Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii, lakini ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kunipatia nafasi hii tena ya kuchangia kwenye Bajeti Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yetu hii ni bajeti ya kimkakati. Ukisoma utakutana na mambo ambayo yanaonyesha wazi kwamba kuna mambo ya kimkakati yameingia huku ndani. Kwa mfano wanapendekeza kwamba tunakwenda kusamehe ongezeko la VAT kwenye viuatilifu, (viua wadudu) kule mashambani na codes zake zimeonyeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake kwenye Sekta ya Kilimo tunakwenda kufanya vizuri kwa sababu sasa wadudu wanaosumbua mashambani kwa kuondoa tu hiyo VAT tutakuwa na uwezo wa kuwafikia wengi zaidi na wataweza kufanya vizuri kwenye mashamba yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiendelea unaona wanapendekeza kusamehe VAT kwenye miamala ya bima. Tunaona kabisa kwamba tunakwenda kuimarisha bima za kwetu hapa nchini ambazo vilevile zitakwenda kuvutia watu wengi kushindana na hizo kampuni nyingine na wakati huo huo kuongeza ajira kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona vilevile tunakwenda kuondoa VAT kwenye bidhaa za nguo ambazo zinaenda kutumia pamba inayotoka Tanzania. Kwa hiyo, utagundua kwamba pamba tunayolima sisi sasa itakwenda kuwa kama tumeongeza unafuu wa wale wakulima wetu kule shambani, kwa sababu ina maana viwanda tulivyonavyo ndani ya nchi hii vinavyotumia pamba hii ya kwetu vitakuwa vimepunguziwa VAT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiendelea utagundua yako mengi yaliyotajwa. Mafuta yetu ya kula yameondolewa VAT. Yalikuwepo majaribio ya mwaka mmoja, sasa tunakwenda kuendelea na zoezi hilo. Tunaweka unafuu kwa Mtanzania wa kawaida aweze kununua mafuta yaliyo safi ndani ya nchi hii na hivyo hivyo kuweza kuviongezea uwezo viwanda vyetu vinavyotengeneza mafuta haya ya kula ambayo yatakuwa yanatumika nchini na wakati fulani yataweza kuuzwa hata nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kabisa kwamba kwenye bajeti hii wanakwenda kuweka unafuu au kuondoa kabisa VAT kwenye ununuaji wa matairi ya matrekta. Tunajua kabisa kilimo kwenye maeneo mengi ndani ya nchi hii kuna sehemu wanatumia matrekta. Sasa tunaenda kuyapunguzia haya matreka VAT hii. Maana yake mwenye trekta sasa anakwenda kupata matairi kwa bei nafuu kidogo. Maana yake ni kwamba tunakwenda vilevile kuwezesha kilimo chetu kiwe cha kisasa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona pia wamesema wanakwenda kupunguza au kuondoa VAT kwenye gesi silia. Ukiondoa kwenye gesi asilia maana yake unaongelea habari ya kufanya sasa gesi asilia iwe na bei nafuu ambayo inaweza kutumika na watu wengi zaidi. Wanajua kabisa kwamba tumekuwa tunazungumzia ndani ya nchi hii kwamba tunahitaji ikiwezekana magari ya Serikali sasa yatumie gesi hii kwa ajili ya kupunguza gharama ya mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiona bajeti ambayo inaongelea sasa kuondoa VAT kwenye eneo hili unaijua hii ni bajeti ya kimkakati. Kwa hiyo, yako mengi ambayo yameandikwa na ninaamini kabisa yakitekelezwa haya tutakwenda kuona unafuu mkubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tena kwenye Sura ya 342 ya kodi zetu, wamesema wanaenda kuweka unafuu katika kuondoa kwenye kodi ya mapato ya pikipiki au vifaa vyenye matairi mawili (pikipiki au bodaboda hizi) na guta ambavyo vinafanya kazi kubwa sana kule vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoondoa hiyo kodi ya mapato ikirekebishwa kule kwenye pikipiki (bodaboda), tuna watu wengi sana Tanzania sasa hivi ni bodaboda wameajiriwa kwenye Sekta hii. Kwa hiyo, maana yake tunaweka unafuu mkubwa kwenye wananchi wetu kule kwenye maeneo yale. Kwa hiyo, yako mengi ambayo yamesemwa hapa, ndiyo sababu nikasema hii inaonekana kabisa ni bajeti yetu ya kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, wataalam na Naibu Mawaziri, kwa kazi kubwa ambayo wamekuja nayo hapa ambayo inatupeleka mahali fulani ambapo tunapaona kwamba patakuwa ni pazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani au utekelezaji wa bajeti iliyopita. Tutakumbuka wazi kwamba tumeona hakuna sekta yoyote ambayo inaonekana imesimama kama ilivyo. Bajeti yenyewe ya mwaka jana ilikuwa shilingi trilioni 50.29 na bajeti ya mwaka huu imekwishakwenda kwenye shilingi trilioni 56.49. Maana yake kuna mambo yanakwenda kuongezeka hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba iko michango mingi imetoka huko nyuma ikionyesha kwamba inawezekana tuki-equate na kwenye dola tukaona kama bado siyo kubwa sana, lakini kiukweli ni kwamba bajeti imeongezeka na mambo makubwa yanakwenda kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye pato la Taifa tunaona kabisa kwamba pato la Taifa limekua kwenda kwenye asilimia 5.5. Ni kweli, uhalisia kwenye researchers unaonyesha wazi kwamba kama itakuwa linakuwa chini ya asilimia nane maana yake bado tutakuwa hatuendi vizuri sana. Kwa hiyo, niwapongeze watangulizi waliolisema hili kwa sababu hii ni wazi kwamba tunatakiwa tuendelee kusimamia hizo sekta za uzalishaji, zitutoe hapa tulipo twende kwenye pato la asilimia 8.8 kwenye ukuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hizo kwenye utekelezaji, ukiangalia utekelezaji uliopita kwenye mwaka wa fedha uliopita yako mambo mengi yametokea ambayo yanatuashiria kwamba kama tukisimama imara tunaweza kwenda vizuri zaidi kuliko hata ilivyokuwa mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme, tunajua wote umeme ilikuwa ni changamoto lakini Bwawa la Mwalimu Nyerere lenye megawati 2,125 limekwishaongezea kwenye umeme. Hoja yetu kubwa sasa kama Wizara ya Fedha ni kuwezesha umeme huu sasa utumike kwenye viwanda tulivyonavyo na upatikane bila kuwa na interruption (usikatikekatike).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa tuliyonayo tena pamoja na kuwa na umeme ni ndugu zangu wa Viwanda kuhakikisha kwamba tunapata viwanda. Wale ambao tumehudhuria mawasilisho mengi imeonekana hata ile American First inatupatia sisi tariff ya chini. Tuna uwezo wa ku-attract wawekezaji wengi wakaja huku kwetu na tukaendelea kufanya vizuri zaidi tukiwa na umeme huu tulionao.
