Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa muda na mimi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii ya mwisho ya mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya na uzima na hatimaye leo tupo hapa tena tunawazungumzia wakulima wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi nianze na suala zima la uwepo wa Watanzania ambao walikuwa wapo tayari kulitumikia Taifa hili ili tuweze kusonga mbele. Nimeingia Bunge hili mwaka 2015. Wakati ninaingia humu ndani kwenye sekta ya kilimo tulikuwa tunaimba na ikifika Wizara ya Kilimo ilikuwa ni tafrani humu ndani hususan kwenye suala zima la pembejeo za kilimo likiongozwa na suala la mbolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Tanzania tunaenda kuandika historia kwamba migogoro na mahitaji ya mbolea inaenda kuwa historia ndani ya Taifa letu. Mwaka huu hatujasikia kelele tena za mbolea, wakulima wetu wamepata mbolea kwa wakati na wameweza kuzitumia na wamepata tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri? Mheshimiwa Waziri, wakulima wetu sasa wamefanikiwa kupata hiyo mbolea, lakini bado tuna changamoto chache. Changamoto ya kwanza ni ufikishaji ama ufikishaji kwa mbolea kwa mkulima yule wa kule chini. Kwa hiyo, ninachokiomba Mheshimiwa Waziri, tutengeneze mfumo wa kuhakikisha wale mawakala wetu wanaosambaza mbolea tuone ni namna gani tunawasukuma watupelekee mbolea kule kwa wakulima wetu chini ili wakulima wetu wapunguze gharama kubwa wanazozitumia kwa ajili ya kuitafuta ama kuifuata hiyo mbolea pale makao makuu ya wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili ambalo ninatamani kulisema kwenye hiyo hiyo mbolea kwamba tuna watu ambao leo wameanzisha viwanda vya mbolea hapa nchini na kuna wengine ambao wanaingiza. Nia na dhamira ya Serikali yetu na Taifa letu ni kuhakikisha tunawalinda Watanzania ambao wamewekeza ndani ya nchi yetu na hata hao wageni ambao wamekuja wakawekeza ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda vipo hapa Mheshimiwa Waziri, vimewekeza na vimesaidia kusukuma uwepo ama ongezeko la mbolea nchini lakini bado wana malalamiko yao; malipo yao hawajalipwa mpaka leo.
Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, utakapokuja watu hawa wanatamani kusikia kauli ya Serikali. Wamewapa wakulima wetu mbolea, je, ili tusiwakatishe tamaa na wakulima wetu msimu unaokuja wakakosa mbolea kwa ajili ya kilimo, wanatamani kusikia ni lini mafao yao, ni lini madeni yao yanakwenda kulipwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiachana na suala zima la mbolea, ninaomba sasa niende kwenye mambo mengine; uwepo wa mbegu ndani ya Taifa letu. Mheshimiwa Waziri, umeelezea vizuri sana kwa mapana yake na jitihada kubwa ambazo mnaendelea nazo kwenye Wizara. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, bado tuna changamoto kubwa sana ya mbegu, hususan mbegu ya mahindi na sio mbegu ilimradi mbegu, ni mbegu iliyo bora yenye tija kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado tuna changamoto ya mbegu ya mahindi, lakini pia na mbegu ya alizeti; bado tuna shida. Kwenye mbegu za miche na nini angalau mmesimama mko vizuri, lakini kwa wakulima wa mahindi na alizeti bado wana changamoto kubwa sana ya mbegu za mahindi. Mheshimiwa Waziri, mbegu nyingi za mahindi na alizeti bado si salama, si mbegu bora kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wengi wao wanaochukua mbegu hizi wanaenda wanapanda, lakini tija yake ni ndogo sana. Kwa hiyo, badala ya kupiga hatua tunaendelea kumrudisha huyu mkulima nyuma. Kwa hiyo, niombe jitihada kubwa muendelee kuziwekeza ili tuhakikishe sasa kwenye hawa watu ama mashamba yetu yale ya mbegu ambayo mmeshayaanzisha, twendeni tukasimamie sisi wenyewe tuzalishe mbegu zenye tija ili wakulima wetu wanapokwenda kuzitumia mbegu hizo ziweze kuwapatia tija kwenye kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia imesema vizuri kwenye suala zima la ongezeko la mbegu za mafuta nchini. Mheshimiwa Waziri, umetuambia sasa hivi kwenye suala zima la mbegu za alizeti ama ongezeko la nafaka za mbegu za mafuta ni za kutosha ni zaidi ya 100%. Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri, mkishirikiana na Wizara ya Fedha ile tozo ambayo mliiondoa, niombe irudi ili mbegu hizi ziweze kutumika kuzalisha mafuta ya kutosha na mazao yao wanayoyalima wakulima wetu yapate soko na hatimaye tuweze kujitegemea kwenye zao la mafuta ili tuepuke gharama kubwa tunazozitumia za kuagiza mafuta kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, viwanda vipo vya kutosha, wakulima wamezalisha alizeti ya kutosha. Kwa hiyo, tunakuomba na wakulima wa alizeti wanasema wameona mazao mengine mmekuwa mkitoa bei elekezi, ni kwa nini zao za alizeti kila mwaka linakuwa halina bei elekezi? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, ninaomba hitimisha tafadhali.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuombe sana Mheshimiwa Waziri na sisi zao la alizeti na hususan kwenye Mikoa ya Dodoma, Simiyu na Singida zao hili ambalo ndio tunaamini litatuondolea changamoto ya mafuta liweze kupewa kipaumbele ili wakulima wetu waweze kupata tija, lakini pia tuondokane na adha kubwa ya upatikanaji wa mafuta kutoka nje na kupunguza hizo gharama na hizo fedha ziweze kufanya kazi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, ahsante. (Makofi)