Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja hii muhimu ambapo tunajadili Makadirio, Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/2026. Kwanza nianze kwa kumshukuru Rais kwa kuwateua hawa vijana wawili maarufu kama Singida boys, wamefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia hali ya uimara wa uchumi wetu kwa kipindi cha miaka hii miwili, kwa kweli uchumi umeendelea kukua, mfumuko wa bei umeendelea kuwa wa chini wastani wa asilimia tatu nukta moja ikiwa imepungua kutoka ile tatu nukta nane. Ni kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia, uchumi umekua kwa asilimia tano nukta tano na tuna makisio ya kukua uchumi kwa asilimia sita kwenye pato la Taifa, namaanisha hapo. Kwa hiyo, ni kazi nzuri ambayo kwa kweli imefanywa na hawa vijana pamoja na wasaidizi wao kwa maana ya Makatibu Wakuu na watendaji wengine, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeangalia mapendekezo mengi, hata katika mipango yao ambayo ameweka pale ni mizuri ambayo inaashiria kwamba huko tuendako ni kuzuri. Sasa nami nitapenda nitoe mchango wangu kidogo niongezee katika msisitizo kidogo katika yale ambayo wenzetu wamezungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika eneo la bajeti kujitegemea, wameonyesha mipango kwamba, kama nchi kuna sababu ya baadaye kuendelea kujitegemea. Kuweza kugharamia bajeti yetu wenyewe ni jambo zuri. Sasa maeneo muhimu ambayo nchi hii bado tumeendelea kulegalega na Watanzania wengi kweli sio waaminifu katika eneo hili la kodi, Watanzania wengi bado hawaoni umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili eneo ni muhimu sana kwamba kama Watanzania wenzetu pamoja nami hatutaki kulipa kodi kwa hiari, ni lazima tusimamiwe kwa nguvu na kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anajua umuhimu wa kulipa kodi kwa sababu ya kujiletea maendeleo yake mwenyewe. Katika jambo hili tutafanyaje? Tuendelee kwanza kutoa elimu, yaani elimu iwe ni jambo la kila siku. Kwa nini Mtanzania ulipe kodi? Kwa nini kuna sababu ya kujenga uchumi wako mwenyewe? Hilo muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmezungumzia suala la kuwajengea uwezo pia wakandarasi wetu wa ndani katika baadhi ya miradi fulani na shughuli fulani kufanywa na Watanzania. Jambo hilo ninawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kama tunatamani nchi hii Watanzania waweze kumiliki uchumi wao wenyewe ni lazima tuwe na mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba baadhi ya miradi yenye kiasi fulani cha fedha, hiyo iwe inatengwa tu kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuwe na mtaji kama nchi, mtaji fulani ambao tumeuweka tu kwa ajili ya kuwaendeleza Watanzania. Nilisoma mahali fulani inaonekana kwamba, nchi ya Oman ilipeleka vijana kwenda kusoma mambo ya mafuta na mambo ya gesi, baadaye walivyorudi wakafunguliwa makampuni, na Serikali ikaweka fedha zake kwenye hayo makampuni ili hao wa Oman waendelee kufanya shughuli za uchimbaji wa mafuta kwa kutumia makapuni yao. Nasi kama Watanzania, tunaweza tukawa na mpango kama huo kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilipenda kulizungumzia, Kiswahili chetu ni bidhaa muhimu sana ambayo sisi kama nchi tunaweza tukauza. Ukienda katika nchi mbalimbali, hata ukienda Marekani, Ulaya unakuta kwamba katika vyuo mbalimbali wanaofundisha Kiswahili hasa, ni wenzetu kutoka nchi ya jirani hasa Kenya, wakati tunasema Kiswahili kilizaliwa Tanzania. Kwa hiyo, nilikuwa napenda tuwe na mikakati ya kuzalisha rasilimali watu ambao tutakuwa tunaiuza nje kwa maana ya walimu kwenda kufundisha Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango mwingine ambao naona unafanywa na hata nchi kama Marekani, sisi kama tunataka kukiuza Kiswahili katika nchi ambazo tunafanyanazo biashara kwa mara nyingi zaidi, tuwe na mkakati