Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja hii muhimu sana ya Bajeti Kuu. Kwanza ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuhusu kuwa hapa leo. Nimekuwa katika Bunge hili la Bajeti ambalo linakamilisha Bunge letu hili la Kumi na Mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kwanza kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutuongoza vizuri na Falsafa zake za 4R ambazo zimedhihirisha kwamba tunakwenda vizuri katika masuala yote na kwa kutuletea bajeti hii ambayo nitaiita ni bajeti ya kimkakati, bajeti bora kabisa ambayo nitaelezea huko mbele kwa nini nimeiita hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa vilevile kuwapongeza wasaidizi wa Mheshimiwa Rais ambao ni Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango; Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa; Naibu Waziri Mkuu Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko na wengineo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa waandaaji wa bajeti hii nao ninawapongeza rasmi Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo pamoja na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa kututengenezea kitu kizuri. Kwa sababu ya muda, ningependa vilevile kuwapongeza wasaidizi wao wote, nisiwataje majina; Naibu Mawaziri wote, Makatibu Wakuu na kadhalika kwa kutuletea kitu kizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bajeti ni ya kimkakati kwa sababu ni kiunganisho kati ya mpango huu unaokwisha na ule mwingine unaoanza. Pia unafurahisha kwa sababu ukiuangalia muunganiko upo (kuna mwendelezo wa mambo yaliyopita na mambo ambayo tunayatarajia yatakuja). Kwa hiyo, ni kitu ambacho tunaanza kuona faida ya kuwa na Wizara kabisa ya Mipango na Tume ya Mipango, yaani ule muunganiko unaonekana vizuri na inaoana kama ambavyo inavyotarajiwa ili kuleta mwendelezo mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha uliopita 2024/2025 tulipanga kutumia shilingi trilioni 50.29 na hadi kufikia Mei tumetumia 89.6%. Kwa hiyo, tunatumia vizuri kadri tunavyopanga. Pia ukiangalia tuliopanga kutumia, tumetumia 85.3% ya hayo makusanyo. Kwa hiyo, hiyo inaonyesha tunatumia kadri tunavyopata. Basi tuboreshe makusanyo ya huko ambako tunakokusanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, nikiangalia vipaumbele vya bajeti vya mwaka huu kama ambavyo vimewekwa kwenye mpango, viko vitano.
(i) Kuna kuchochea uchumi shindani na shirikishi;
(ii) Kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma;
(iii) Kukuza uwekezaji wa biashara;
(iv) Kuchochea maendeleo ya watu; na
(v) Kuendeleza ujuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kwa nini ninasema ni bajeti ya kimkakati? Ukiangalia Dira tarajiwa hii ya mwaka 2050 ina nguzo tatu. Nguzo ya kwanza ni uchumi shindani na shirikishi na ukiangalia kwamba hiyo nguzo ndiyo hiyo hiyo ambayo ni kipaumbele cha bajeti yetu. Kwa hiyo, unaona muunganiko unakuwa ni mzuri ambao unatuletea matumaini makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nguzo ya pili ni uwezo wa rasilimaliwatu. Kwa hiyo, ukiangalia bajeti hii ilivyokuja rasilimaliwatu imepewa kipaumbele sana kwenye elimu. Bajeti ya Elimu inaashiria mkazo mkubwa katika kuendeleza rasilimaliwatu. Vilevile, kwenye afya bora, Bajeti ya Elimu nayo iko vizuri kwa kuonyesha kwamba tumeweka kipaumbele kikubwa katika kuboresha afya za Watanzania. Vilevile, tumeweka vigezo vya kuwa na rasilimaliwatu ambayo wamehamasika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nguzo ya tatu ni mazingira bora yenye kuhimili mabadiliko ya tabianchi na hii yote inajengwa na ile misingi miwili ya kwanza. Vichocheo ambavyo vimepangwa katika dira yetu hiyo, cha kwanza ni usafirishaji jumuishi. Hii wanaita Integrated Logistics na ukiangalia hotuba ya Bajeti Kuu, hii usafirishaji umepewa umuhimu mkubwa. Kwa hiyo, tutakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; kuna sayansi na teknolojia; nimepitia ile bajeti, hotuba ya Wizara ya Elimu inaonyesha kwamba kuna mkazo mkubwa kwenye sayansi na teknolojia, mpaka kuna bajeti za wanafunzi waliofanya vizuri katika sayansi wanapewa scholarship. Kwa hiyo, ni vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; kuna hili la utafiti na maendeleo na ubunifu wa RND ambayo nayo imeongelewa na wenzangu waliotangulia. Kwa hiyo, sitairudia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia