Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru mno kwa kunipa nafasi kuchangia katika hoja hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kufika leo hii kwa sababu ni karibu kipindi cha miaka mitano, huu ndiyo mchango wangu wa mwisho katika Bajeti Kuu na katika Bunge hili la Kumi na Mbili tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana viongozi wa CCM katika Wilaya yangu ya Moshi Vijijini, Mkoa na Taifa kwa kuniteua kuwa Mbunge, ninawashukuru wananchi wa Moshi Vijijini, nimefanya makubwa sana kwa kushirikiana na Serikali, kwa hiyo, ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza sana Mawaziri wote wawili kwa kazi kubwa wanayoifanya pamoja na wasaidizi wenu. Kusema kweli mnyonge mnyongeni lakini mpeni haki yake. Sisi kule Kilimanjaro katika hiki kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumepata karibu trilioni 1.4, hii ni hela nyingi haijawahi kutokea. Kwenye Jimbo langu la Moshi Vijijini nimepata miradi mingi ya kuridhisha, bado haijatosha lakini inaridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo miradi ya shilingi bilioni 61, haba na haba hujaza kibaba. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake. Niendelee kumpongeza, kusema ukweli muundo wa bajeti unakwenda vizuri. Bajeti hii tunayoimalizia ilikuwa trilioni 50.29 na hii anayoomba tumpatie fedha sasa hivi ni trilioni 56.49, kuna ongezeko la shilingi trilioni 6.2 ambayo ni karibu 12.3 percent increment. Kwa hiyo, ninampongeza sana tunakwenda vizuri, hii ni bajeti ya kihistoria na tunaendelea kumwombea kwa Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kuna kitu ninataka niseme hapa ambapo watu wengi hatujakisema. Tunaona kwenye miaka hii mitano tumepata mafanikio makubwa sana, kama tusingekuwa na Waziri makini wa kukusanya na kusimamia fedha hivi vicheko ambavyo tunasema tumeupiga mwingi isingekaa ionekane. Ni kwa sababu Waziri na wasaidizi wake wanakusanya vizuri, wanasimamia vizuri, tumepata miradi mingi ya maendeleo katika majimbo yetu sisi Wabunge wote. Ni kutokana na usimamizi mzuri wa Waziri na wasaidizi wake. Kwa hiyo, tunampongeza sana kwa hilo. Kusema kweli mnyonge mnyongeni, lakini haki yake lazima tumpe maua yake mkwe wangu, tunampa hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Moshi Vijijini ninajua nina miradi mingi niendelee kumwomba Waziri vile vituo vya afya viwili ambavyo bado sijapokea fedha, ninaomba nipate fedha, ukamilishaji wa zile barabara ambazo wameshaanza kupeleka fedha kule, tunaomba tuendelee kuzikarabati, ili mambo yaendelee na watu wa Moshi Vijijini tuendelee kuipenda na kuiheshimu Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kuwaomba Watanzania kama alivyosema Mheshimiwa Kiswaga. Kama tunataka tupate maendeleo, tulipe kodi tuchangie kwenye maendeleo ya nchi yetu. Tusipolipa kodi kuna watu wanabeza, akiona kimeongezwa kitu kidogo anabeza wameongeza. Sasa wewe unataka huduma za afya, unataka huduma za elimu bure, maji, barabara zijengwe, nani unataka aje akusaidie kujenga barabara, vituo vya afya, kusomesha watoto wako kama siyo michango yetu sisi wenyewe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Watanzania tusiwe wazito kuchangia kwenye kulipa kodi ambazo zitatusaidia kuendesha Serikali yetu. Tusipofanya hivyo itakuwa ni kitu cha ajabu sana. Niseme sasa hivi tumeona wadau wetu wa maendeleo wengi sijui niseme wametuchoka ama kuna kitu hakiendi sawa, sasa wale wakijitoa na sisi tusipochangia tunataka nani aendeleze maendeleo ya nchi yetu? Kwa hiyo, niendelee kuwaomba Watanzania tujitoe tuchangie ili tuweze kuiendesha nchi yetu sisi wenyewe. Tutafarijika sana na tutajisikia vizuri kama maendeleo yetu tutayaleta sisi wenyewe kwa kutumia fedha zetu za nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu kwenye kulipa kodi wanakuwa wagumu maana yake hata kwenye Biblia ukiangalia Mathayo 22:17-22, watu walienda kumuuliza Yesu je, tumlipe Kaisari kodi? Sasa, ubishi wa kulipa kodi ulikuwepo tangu enzi hizo. Yesu akawaambia ya Kaisari mpeni Kaisari na ya Mungu mpeni Mungu. Kwa hiyo, Kaisari pale alikuwa ni mtawala na hapa niendelee kuwaomba Watanzania wenzangu kama tulivyoelekezwa kwenye vitabu vitakatifu, tulipe kodi tumpe Serikali vya kwake, Serikali ndiyo Kaisari wetu ili iendelee kujiendesha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Waziri kwa sababu kuanzia wakati wa lile janga la UVIKO tuliona uchumi haukufanya vizuri kidogo, ulishuka mpaka ukafika asilimia 2.2 na ukuaji wa uchumi kwa hii bajeti tunayomalizia umefikia asimilia 5.5 na bajeti anayopendekeza huenda ikapanda mpaka ikafikia asilimia sita. Hii ni hatua nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mfumuko wa bei umeteremka, sasa hivi upo kwenye digit moja ambapo ni 