Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon Lucy John Sabu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii, lakini kiupekee kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya katika Wizara hii ya Kilimo, tunampongeza kwa dhati kabisa Waziri wa Kilimo - Mheshimiwa Hussein Bashe, Naibu Waziri - Mheshimiwa David Silinde na watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya katika Wizara hii. Mmedhihirisha kwamba wakulima wa nchi hii mmewatendea haki kweli kweli kwa namna ambavyo mmeweza kuwapa kipaumbele na tunajionea. Bajeti ilikuwa shilingi bilioni 294 na sasa tunaenda kwenye shilingi trilioni 1.2, ama kweli ongezeko la bajeti hili tuna imani linaenda kuwa na matokeo chanya kwa wakulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Simiyu ni mkoa kinara katika uzalishaji wa zao la pamba, tunashukuru Serikali kwa kuwekeza katika zao la pamba na kwa namna ya kipekee tunampongea Balozi Mwanri kwa namna ambavyo ameendelea kuhamasisha wakulima wa zao la pamba. Pia kiupekee ninampongeza Mkuu wa Mkoa - Mheshimiwa Kenani Kihongosi kwa usimamizi mzuri pamoja na Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Simon Simalenga, wameendelea kuwasimamia wakulima vizuri, na kwa kweli uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali ambapo tunaona pembejeo za pamba za kutosha pamoja na dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji huu wote unakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi bilioni 5.5. Kwa kweli wakulima wa Mkoa wa Simiyu wa zao la pamba tunaishukuru sana Serikali kwa kututhamini, lakini pia kwa kuwekeza katika zao la pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti tumeona Mheshimiwa Waziri kuna mpango wa ujenzi wa kiwanda cha vifaatiba. Kwa kweli kiwanda hiki kitakuwa na manufaa makubwa sana kwa wakulima wa pamba na itawapunguzia mzigo Serikali kuagiza vifaatiba nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nzuri iliyofanywa katika Wilaya ya Bariadi, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, tunaipongeza Serikali kwa kuleta matrekta 13 ambayo kama tulivyoambiwa Serikali imeweka bei elekezi ya shilingi 35,000 ambayo imewapunguzia gharama wakulima kuweza kulima katika mazingira ambayo hayatawapa vikwazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumepokea vijana wa BBT 15 katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ambapo vijana hawa wanafanya kazi nzuri sana ya kuelimisha wakulima na kutoa mafunzo. Tunaishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea viuadudu acre pack 145,000 tunaishukuru Serikali, mbegu tani 555, pump 1,500, ndege nyuki sita. Kwa kweli tunaishukuru sana Serikali kwa uwekezaji mkubwa huu ambao unaenda kuwanufaisha wakulima wa Wilaya ya Bariadi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Kwa mara ya kwanza Serikali imeruhusu mfumo huu wa wa stakabadhi ghalani katika Mkoa wa Simiyu na tunaishukuru ambapo wameanza na zao la choroko na msimu huu unaofuata tutaenda kwenye mazao ya mbaazi na dengu. Tunaiomba sasa Serikali kwa sababu kuna changamoto ya maghala, iweze kutuongezea ghala ambapo itaruhusu minada ya mazao mchanganyiko kuweza kuendelea katika Wilaya yetu ya Bariadi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Wizara ijenge ghala katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambapo ndipo tunao wakulima wengi, iweze kuwafikia na waweze kupata uhakika wa masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru Serikali kwa kuwekeza katika miradi ya umwagiliaji, pale Wilaya ya Bariadi tunao Mradi wa Kasoli ambapo mradi huu kwa kweli umekua ukisuasua sana na tunaomba Mheshimiwa Waziri aweze kutupia jicho, na ikiwezekana aweze kuufuatilia kwa karibu sana kuweza kuhakikisha kwamba, kwa sababu wananchi hawa wanausubiri sana mradi huu, na wanaamini kwamba utaenda kuwasaidia kuwa na uhakika wa kulima mwaka mzima bila changamoto ya aina yoyote. Tunaomba utusaidie Mheshimiwa Waziri utakapokuwa unahitimisha hoja yako basi uweze kutoa tamko ambalo litawasaidia kuweza kuona wananchi wa Bariadi katika mradi huu umetupia jicho la karibu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tunao mradi ambao uko katika Kata ya Mhango ambapo mradi huu ni mahsusi kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi, ni mradi wa umwagiliaji. Tunaomba pia utusaidie Mheshimiwa Waziri, muweze kuusukuma mradi huu na uweze kukamilika kwa wakati na wananchi waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee ninashukuru sana kwa namna ambavyo Serikali imeweza kuwatumia vijana wa BBT na katika Mkoa wa Simiyu kama nilivyosema, Halmashauri ya Mji wa Bariadi tunao vijana 15 ambao kwa namna ya kipekee wameonesha ushirikiano na sekta binafsi kupitia makampuni ya pamba kuweza kuwaajiri. Tunaomba muendelee kutuongezea vijana wengine ili kilimo kiendelee kuwa na tija zaidi na waweze kunufaika kupitia elimu ya mafunzo na kilimo cha kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwa kujenga visima virefu vya umwagiliaji katika Mkoa wa Simiyu na ninaomba Wizara iweze kutuongezea kujenga visima vingine katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambavyo vitawasaidia wakulima kuwa na uhakika wa maji ama kwa kuweza kulima kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa kumalizia ninaiomba Wizara katika mpango wa ununuzi wa magari, ikumbuke pia Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuweza kuiongezea gari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tunamhakikishia Mkoa wa Simiyu ana kura za kishindo ifikapo Oktoba, 2025. (Makofi)