hapa kuna muunganiko mzuri sana kati ya Dira tarajiwa hiyo ya 2050, Mpango wa 2025/2026 pamoja na Bajeti Kuu. Sasa, nikiingia kwenye Bajeti Kuu moja kwa moja, nikiangalia katika aya ya 138 mpaka aya ya 170 kuna mabadiliko ya sheria pendekeze ili kuongeza uzalishaji katika viwanda vyetu. Hizo ni hatua za kikodi ambazo zimefanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia kwa mfano aya ya 139 kuna kusamehe VAT kwenye vipuri vya matrekta, magurudumu na kadhalika. Aya ya 146 kuna kudhibiti uingizaji wa bidhaa mbalimbali: nondo, misumari na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, hili la nondo nilitaka niliulizie hapa. Juzi nilipita kwenye site moja huko ambako tunakopitapita sisi wahandisi, nikavutiwa na kuangalia nondo. Nondo hizi zinatoka wapi? Nikabaini kwamba nondo hizi zinatengenezwa hapa hapa nchini, kampuni sitaitaja kwa sababu itakuwa namtangazia biashara, lakini viwango vyake ni vile vile ambavyo tunavitaka, ambavyo zamani tulikuwa tunaulizia kwamba tunataka nondo tunasema ya BS (British Standard). Pia, ukiangalia hata hizi, viwanda vyetu vimeweza kutoa nondo za hali ya juu kiasi kwamba unaona wazi kwamba tunakwenda vizuri kulingana na mpango na tunakwenda vizuri kulingana na Dira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, hivi viwango vya kikodi vimelenga hasa katika kulinda bidhaa za ndani. Hii inakwenda vizuri lakini sasa ambacho sikukiona ni mpango au marekebisho ya sheria ambayo yanakwenda kulinda huduma hasa na nitaongelea hapa huduma za wakandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakandarasi wa ndani ambao wanatoa huduma nzuri kwetu sisi ambao tunataka hawa wakandarasi waweze kukua. Vilevile, waweze kutoka hata nje ya nchi yetu kwenda kufanya kazi zao hizo za ukandarasi. Sasa, ili wafanye hivyo na huduma hii nayo inabidi tuilinde ili iweze kufikia mafanikio hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sheria ambazo zinalalamikiwa na hawa wakandarasi, basi hizo nazo tuzijumuishe katika mipango ya baadaye ya kuziboresha ili tuweze kuwa na wakandarasi ambao wanakuwa na ambao wanahamasika ili waweze kutoa huduma nzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependekeza kwa Waziri wa Fedha, lakini hata awamu ya sasa au ya baadaye waangalie. Kwa mfano wakandarasi, sheria ambazo wanazilalamikia sana ni sheria za kikodi ambazo wanalazimika kulipa kodi kabla hawajapokea fedha zao za kazi waliyoifanya. Sasa, hili linawaumiza kidogo. Kwa hiyo, katika haya mapendekezo ambayo ni ya kikodi ya kulinda bidhaa za ndani, basi tuwajumuishe na wao katika sheria za kikodi ambazo zitawalinda nao waweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anapofanya kazi mkandarasi anapopewa ile certificate tayari TRA mwezi huo huo wanadai VAT ya gharama ile aliyotakiwa kulipwa. Sasa, ile anakuwa anatozwa fedha kabla hajapokea ile fedha. Kwa hiyo, kama mapendekezo ya sheria hizi yakiwajumuisha na wao itawasaidia sana ili waweze kupata cashflow nzuri, waweze kukua na waweze kuhamasika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wa mwaka huu vilevile nimeangalia pale ukurasa wa 104 mpaka 122, Kiambatanisho Na. 1, kuna orodha ya miradi 423 ambayo imepangwa kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha na miradi hiyo jumla yake ni shilingi trilioni 15.86. Ni vizuri kabisa kwamba miradi hii imo kwenye mpango, lakini miradi hii ukiiangalia, ukiifanyia uchambuzi utaona iko ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mikubwa, kuna miradi midogo, kuna miradi ambayo imekwishaanza kutekelezwa na kuna miradi ambayo ni mipya. Sasa, ninapendekeza kwa Waziri kwamba, kipaumbele kiende kwa miradi ambayo imekwishaanza ili iweze kukamilika na tuweze kupata manufaa yake ili isaidie katika kuendeleza pato la Taifa kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ambayo inayokaa kwa muda mrefu bila kukamilika, isipofanya hivyo kwa mapema inazua riba ambayo tena inatuletea gharama ambazo hatuzitarajii. Hivyo, ningeshauri miradi ambayo imekwishaanza ndiyo hiyo ambayo tuendelee nayo na tuikamilishe ili tuweze kupata manufaa yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia kengele imelia. Ninakushukuru kwa hayo, ninapenda kuunga mkono hoja na kuahidi kwamba katika siku ya kupiga kura bajeti hii nzuri nitaipigia kura ya ndiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)