Japokuwa kwenye umeme bado tunatakiwa tuendelee kuweka mkazo kwamba, tunatakiwa tuongeze umeme kwa sababu, baadaye umeme tulionao utakuwa kidogo, ndani ya miaka mitano tu ijayo kwa sababu, uzalishaji utakuwa ni mkubwa. Tumeona kuna ujenzi wa daraja ambalo linafunguliwa tarehe 19, la Busisi – Kigongo. Ninatokea eneo lile, pale tulikuwa tunavuka kwa nusu saa, sasa hivi ninakadiria tutavuka kwa dakika sita au saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sawasawa na SGR, tulikuwa tunasafiri kwenda Dar es Salaam kwa saa tisa, sasa tunakwenda kwa saa tatu na robo. Ukicheza na muda maana yake ni tayari ile sehemu inayobaki, wale wanaosoma grant activities zile utagundua, kama muda unaobaki tutaufanyia uzalishaji wa kitu kingine. Kwa hiyo, tutakuwa tunainua uchumi wetu kwa kadri ambavyo tunacheza na muda ule. Ukiangalia, pamoja na hiyo SGR, kuna vipande vingine ambavyo navyo kwenye bajeti iliyopita vimeanza kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo cha Tabora, cha Isaka kwenda Mwanza kimeshakwenda 14% cha hapa kutoka Makutupora kwenda Tabora kipo asilimia takribani sita na vingine; kwenda Makutupora hapa kimeshakwenda kwa percent kubwa. Tuendelee kuweka mkazo kuhakikisha kwamba, haya mambo yanakamilika, kama tutaweza kuwa na reli inayotoka hapa kwenda Mwanza, inayotoka hapa kuunganisha Kigoma, uchumi huu utakimbia kuliko unavyokwenda leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya niliyoyazungumza hapa tuna mambo kadhaa yametokea kwenye sekta mbalimbali. Tumeona kwenye Sekta ya Elimu, wamelinganisha kutoka uhuru mpaka leo, kuna mahali fulani unaona uvivu kuisema kwa sababu, kuna mahali labda vyuo vilikuwa 41 leo vipo 2,000 na kitu, maana yake ni kwamba, kazi iliyofanyika ni kubwa sana. Sasa kama sekta hizi zimeshafanya kazi kiasi hiki, kazi yetu kubwa kwenye bajeti hii ni kuongeza kuchochea kuhakikisha kwamba, kwenye elimu tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaonekana tunakwenda vizuri, lakini kwenye kilimo twende vizuri, kwenye ufugaji twende vizuri kwa sababu, hizi sekta za uzalishaji ndiko mahali tunapoweza kupata mapato haya, yakapanda haraka. Hata haya yanayoongelewa, yanaonekana ni madeni, tunaweza kuyalipa kwa urahisi kwa sababu, sekta za uzalishaji zimefanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunategemea kuwa na skimu za umwagiliaji. Leo hii yapo maeneo mengi ambayo tungetegemea skimu ziwepo, hatujaenda vizuri sana kule, ni kwa nini? Inawezekana tulibajeti kwamba, tutapeleka shilingi trilioni moja, lakini fedha iliyokwenda ni shilingi milioni 600 au ni bilioni 600 au bilioni 500, maana yake ni ile shilingi bilioni 500 ambayo haijaenda zile skimu hazijakamilishwa kama tulivyotarajia na matokeo yake sasa ni kile ambacho tunakifikiria, kama tunakwenda kwa kiwango hicho, tunakuwa hatujaenda kwa kiwango tarajiwa. Kwa hiyo, nawaomba sana, yale ambayo tumeyasema kwenye uzalishaji, leo tunasema tulikuwa na viwanda viwili au vitano vya nyama, lakini je, hiki ambacho tunakifanya sasa hivi tunaweza kukifanya tena miaka mingine miwili tukawa na viwanda labda 20 au 30, ili tuweze kuuza nyama yetu nyingi na maziwa mengi nje ya nchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna kazi kubwa kwenye bajeti hii tunayoishughulikia sasa hivi tuhakikishe kwamba, inakwenda kututoa mahali fulani kwenda mahali pengine kwa sababu, kilichoongezeka, kiongezeke vilevile katika uzalishaji kwenye sekta za uzalishaji. Tofauti na hivyo tunaweza kuwa tunafanya maoteo makubwa na kama inakwenda kidogo basi hatutaona matokeo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda ninaomba niunge mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)