Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana ya Wizara ya Kilimo kwa ustawi wa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu kwa miaka minne nchi yetu imeshuhudia mapinduzi makubwa sana katika sekta ya kilimo. Sensa pekee tuliyofanya kwa kipindi hiki imetuonesha kwamba Watanzania wengi zaidi ya 70% wanategemea shughuli za kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bajeti hii ni bajeti ya Watanzania walio wengi na Mheshimiwa Rais ameendelea kutuheshimisha kwa kuweka ongezeko kubwa sana la bajeti na mpaka sasa tunavyozungumza, tunazungumza bajeti ya shilingi trilioni 1.2; haijawahi kutokea katika historia ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ambayo inasimamia Wizara hii. Wizara hii imekuwa ni Wizara sikivu kila tunapoishauri, tunabadilishana mawazo na mwisho wa siku wanakwenda kutekeleza yale tunayoshauriana kwa mustakabali mzima wa Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, tulikuwa na mtikisiko mkubwa sana mwaka jana katika bajeti ya mwaka 2023/2024 katika suala zima la sukari. Wote tunajua namna gani tulitikisika humu ndani, tunajua namna gani Watanzania walitikisika, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisimama imara, Waziri alisimama imara, Kamati ilisimama imara, Bunge hili lilisimama imara na mpaka sasa tunavyozungumza, sisi Wanakamati tumekwenda kutembelea kiwanda ambacho kimefanya extension na extension hiyo ikikamilika suala la sisi kuagiza sukari litakuwa ni historia kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaamini kwamba mapinduzi makubwa yanayofanyika katika kilimo katika Serikali hii ya Awamu ya Sita yanakwenda kupunguza ikiwezekana kuondoa kabisa changamoto ya umaskini kwa Watanzania wote. Kati ya vitu ambavyo pia sisi vijana wa Kitanzania tutaendelea kumpenda, kumuombea na kumshikia bango Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni katika kutushirikisha sisi au kuona haja ya kushirikisha vijana na wanawake katika kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisimama mbele ya Afrika nzima katika kikao kilichofanyika pale Dar es Salaam cha Usalama wa Chakula, akaahidi Afrika nzima kwamba nchi hii inakwenda kuhakikisha inashirikisha vijana na wanawake katika kilimo na kuhakikisha tunakwenda kuondoa kabisa changamoto ya usalama wa chakula; kwanza, kwa nchi yetu, kwa Afrika na ikiwezekana tutailisha dunia nzima na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesimamia msimamo huo na mimi kama mwanakamati nipo hapa kushuhudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, programu ya BBT tulianza rasmi Machi, 2023. Tulianza kwa kuhakikisha tunaweka vijana na wanawake katika kilimo. Kwanza, kuhakikisha tunawawezesha lakini tunawavutia na kuhakikisha tunawawekea miundombinu bora ili pale wanapoingia katika kilimo, kilimo hicho kiwakomboe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza sasa tuna miaka miwili tangu tuanze programu hii na programu hii watu wengi walishikilia bango katika kitu kimoja tu, lakini programu hii ya BBT ina vitu vitano; moja, ina mashamba makubwa ambayo ndio block farming; lakini mbili kuna BBT financing ambayo ni suala la kuwawezesha kiuchumi wanawake na vijana katika kushiriki kwenye shughuli za kilimo. Pia tuna suala la uchimbaji wa visima kwa wakulima wadogo kwenye BBT, lakini tuna suala la BBT ugani na pia tuna suala la value addition kwenye BBT. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la mashamba makubwa tulianza na ku-recruit vijana kama 812. Vijana wale walipewa mafunzo na mwisho wa siku walihitimu kupitia mafunzo ya JKT vijana kama 600 na kitu. Tunavyozungumza sasa pilot phase imefanyika katika mashamba makubwa mawili; Chinangali na Ndogoe na mpaka tunavyozungumza sasa sisi Wanakamati tumetembelea zaidi ya mara moja, mara mbili kwenda kuangalia nini kinaendelea pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wale wamejengewa nyumba. Zaidi ya 80% ya vijana wale waliopo katika kambi zile za mashamba wanaishi kwenye nyumba ambazo waliahidiwa. Pia vijana wale wa Chinangali wamepewa kila kijana ekari tano, lakini kwenye Shamba la Ndogoe kila kijana ekari moja. Vijana wale wametengenezewa miundombinu kwa ajili ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu nyingine ambako utaratibu unaendelea