Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii kuchangia katika bajeti yetu hii ya mwisho, Bajeti Kuu ya Serikali. Kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wenzangu hapa, ninaunga mkono hoja zote mbili kwa kishindo kabisa na nitaeleza msingi wa kuunga mkono hoja hizo kwa nguvu kabisa kwa sababu ya mambo makubwa ambayo tumeyapata katika jimbo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uhakika kabisa tunacheza na tutashinda na kwa ridhaa ya wananchi na ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi nina imani tutarudi tena hapa kuendeleza miradi mizuri, ambayo tulikuwa tumeianza. Kwa hiyo, wale ambao wanafikiri hatuchezi na hatutakuwa na nguvu ya kushinda, tutacheza na tutashinda kwa kishindo kikubwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu, miradi mingi ambayo tumeipata katika Jimbo la Kilombero, Mkoa wa Morogoro na nchi yetu inatokana na mipango ya Serikali na ukusanyaji wa fedha unaoufanya wewe na watumishi wako wa chini pamoja na Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa sababu, hii ni hotuba yetu ya mwisho katika Bunge hili kabla hatujarudi hapa Novemba, insha Allah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu ni muhimu tukawakumbusha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaingia hapa mwaka 2020 Novemba, 2021, 2022, 2023, 2024, 2025 yapo mambo makubwa tulikuwa tunalalamikia katika jimbo letu. Leo nimesimama hapa kwa heshima kubwa kusema mambo yale yamekamilika na ni kutokana na mipango ya Serikali na utafutaji fedha wa Wizara ya Fedha kwa ujumla, chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiyo maana tumeyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kilombero ulikuwa unaweza kufanya yote, lakini kuna lami yao, ile barabara ya lami, kama haijakamilika ile haupati, huwezi kurudi kuchaguliwa tena. Leo ninazungumza hapa, nilikaa chini kwenye kapeti, nilikaa kwenye matope kupiga kelele kupata barabra ile, tumepata fedha, tumeletewa fedha, leo barabara ya lami watu wanateleza kutoka Ifakara kwenda Kidatu lami imekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tumepata Barabara nyingine ambayo imesainiwa, ya Ifakara – Kikwawila – Mbasa – Lipangalala kwenda Malinyi. Tumepata barabara nyingine ya Ifakara kwenda Mlimba, ambayo Mkandarasi kaanza. Ninamwomba tu Mheshimiwa Waziri anihakikishie kwamba, imesainiwa barabara ya Ifakara kwenda Malinyi, basi ianze kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata Daraja jipya la Ruaha, tumepata kiwanda kipya cha sukari, shilingi bilioni 700, Mwenyezi Mungu anipe nini tena. Jimboni kwangu zimekuja karibu shilingi bilioni 750 za uwekezaji za kiwanda kipya cha sukari, K4, ambacho Mheshimiwa Rais ameweka jiwe la msingi na wakati wowote kinaweza kwenda kuzinduliwa, kilichobaki hapa sasa ni tunafuatilia tu kuhakikisha wakulima wetu wanapata haki yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu wilaya imeumbwa sasa hivi tumepata hospitali ya wilaya, vituo vya afya viwili, zahanati 12, sekondari za O’level 12, sekondari za advance tano, shule za msingi nane, madarasa zaidi ya 100, substation ya kuondoa kukatikakatika kwa umeme shilingi bilioni 25. Tumepata miradi ya maji mingi sana na mradi mmoja mkubwa wa shilingi bilioni 41, haijawahi kutokea katika Jimbo la Kilombero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu wilaya imeumbwa, jimbo limeumbwa, hatujawa na Mahakama ya Wilaya. Tumepata Mahakama nzuri ya Wilaya, tumepata Kituo cha Polisi kizuri cha Wilaya, tumepata magari ya polisi, magari ya zima moto, ofisi mpya ya Mkuu wa Wilaya ya ghorofa na minara ya simu zaidi ya sita. Sasa tumepata chuo cha KATRIN, kinaboreshwa, kitakuwa ni sehemu ya kuhaulisha vifaa vya Kilimo. Tumepata miradi ya bonde itakuja kujenga mabwawa ya umeme, Miradi ya TACTIC ya soko jipya, stendi mpya, lami, visima vya maji na tumepata ziara ya Mheshimiwa Rais; amekuja katika jimbo letu kutuzindulia kiwanda na barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya yote makubwa yamefanywa chini ya Wizara ya Fedha na mipango mikubwa ya nchi hii. Ninaunga mkono hoja kwa 100% kwamba, wananchi wakitupa ridhaa tena tutaendeleza yale machache yaliyobaki, ambayo nitasema baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kwenye barabara za mitaa, kuna changamoto