Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mimi nikushukuru wewe na pia nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais leo imetuchukua miaka 61 hatukuwa na Benki ya Ushirika, lakini kipindi cha Dkt. Samia Suluhu Hassan leo kazindua Benki ya Wana-Ushirika. Ni benki ya wakulima, ni benki ambayo ilikuwa ni ndoto za Mwalimu Nyerere, Mheshimiwa Rais amezitimiza na leo wakulima wanaenda kwenye dirisha lao la kuchukua fedha/mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tu, benki hii ya ushirika ambayo Mheshimiwa Rais ameizindua ambayo Mheshimiwa Rais ametimiza ndoto yake, tunaomba isambae nchini kote kwa wakulima wote. Ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, ndugu yangu Mheshimiwa Hussein Bashe na timu yako yote, pia nimpongeze sana Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege, ninawapongeza sana viongozi wote wa Vyama vya Ushirika nchini, Vyama Vikuu kwa umoja na mshikamano waliouonesha kuhakikisha kwamba benki hii inatimiza malengo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninawapongeza sana Warajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, wao walikuwa pia washauri wazuri wa vyama vyetu vya ushirika kwa ajili ya kupeleka hisa kwenye benki hii ambayo leo ina zaidi ya shilingi bilioni 55. Pia niendelee kukupongeza Mheshimiwa Waziri, umetengeneza kura za Mheshimiwa Rais kwa wakulima wote nchi hii kwa heshima kubwa, kwa kiwango ambacho ni cha kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nenda popote kwa wakulima wa chai wanamsifia Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakulima wa tumbaku wanamsifia Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakulima wa mpunga, mahindi, chai, kahawa na maeneo yote ambako wakulima wanalima nchi hii wote wanafurahia ruzuku ya pembejeo, wote wanafurahia ruzuku ambayo ilikuwa ni kama ndoto kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakumbuka Mheshimiwa Waziri tulipokuwa Mbeya wakati Mheshimiwa Rais anazindua, watu wengi hawakuamini, maneno mengi yamesemwa, lakini leo waliosema maneno ndiyo wanaotumia NPK ya shilingi 60,000, ndiyo wanaotumia CAN ya shilingi 60,000, ndiyo wanaotumia urea ya shilingi 70,000 na leo wameamini kwa macho. Nami niendelee kukutia moyo Mheshimiwa Waziri, chapa kazi, songa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kukuomba Mheshimiwa Waziri, benki yetu ya kilimo imefanya mema sana kwa wakulima. Kwa upande wa pamba pamoja na kahawa ni zaidi ya shilingi bilioni 132 zimeenda. Ni hawa ambao toka mwaka 2018 Mheshimiwa Waziri mwaka 2019, wewe mwenyewe ukiwa Naibu Waziri ulikuja Kahama kuungana na wananchi wa Kahama na wakulima wote na ukaanza wewe kwa sauti yako kupeleka fedha zaidi ya shilingi 4,500,000,000 kwa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) ambacho kilikuja kufanya kazi nzuri sana. Leo ni zaidi ya miaka saba kinaendelea kununua pamba kwa wakulima kwa ushindani mkubwa na leo kimepewa Kiwanda cha Wilimili, kimeyajenga, kinasimika pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kuipongeza Bodi ya KACU ikiongozwa na Mwenyekiti wake Ndugu yangu Emmanuel Nyambi Masanja pamoja na menejimenti yake. Wameonesha utulivu mkubwa wa kusimamia fedha za benki. Niendelee kupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Vyama vya Ushirika tukivisimamia vizuri, Vyama vya Ushirika na vile Vyama Vikuu tunaenda kuonesha mapinduzi makubwa sana kwenye ushirika. Tuendelee kuwatia moyo, tuendelee kuwashika mkono ili wasimamie mazao yetu kwa sababu ndiyo wanaosimamia wakulima wetu. Mheshimiwa