3.1 percent, tunampongeza sana kwa hilo tunaendelea kukuombea kwamba hiki ulichoomba ukisimamie vizuri ili uchumi ufikie pale asilimia sita na mfumuko wa bei uendelee kushuka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia pato la Taifa limekua ni kitu kikubwa sana na chenye heri. Pato la Taifa linatakiwa likue liende sambamba na uchumi wa kila mtu mmoja mmoja. Sasa hapa ndiyo nina matatizo na ninapenda niishauri Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mungu kwamba nchi yetu imeshaingia kwenye uchumi wa kati wa ngazi ya kwanza ambapo Pato la Mtanzania mmoja linakadiriwa kua dola 1,090. Ni jambo zuri lakini hebu tujiulize kiuhalisia wale wakulima wetu kule vijijini, wafugaji na wavuvi, Je, kuna mtu mwenye pato la uhalisia la dola 1,090? Mimi nitasema haya ni mahesabu ya kwenye makaratasi lakini kiuhalisia uchumi wa hawa watu kule vijijini haupo hivyo, upo duni na chini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu uchumi huu wa kitakwimu huwa wana-calculate ka kutumia GDP unagawa kwa idadi ya watu wote. Unachukulia kwa mfano uchumi wetu Wabunge mchango tunauotoa, akina Bakhresa, Mo Dewji, bodaboda wote wanaolipa, ukigawa kwa ile ndiyo unapata ile dola 1,090, lakini kiuhalisia kuna watu hawana hata dola 100 kwa mwaka, kuna watu huko vijijini hawana hata dola 500 kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekea kwamba inabidi kwenye hii bajeti na mpango ambao mmeupitisha tuweke juhudi zaidi kwenye kuwasaidia wale watu wa vijijni ili uchumi tukisema kweli kama ni dola 1,090 wawe na hizo fedha. Kule vijijini tuna baraka kubwa mno. Tuna mitaji mikubwa ya ardhi inayofaa kulima na kufuga, tuna mitaji mikubwa ya maeneo ya bahari, maziwa na mito mikubwa, hivyo tunavyo vyote na tunayo baraka ya kuzalisha mazao ambayo unaweza ukayauza nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kahawa, katani, tumbaku, pamba, mchele na mahindi yote haya ni mazao ambayo tukilima yana soko kule nje. Sasa ni kwa nini 65% ya watu wetu wapo kule na tuna hizi baraka za ardhi, mazao tunayoyalima, mifugo tunayoifuga na uvuvi, kwa nini hawa watu bado uchumi wao ni duni? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kwamba tutumie hii mitaji vizuri, mpango wetu huu kama walivyoahidi tuwekeze kweli kweli kwa hawa watu ili tuwakwamue kutokana na changamoto za umaskini. Ninaishauri Serikali yangu pendwa, wote huku ni watoto wa wakulima, wafugaji na wavuvi, wafanyabishara ni wachache sana humu ndani. Ninaishauri Serikali tuendelee kuwekeza kikamilifu kwenye sekta za uzalishaji, kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna ile Malabo Declaration na ile ya Maputo ambayo walipendekeza angalau 10% ya pato la Taifa ipelekwe kwenye hizi sekta za kilimo. Hili bado halijatekelezwa na hawa watu ndiyo wengi, tukitaka tuchomoke tupende tusipende tukiwekeza pale tutachomoka vizuri. Niendelee kumwomba Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla tuwekeze kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bajeti ukweli wamefanya vizuri wameshaiongeza kiasi fulani, ninaomba hebu twende kama Malabo walivyopendekeza, waone maajabu kwa sababu hakuna ambacho kimeshaharibika sasa hivi, fedha kidogo ambazo wamewezeka, ninasema kidogo bado tunaona matokeo, Mheshimiwa Bashe na Waziri wa Mifugo wanafanya vizuri mambo yanaonekana. Hebu tuongeze bajeti ya Wizara ya Kilimo na ya Mifugo tuone maajabu ambayo yatatokea kwenye nchi hii kwenye kutuletea maendeleo. Kwa hiyo, wazo langu tuendelee kuziunga hizi sekta tuwapatie fedha za kutosha ile Miradi ya BBT ambayo imeanzishwa kama vile BBT Mifugo, BBT Kilimo na Uvuvi ili isaidie wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua muda ni kidogo pia niipongeze Serikali imeanzisha Mfuko maalum wa Bima ya Afya ili watu wetu waanze kupata huduma kule, hili ni jambo jema. Nishauri pale walisema 70 kwenye HIV na 30 kwenye Mfuko wa Bima ya Afya, wengi wapo kwenye Mfuko wa Bima ya Afya watu wenye HIV ni kidogo zaidi. Kwa hiyo, ninapendekeza 70 ndiyo iende kwenye Mfuko na 30 irudi kwa watu wenye HIV. Katika hili ninaomba yale makundi maalum sasa, twende tukawasaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa kwa ruhusa yako, pia niipongeze Serikali kwa kuongeza pensheni kwa wazee wastaafu. Hongera sana, wameongeza kwa zaidi ya 150%. Lilikuwa ni jambo ambalo Wabunge wamepiga kelele huku na wamewasikiliza. Hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali, wale wazee ambao hawapo kwenye ajira rasmi za Kiserikali kama ilivyo kule Zanzibar, Rais wa Zanzibar anawapa wale wazee kitu kidogo cha kununua sukari; nao tujiongeze tuangalie namna ya kuwasaidia wazee ambao hawako kwenye sekta rasmi nao wapate pensheni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)