kwenye mambo ya bei ya miwa na sukari ambapo tuna imani wakitupa ridhaa tena tutaendeleza kwa kiasi kikubwa. Haya niliyosema ni machache tu, lakini kwa undani wake kuna mambo makubwa sana, wananchi wangu wa Kilombero ninawaomba tushikane mkono na Chama Cha Mapinduzi, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na tusiwasikilize wale wapotoshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna rafiki yangu mmoja na rafiki yake kaka kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, anaitwa John, alikuja na chama chake siku za karibuni akaongea mengi sana ya kuiponda nchi. Anasema nchi gani hii? Inaongozwaje? Imeuza bandari, imeuza sijui nini! Waziri Mwigulu anazunguka tu duniani! Kaponda weee, kamaliza hata tofali moja hajaacha! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuibie siri, nimegundua kumbe wale watu wanaenda kuchangishachangisha pale elfu moja tuchangie mafuta, kumbe zile elfu mojamoja, elfu mbili, wengine wanawapa. Yaani inakuwa kama ile pata potea ya kamari ya Kariakoo, ukisimama ukijifanya unatoa hela unashiriki kwenye kamari kumbe unaliwa wewe, wenzako wanaenda kugawana pembeni baadaye. Kwa hiyo, wanawagawia wachache wanaenda kutoa elfu mojamoja, elfu mbilimbili na wengine wanapeleka mikono mitupu kwenye sanduku lile. Mtu anaongea mishipa mpaka inamtoka, anatukana watu nchi hii haina chochote, nchi hii haifai, nchi imeuza bandari! Mimi nipo Kamati ya Miundombinu na bandari haijauzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia fursa hii kuwaambia wananchi wa Jimbo la Kilombero haya mambo nimeyasema hapa yapo kule, hakuna maendeleo yanayokuja kwa kujengwa siku moja. Tumesema humu mikakati imewekwa, fedha zimetafutwa, tumepata miradi kwa hiyo, wasidanganyike na mtu yeyote, ambaye anataka kuleta propaganda na siasa nyepesi nyepesi, kama kaka yangu huyu John ambaye namheshimu sana, lakini hajabisha kwamba, alilala na kusinzia kwenye treni, kama nilivyosema hapa. Katika Bunge lililopita alikuwa Mbunge alibisha kwamba, Serikali ya CCM haiwezi kujenga SGR, lakini nimemkuta kapanda na kasinzia kwenye SGR. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kasema kule jimboni kwangu kwamba, japokuwa nimepanda nikasinzia, lakini treni sio la baba yako. Sijasema kama treni ni ya baba yangu, nimesema yeye alipinga humu CCM haiwezi kujenga, sasa hivi imejenga na yeye amepanda akasinzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, sisi changamoto kubwa ni barabara za mitaa. Tuna mpango wa kilometa 10 za barabara za mitaa kwa kila kata katika kata 19, imani yetu ni katika mpango ujao wa Serikali tukipata hiyo itatusaidia kupunguza changamoto kubwa za wananchi wetu. Tutasimamia hizi barabara za kuunganisha na wilaya nyingine, kilimo cha miwa, kituo hicho cha KATRIN na haya mabonde ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa ninamalizia yapo mazuri katika bajeti hii na kuna changamoto ambazo tutazishauri. La kwanza ni bima ya afya; wamesema Wabunge wengine hapa na mimi nina maoni, sasa hivi kuna vinywaji ambavyo tunakunywa baada ya miaka 20, 25, watu watapata BP. Kuna kinywaji kimeandikwa kabisa hii usinywe zaidi ya moja, energy, lakini kuna vijana wetu wanakunywa sana huko. Hakuna sababu ya vinywaji kama hivi kupunguza kodi, wekeni kodi iende bima ya afya isaidie masikini wa nchi hii kutibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza sana katika kupambana na HIV/AIDS na mpango mkakati wa kuzuia Bajeti ya Serikali na mitikisiko ya kiuchumi. Kwenye economics wanasema certainty zinazotokea duniani, juzi nimeona Israel na Iran imeanza, bei ya hisa na mafuta ime-shake, athari zitakuja kwetu. Kwa hiyo, wakati huu tupo kwenye bajeti tutazame kama zile shilingi bilioni 500 zinaweza zikajitosheleza zenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono zile kodi zote katika elasticity of demand ambazo mmezipandisha, kwa mfano bia na nini na nini, hivyo ambavyo hata vikipanda bei watu wataendelea kunywa, ili viendelee kusaidia masikini. Viuatilifu wamepunguza kodi, nyongeza ya mishahara naunga mkono, kuwajali bodaboda na bajaji naunga mkono, namuunga mkono TRA, Mwenda anakusanya kodi bila kusumbua wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Mheshimiwa Waziri amesema, katika sera hapa kwamba, hakuna kanuni inayokuja sasa, biashara