Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Awali ya yote kwanza ninachukua nafasi hii kwa dhati kabisa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Bahi kwa kuniamini kuwa mwakilishi wao ndani ya miaka hii mitano. Kwa ushirikiano wao na kwa pamoja na Serikali, wilaya na jimbo letu tumeweza kupata maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali. Ninapenda kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa heshima kubwa hii ambayo wamenipa na nataka niwaahidi kwamba, bado nina nia ya kuendelea na sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu katika Ukanda wa East and Central Africa inaongoza kwa uzalishaji wa mahindi na kwa kiasi kikubwa Tanzania inategemewa. Biashara ya mahindi kwa East and Central Africa ni takribani dola bilioni 6.7, lakini the epicenter mzalishaji mkubwa akiwa ni Tanzania na mwaka jana, 2024, tulipata mavuno jumla ya tani milioni 8.01, lakini 70% ya uzalishaji huu ni jembe la mkono, 20% ni jembe la kukokotwa na ng’ombe na 10% ni mechanization.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kiasi kikubwa pamoja na kwamba, tu sisi tunategemewa kwa Afrika Mashariki na Kati katika kuzalisha mahindi, lakini bado tunatumia jembe la mkono kwa sababu, 70% ya wakulima wetu ndio wanaochangia na wanatumia jembe la mkono. Ninadhani inatakiwa tuwe na kampeni mahususi ya kutoka kwenye jembe la mkono twende kwenye jembe la kukokotwa na ng’ombe; kama ambavyo tulifanya kampeni mahususi ya kumtua mama ndoo kichwani na kampeni mahususi ifanyike ya kuachana na jembe la mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa jembe la ng’ombe linauzwa 160,000 kwa bei ya rejareja, bei ya jumla ni 130,000, lakini majembe haya yanazalishwa nje ya Tanzania. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali, kwanza ichukue hatua madhubuti ya kutafuta muwekezaji aje kuweka kiwanda hapa cha kuzalisha majembe yanayokokotwa na ng’ombe, lakini vilevile, kama ambavyo tunatoa incentives kwa uwekezaji, huyu apate incentives kubwa sana, ili wananchi wetu waweze kupata jembe hili walau kwa 80,000 au 100,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi tunaenda kuachana na kilimo cha kutumia jembe la mkono ambacho si kilimo, ni kilimo cha adhabu, ile ni corporal punishment. Kwanza kinakuzeesha, lakini vilevile unalima huku upo kwenye adhabu kwa hiyo, ninaomba Bajeti ya Serikali iangalie kumtafuta muwekezaji wa majembe ya kukokotwa na ng’ombe, tutoke kwenye 20% sasa tupande, tupunguze kule kwenye 70%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa mahindi kwa nchi yetu, umwagiliaji ni asilimia 2.5 tu. Mahindi yote haya asilimia kubwa yanategemea mvua kwa hiyo, kilimo chetu bado ni cha kubahatisha na utaalam unaonesha kilimo cha umwagiliaji, kilimo cha kawaida cha mvua kinatoa tani 1.6 kwa hekta, lakini ukimwagilia kinatoa takribani tani tatu mpaka 5.7 kwa hekta. Kwa hiyo, kwa vile nchi yetu inategemewa kwa uzalishaji wa mahindi ipo haja ya kubadili Kilimo chetu, badala ya kuwa tunategemea mvua sasa kiwe kwa umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Kanda ya Kati tumekuwa waathirika zaidi, mwaka huu tuna mvua, mwaka mwingine hatuna mvua, njaa kubwa, hakuna njaa. Kwa hiyo, Serikali iangalie jambo hili kwamba, sasa tutoke kwenye kutumia mvua katika kilimo cha mahindi kiwe cha umwagiliaji. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kuongeza mavuno ya kutosha na vilevile wakulima wetu waweze kupata ahueni kubwa sana ya kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majembe; jembe la kukokotwa na ng’ombe Serikali ifanye uwekezaji, lakini vilevile kwa sasa kivutio kubwa cha kilimo ni kwenye bustani na matunda, ambayo tuseme ni horticulture. Kilimo hiki kinavutia zaidi vijana kwa sababu, vijana shuruba ile ya kutumia jembe la mkono wengi hawaiwezi kwa hiyo, wanaenda kwenye bustani, lakini kwenye bustani umwagiliaji unatakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo pump za umwagiliaji ambazo hutumii solar energy wala umeme, unatumia nguvu yako, kama ile pump ya moneymaker inauzwa shilingi laki tano, lakini nayo inazalishwa kutoka nje. Kwa hiyo, eneo hili nalo Serikali iangalie kwa makusudi kabisa iweke mwekezaji, kwa ajili ya kuzalisha mashine hizi. Tukifanya hivyo, tutaenda sawasawa na Sera ya Wizara ya Kilimo, ambapo wameongeza, wameleta magari, kwa ajili ya kutoboa visima vya umwagiliaji vijijini, tukiwa na eneo hilo tutaweza kuwapa vijana wengi fursa ya kununua mashine hizi, hizi pump, ili waweze kufanya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu uwekezaji wa kilimo, sambamaba na reli ya SGR. Ukitoka kuanzia Soga station unashuka sasa huku huoni shamba lolote la kilimo la kibiashara. Mgeni akitoka nje ya nchi akipita kwenye reli anaona nchi hii hawalimi, completely hakuna commercial farms, hakuna hata kilimo cha nyasi; kutoka Soga unapita pale Ruvu, maji yanatiririka hakuna hata kilimo cha matunda, hakuna hata kilimo cha nyasi, hakuna umwagiliaji, unakuja unashuka ukija Dodoma kwetu, huku sasa ndiyo kukavu. Kwa hiyo, mgeni akija jambo la kwanza atashangaa, nchi hii mbona hailimi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli ukitembea along reli huoni kama tunalima. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali kwanza ukiwekeza sambamba na reli unatengeneza logistic harbour nzuri za matunda na mbogamboga kwenda kuzipeleka katika masoko, lakini vilevile kama nilivyosema kuondoa aibu kwamba, nchi hii hawalimi ni kuweka commercial farms. Bahati mbaya Mkonge upo kule kwenye barabara, lakini kwenye reli hakuna kabisa ni nyasi. Kwa hiyo, Serikali iangalie namna ya kutoa aibu hii ambayo mtu akija anajua hawa watu hawalimi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kwa dhati kuipongeza Serikali, kwenye suala zima la kilimo imefanya uwekezaji mkubwa hususani katika sekta ya mabwawa. Kwenye mpunga tumeona fedha nyingi zimeenda, karibu mabwawa 780 yameweza kujengwa katika kipindi hiki cha miaka mitano, lakini kubwa zaidi tumeona ubunifu mkubwa uliofanyika wa kuwa na magari ya kuja kutoboa visima kwa wananchi wa vijijini badala ya kutumia maji, kwa ajili ya kunywa na matumizi mengine sasa twende katika sekta kubwa ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninashukuru sana. Ninampongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo katika kipindi hiki cha miaka mitano ya uongozi wake tumeona mapinduzi makubwa ya utekelezaji wa bajeti hii, ambayo imeenda zaidi ya nusu, ambavyo wakati mwingine ilikuwa haiwezi kufikia katika kiwango hiki. Ninakushukuru sana. (Makofi)