Waziri mimi niendele kutoa ombi, umefanya vizuri sana kwenye mazao yote, umefanya vizuri sana kwenye tumbaku kama walivyoongea Wabunge wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukiangalia trend ya masoko inavyoenda na masoko yaliyoishia jana, wastani wa bei unaocheza ni dola 2.8. Pia wanunuzi wa tumbaku leo wakati Mheshimiwa Waziri Bashe ukiwa Naibu Waziri, wewe mwenyewe ulikuwa unatembea Ofisi za Wizara ya Fedha kwenda kuondoa kodi na kufuta tozo, kitu ambacho ilikuwa ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi cha Mheshimiwa Rais leo miaka minne, tozo zaidi ya 26 zote zimeondolewa kwenye tumbaku. Leo wastani wa bei ambao wakulima wanafurahia ni dola 2.8. L10F ambayo ilikuwa inauzwa dola mbili leo L10F ina dola 3.320. L1O ina dola 3.3, L1L ina dola 3, L20F ina dola tatu, madaraja yamebadilika wakulima wanafurahia sana. Hawa wakulima Mheshimiwa Waziri wanaenda kanisani, hawa wakulima wana ibada, wanakuombea sana wanamwombea sana Mheshimiwa Rais. Nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri, chapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu moja ambalo tunakuomba Mheshimiwa Waziri, tuondolee tozo ya mionzi. Tozo hii inawaumiza wanunuzi. 0.2 ya kila tumbaku inayouzwa kusafirishwa nje wanatozwa hawa wakulima thamani yake, ina maana wanunuzi wakisafirisha dola milioni mbili, asilimia mbili lazima watozwe. Wanunuzi wanachofanya Mheshimiwa Waziri, hawaendi kulipia fedha yao, wanachofanya kazi yao ni kumpunguzia bei mkulima na mimi ombi langu Mheshimiwa Waziri, export leavy hii dola 0.2 ikifutwa kwenye mionzi wanunuzi wanaenda kumpelekea bei mkulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaenda kutoka kwenye dola tatu tunaenda kwenda kwenye L10F ambayo ni tumbaku bora, tunaenda kwenye dola nne. Tutaenda kukimbizana na mataifa ya wenzetu Malawi na Zimbabwe ambao wenzetu wameenda kwenye dola nne mpaka dola tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kushauri kwa sababu tumepiga hatua, uzalishaji sasa umeongozeka, basi tuwe na mnada wa masoko ya tumbaku. Tuwe na mkataba, lakini pia tuwe na minada ili tupige hatua tuende kama mataifa wenzetu wanavyofurahia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wakulima wenye uwezo wa kufanya kwa mnada na wapo wakulima ambao hawana uwezo wataingia kwenye mikataba. Hili inawezekana likakuvusha sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri kuna zao ambalo tumelisahau sana, nalo ni zao la maembe. Maembe ningekuomba ingiza na lenyewe kwenye ushirika. Ongea na Vyama vya Ushirika hivi wafanye tathmini ya maembe ambayo yanavunwa kiholela kule kijijini, yavunwe kwa utaratibu mzuri kama ulivyofanya mazao mengine, yavunwe kwa utaratibu mzuri. Ni eneo ambalo yatachangia mapato makubwa kwenye Serikali zetu, halmashauri zetu zitapata fedha nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu leo mti mzima wa embe unauzwa shilingi 2,000, mtu anaokota maembe yote, tena kwa utaratibu wa kutikisa na yale machanga nayo yanapotea, lakini tukiwaingiza kwenye utaratibu mzuri, tukawapa dawa wakayapulizia vizuri, tutawapa utaratibu mzuri wa kuvuna yale maembe yetu. Tayari kwenye halmashauri zetu tutapata mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri niendelee kukuomba, tayari benki ya TADB inahudumia KACU, inahudumia MBCU, inahudumia, ACCU, inapeleka fedha SIMCO, ombi langu usimkatie tamaa SHIRECU na Nyanza.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Cherehani kwa mchango mzuri. (Makofi)

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)