hazitafungwa tena; ni jambo kubwa sana ninaliunga mkono na kwa kweli, tunatakiwa tumpongeze sana Kamishna wa TRA, hata juzi nilikuwa TRA pale. Nimeona asubuhi kwenye maswali hapa, kwamba, watu wanasema ile TIN miezi sita bado watu wanatozwa, mimi sijatozwa. Kwa hiyo, wameshafanya kazi kubwa na nimeona mfano mzuri kutoka TRA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishati safi 80% kufikia 2034 ni jambo kubwa, ujenzi wa Makao Makuu Dodoma ninaunga mkono, kupandisha mishahara kima cha chini mpaka laki tano, ninaunga mkono na mkakati wa kupunguza importation na kuongeza exportation katika economics ni jambo la msingi sana. Mheshimiwa Waziri tunakutana na watu kibao, China kule Guangzhou, lakini ni muhimu tukawa na mipango na Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango, mtu anaenda China tum-discourage kama anaenda kununua ma-toy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakutana na watu kule, China, dada zetu wengine mpaka unamshauri cha kununua. Yaani mtu anasafiri anaenda China anafungasha ma-toy wakati kuna bidhaa za msingi. Katika nchi yetu tunaweza ku-discourage vile vitu ambavyo havina maana kwa kuongeza kodi na kupunguza kwa vile vya muhimu, kama majembe ya umeme; sasa hivi kuna jembe unalivaa mgongoni tu hapa, linalima kama mota, tu-discourage wale wanaenda China kununua ma-toy na vitu ambavyo sio muhimu sana, ili kupunguza importation na kuongeza exportation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa kumalizia changamoto na maoni yangu ni suala la kodi kwa hisa ambazo hazijagawanywa kwenye kampuni. Ninashauri Mheshimiwa Waziri, mjaribu kulifikiria, hili haliwezi kuwa double tax, sisi tuna kampuni yetu tumepata faida, tumelipa kodi zile hisa ambazo hazijagawanywa, nafikiri Mheshimiwa Waziri atanisaidia kulifafanua vizuri jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, wakandarasi walipwe. Kuna miradi ya maji kule kwangu, kuna mzee wangu mmoja mpaka leo bado hajalipwa. Ninaomba alipwe na hapahapa Mheshimiwa Waziri nasema kwamba ni muhimu sana kabla ya kusaini miradi mingine mipya, hii mikubwa ya Serikali, ambayo imesainiwa basi ikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia, Mheshimiwa Waziri watoe elimu kuhusu Deni la Taifa. Ninataka niwahakikishie kuna watu wanapotosha kuhusu Deni la Taifa na wengine wanafikiri Mheshimiwa Waziri Mwigulu akikaa pale anajiamulia tu kukopa. Kuna mwananchi wangu mmoja nilikuwa namwelimisha juzi, anafikiri Waziri Mwigulu nyuma ya mlango wake kule kuna fedha za wananchi. Anasema, bwana mafedha si anakaa nayo Wizarani pale na Waziri Mwigulu anavyong’aa hivi, basi anajua basi yeye ndiyo anakula tu fedha zetu, pole sana kaka yangu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inabidi mtoe elimu kuhusu Deni la Taifa kwa sababu, watu wengi sana wanapotosha. Kwa kumalizia naomba kusema kwamba, kwenye ujenzi, mabati ya gauge 30 sisi watoto wa fundi cherehani ndiyo tunatumia kujengea, kodi iwe zero. Nondo kwa mfano, chini ya milimita 16 ambazo tunajengea kwenye nyumba zetu kule kodi ipungue, cement ile 32.5% ipungue. Sisi tunajenga kwa matofali ya kuchoma na tope, tukifika pale tunakazia na nondo milimita 10, 11, mabati yangu mimi ni ya gauge 28 hayo, waweke kodi kwenye miradi huko, kwa wakandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bati gauge 30, ukikunja hivi linakunjika, kodi ya nini? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mwigulu, amefanya kazi nzuri sana ili tuendelee kujenga nyumba huko tunakokwenda, wananchi wetu ni vizuri sana wakawasaidia katika kupunguza kodi katika vitu ambavyo wanavifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni dunia ya artificial intelligence. Juzi nilikuwa ninaona hata kama hujasoma accounting kuna course ukisoma miezi mitatu unaweza kufanya uhasibu, kama mhasibu, dunia ambayo tunaenda. Tunaomba sana, wwekeze huko wanakoenda katika mipango ya Serikali hii. Kama mwanafunzi anachukua mtihani anaupiga picha chaa! Unaenda artificial intelligence, unaleta majibu, ni dunia nyingine kabisa ambayo tunakuja nayo. Kwa hiyo, ni muhimu sana kupambana nayo hiyo, kuhakikisha tunaiendeleza nchi yetu katika sekta kama hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninakushukuru sana. Tutacheza na tutashinda insha Allah, ahsante. (Makofi)