kuweka central pivot system ya umwagiliaji, lakini kuna kwingine drip system zimekwisha kamilishwa. Pia kuna bwawa linaloweza kubeba maji takribani lita milioni 27 limekwishajengwa katika Shamba la Chinangali, wale vijana wanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote tunajua nchi hii ina miaka 60 ya uhuru, lakini dunia hii imetokea mbali. Maendeleo ni hatua, hatuwezi kuwa tumeanzisha BBT mwaka 2023 leo hii mwaka 2025 tukataka tuwe tumekamilisha ila sisi tuliokwenda kuona na tunasimamia tunakiri kwamba hatua zilizofikiwa ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaamini na tulishauri kwamba ile system iliyotumika ku-recruit wale vijana imeacha vijana wengi wakiamini kwamba na wao wangefaa kuingia mle. Mheshimiwa Waziri, tunakushukuru ulikuwa msikivu ukasema hapana tushushe katika ngazi za halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza sasa zaidi ya halmashauri 20 kwa maana ya halmashauri 21 katika mikoa tisa, zimekwishaanzisha system za BBT, lakini tunavyozungumza sasa halmashauri zipo katika mazungumzo na Wizara yetu kuhakikisha zinatenga maeneo. Maeneo haya yanapatikana na Wizara inaingia kuanzisha haya mashamba makubwa ili kijana asilazimike kuomba katika ngazi ya Taifa, kila mmoja katika halmashauri yake apate kufikiwa na neema hii na hiki ndicho tunachosema kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhia kwamba vijana wajikomboe katika umaskini na wajiajiri kupitia kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la visima juzi tu hapa tumeona Mheshimiwa Waziri, ametutangazia kwamba kuna magari 12 yameshakuja ya kuchimba visima. Visima zaidi ya 62,000 vitachimbwa kwenye mashamba ya wakulima wadogo wadogo. Wote tunajua kilimo hakihitaji mvua, kilimo kinahitaji maji na maji ndio haya Waziri leo kupitia visima hivi tunakwenda kuondoa changamoto hii na wakulima watalima mwaka mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la BBT financing, kwenye hili kwa kweli tumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wakati anaingia alituahidi kwamba atahakikisha mikopo katika kilimo inapata riba ya single digit. Tunavyozungumza sasa benki ya kilimo na benki za kibiashara zinatoa mikopo kwa wakulima kwa asilimia tisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, Mheshimiwa Waziri na Wabunge wote hapa mtakuwa mashahidi, mkulima alikuwa hakopesheki katika benki za kibiashara, lakini kupitia programu mbalimbali zinazoendelea, mkulima sasa ameaminiwa na anakopesheka katika benki za kibiashara. Leo hii tunazungumzia programu kupitia AGITF kuna mikopo inatoka kwa vijana kwa 4.5%. Tunachotakiwa kufanya ni kuchangamkia fursa hizi, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametufungulia milango ya kuhakikisha vijana na wanawake wanawezeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye suala zima la BBT Ugani, wameanza katika mazao ya korosho na pamba ambako vijana kwa kushirikiana na Chuo cha SUA, vijana waliosoma elimu ya kilimo wanapelekwa kwenda kusaidia wakulima kwenye uzalishaji. Leo hii tunapozungumzia katika zao la pamba peke yake, vijana maafisa ugani zaidi ya 730 wamepelekwa katika mikoa inayolima pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, samahani dakika chache, nimpongeze sana Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba, kwa sababu vijana hawa kwa kazi waliyofanya kwa msimu mmoja haijawahi kutokea katika historia ya nchi hii. Wakulima wa pamba, mikoa inayolima pamba watatuambia hapa, ilikuwa ni kwa ekari moja hazizidi kilo 200 miaka yote, lakini kwa mwaka huu wakulima wamevuna kuanzia kilo 1,000, 1,500 na kuna wengine wanazungumzia kilo 2,000 kwa ekari moja ya pamba kupitia vijana hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo kwenye korosho tunategemea kwamba kupitia programu hii, vijana hawa waende katika...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako ulishaisha.
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazao yote ili tuweze kukuza uzalishaji, tunavyozungumzia suala la kulisha Afrika na kulisha dunia hiki ndicho tunachozungumzia. Mimi nishauri mambo machache, samahani kwa..... (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako ulishaisha, tuna wachangiaji wengi.
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja. (Makofi)