Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuunga mkono hoja, lakini pili nitumie fursa hii kumshukuru sana na kumpongeza Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo ameifanya sekta ya kilimo kuwa na mageuzi makubwa sana na hasa ukianza kuangalia mafanikio yale yaliyoorodheshwa katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Mimi pia ninaona hayo ni mafanikio makubwa katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na daktari bingwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Waziri Bashe pamoja na Naibu Waziri na kwa kweli kwenye hii Wizara kama hii dhima ilikuwepo miaka mingi, lakini hii dhima iliyokuwepo kwenye Wizara yenu ya kujenga sekta ya kilimo endelevu na yenye ushindani ili kukuza uchumi shirikishi, kuboresha maisha ya mkulima kwa mara hii mmeipatia kuliko mara nyingine yoyote. Hongera sana Mheshimiwa Bashe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hayo mafanikio kuna eneo kubwa ambalo tunaona kabisa kwamba upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu ni jambo ambalo limeongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa sana. Nikiangalia baadhi ya mafanikio, kwanza unakuta bei ya mazao hasa sisi watu wa Mkoa wa Mtwara kama mashuhuda, ni mashuhuda wazuri kwa sababu kwa msimu uliopita korosho iliuzwa kwa wastani kwa bei ya shilingi 3,500 mpaka 4,195 kwa lile soko la TMX. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mliona picha kwenye mitandao ya kijamii watu walikuwa wanatutania kule. Sitaki kwenda kwenye huo utani, lakini mbaazi pia iliuzwa kwa shilingi 1,800 mpaka 2,200. Ninataka nimwambie Mheshimiwa Bashe, kazi aliyoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wakulima wa Mkoa wa Mtwara haijapata kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwetu mbaazi ilikuwa ni mboga Mheshimiwa Bashe. Ulikuwa unavuna tenga mbili unaiweka tena ukianza kula na familia yako mpaka wakati mwingine ina-pukuswa, nikwambie kwa kikwetu. Ukitaka kubadilisha mboga unaitoa kwenye zile punje unasaga inaitwa barahoa, lakini kwa mara ya kwanza mbaazi imekuwa ni zao la biashara, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufuta umeuzwa kwa wastani wa shilingi 4,000 haijapata kutokea. Sisi tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na pia tunakushukuru wewe Mheshimiwa Bashe, wewe huna baya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi hiyo nzuri na kwa kweli leo baada ya mafanikio makubwa uliyoorodhesha kwenye kitabu chako, ninaomba nishauri maeneo mawili kwa ufupi sana. Eneo la kwanza, hii kazi nzuri inayofanywa na Wizara, maafisa huduma za ugani kubaki kwenye halmashauri sio sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakurugenzi wa Halmashauri wana vipaumbele vingi, wana mambo mengi, kwa hiyo, hata bajeti inapowekwa kwenye Idara za Kilimo kwa Maafisa Ugani haitoki, lakini hata inapotoka inawekwa kutekeleza majukumu mengine, si rahisi sana. Kwa hiyo, huduma za ugani, na mmewapatia maafisa ugani pikipiki kwa mfano, tunatarajia sasa hao wakaweke mafuta kwa mishahara yao halafu wakulima watembelewe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninadhani kutokana na vipaumbele vingi walivyonavyo wakurugenzi si rahisi huduma za ugani wakatekeleza miradi yote ama kazi zile kwa 100%, kama watakuwa wanasimamiwa na Wakurugenzi wa Halmashauri. Ni muhimu kurejesha huduma za ugani Wizarani, inawezekana, lakini tukiacha hivi watakuwa bado wananing’inia tu kwa sababu, hata wakipangiwa, kwa mfano fedha kidogo; unataka kuniambia atapewa Afisa Ugani akashughulikie? Aka-check shamba darasa? Badala ya hiyo fedha ikalipe deni ambalo kwa siku hiyo, ama kwa wiki hiyo, mkurugenzi anatakiwa alilipe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ninadhani umefika wakati kwa kweli, huduma za ugani zirudishwe Wizarani ili kuona tija. Pia kuwa na mtiririko sahihi kutoka Wizarani mpaka kule chini kwa wanaowasimamia wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo mwaka jana hapa katika hili Bunge tulikurudishia, tulikupa tena kisheria, fedha za export levy na ni za kisheria kabisa. Sasa mimi nilikuwa ninatamani kujua tangu tulipokurudishia hapa Bungeni fedha za export levy, umepata kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hizi fedha kwa mujibu wa sheria zinatakiwa zirudishwe bodi. Zikifika Bodi ya Korosho zikatekeleze majukumu ama wajibu uliopangwa kisheria, pamoja na kuendeleza zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hizi fedha kama zinaenda zinatoka huko, asubuhi hapa Mheshimiwa Katani alichangia, zikaenda huko zinakokwenda, halafu tena Waziri sijui kwa taratibu zako, sijui kwa namna utakazozipata, lakini mimi nina uhakika kwa sababu ukiacha kuwatetea wakulima, lakini pia mimi ni mkulima, hatujaiona tija ya hizo fedha tulizokurudishia. Pengine wanaohusika watuambie, ni kwa kiasi gani fedha za export levy zimekuja kwako, kama Waziri wa Kilimo ama Bodi ya Korosho, kwenda kuendeleza zao la korosho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nirudie tena kuwashukuru sana, nikushukuru sana Waziri, Mheshimiwa Bashe, kwa kazi nzuri. Mungu abariki kazi ya mikono yenu, nina imani kura zote za Mkoa wa Mtwara, kwa mafanikio mazuri tuliyoyapata katika kilimo, tunampelekea Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)