakiwa kuliangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali kwa ujumla kwa jinsi wanavyofanya juhudi ya kuendelea kuwalipa wakandarasi wa ndani. Juhudi zinaonekana; na kwa kweli ni jambo zuri sana kwamba wakandarasi wa ndani waendelee kulipwa ili kuchechemua uchumi; hasa wanaofanya sekta za maji, sekta za barabara na sekta nyingine. Ombi langu ni kwamba katika kipindi hiki wakandarasi wale ambao bado hawajalipwa waendelee kulipwa ili kuendelea kuhakikisha kwamba uchumi wetu unaendelea kuwa imara na kwamba Watanzania waliowekeza katika miradi mbalimbali ya Serikali wanaendelea kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba upo wakati ambapo tumeona jinsi ambavyo Serikali inatoa fedha nyingi kuwalipa wakandarasi hawa na kwa kweli pia hata namna ambavyo motisha kwa wakandarasi wa Tanzania inaonekana hata kiwango cha miradi wanayoweza kufanya tumeona kimeongezeka; kwamba ni fedha nyingi zaidi wanaweza kufanya miradi mikubwa zaidi. Watakapomaliza kufanya kazi pia vilevile ambavyo tunawapa kipaumbele basi pia tuwape kipaumbele katika ulipaji ili mzunguko wa fedha katika uchumi wa nchi yetu uendelee kuwa bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumalizia niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Nirudie tena kwa sababu Wanakilolo wanajua kazi kubwa aliyoifanya. Sisi Wanakilolo kwa ujumla wetu tumejipanga na tuko tayari kwa ajili ya Oktoba kuonesha shukurani zetu kwa Mheshimiwa Rais na kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imefanya mambo makubwa sana katika kipindi hiki cha mwaka huu, lakini pia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kwa kuwa kazi hiyo imeonekana na wananchi wote wa Kilolo mimi kwa niaba yao ambaye walichagua ili niweze kuwawakilisha ninafikisha shukurani hizi lakini huku nikisema tunajua kuwa bado ana miaka mingine mitano ya kututumikia na tuna uhakika atawatendea haki Watanzania kama ambavyo amewatendea kwenye kipindi hiki cha miaka mitano iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwaombea, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Waziri wa Mipango pamoja na Manaibu wao na wao pia warejee Bungeni ili waendelee kulitumikia Bunge letu. Mwenyezi Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)