wa kuweka udhamini wa kusomesha vijana kutoka katika nchi hizo ambazo tunazilenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta kwamba Marekani inachukua vijana kutoka Tanzania au Angola, inachukua, wana malengo, hee! Ya kukuza uchumi wao kwa kupitia hao ambao wanawasomesha na sisi tunaweza tukafanya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia nchi kama Sudan Kusini tunafanya nao biashara kubwa, tunaweza kila mwaka tukawa na mpango wa kusomesha vijana kadhaa na nchi nyingine, hiyo itatusaidia kukuza Kiswahili na kutengeneza mazingira ya kuwafikia kibiashara katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni kwenye upande wa ardhi, nimekuwa nikizungumza mara nyingi kwamba kwenye upande wa ardhi bado hatujafanya vya kutosha. Tanzania tunategemea kilimo kama ndiyo uti wa mgongo, lakini wawekezaji wengi wanapokuja nchini hawapati maeneo ya kuwekeza. Ndiyo maana ninashauri ni muhimu sana kuwa na benki ya ardhi, kuwa na akiba ya ardhi itasaidia sana wawekezaji wakubwa wanapokuja nchini kujua ukitaka kwenda Iringa tuna hekta 100,000 au kiasi fulani ni rahisi kwenda kufanya hivyo na tukileta wawekezaji wakubwa katika eneo la kilimo, kwanza ile kushirikisha teknolojia na hawa wenzetu wanaotoka nje, itasaidia Watanzania wengi kupata teknolojia na pia kupata masoko ya bidhaa zetu kule wanapotoka. Hilo ni jambo ambalo tunaweza kulifikiria namna ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nimeona katika mapendekezo ya bajeti, wamependekeza kufuta kanuni za usimamizi wa mazingira, Kanuni ya Mwaka 2024 kwenye GN 588. Jambo hili mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na Mazingira sijaliunga sana mkono, kwa sababu sasa hivi kama dunia tunahangaika kutafuta fedha za kuweza kusimamia mazingira. Tulitarajia kwamba hizi kanuni ziwawezeshe wenzetu wa Baraza la Kusimamia Mazingira wapate fedha ili kukagua shughuli za mazingira zinazofanywa kwenye migodi na maeneo mbalimbali ambayo yana uzalishaji, viwanda na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninatamani eneo hili badala ya kuzifuta tuone namna gani tunaweza kufanya marekebisho, kwa sababu tukisema tunafuta moja kwa moja maana yake tatasababisha tukose fedha za kwenda kusimamia mazingira, jambo hili ninaliona halijakaa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pia kwenye matumizi makubwa ya fedha. Kwa muda mrefu tumekuwa tukitekeleza miradi mikubwa mingi na ya kielelezo. Sasa, miradi mikubwa hii ya kielelezo ambayo tumekuwa tukiitekeleza SGR, kwenye umeme na mambo mengine, kwenye barabara na madaraja tumezalisha madeni makubwa ambayo sasa yanasababisha riba kuongezeka. Ninafikiri tunavyoendelea tuone ile miradi mikubwa ya kielelezo tuanze kuipunguza kwanza, tumalize ile ambayo tunaendelea nayo ili Taifa lisiendelee kuzalisha madeni ya ndani na ya nje, lakini haya madogo kwa sababu lazima mzunguko wa fedha uendelee kuwepo ile miradi midogomidogo tuendelee kuitekeleza. Kwa hiyo, wenzangu katika mipango yao wataangalia kwamba ile miradi mikubwa ambayo inatumia trilioni za fedha kwa sasa tuipunguze ili tutekeleze ile ambayo tayari inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani sana tuweze kuimarisha Benki yetu ya Maendeleo, tukiimarisha Benki ya Maeneleo na tukawa tunatoa mikopo ya muda mrefu kwa wakulima na kwa wafugaji, eneo hili kwa sababu tunasema kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu ni muhimu sana kuwa na mtaji mkubwa kwenye Benki ya Maendeleo, tuwe tunakopesha mikopo ya muda mrefu kwa wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mtanzania anaweza kuanzisha ranchi yake mwenyewe akafuga mifugo na akaweza kuuza tunakuza uchumi. Pia hata kwenye kilimo, kwamba sasa Serikali inatengeneza miradi ya umwagiliaji lakini tunaweza tukaruhusu Watanzania mmoja mmoja akaweza kukopa kwenye Benki yetu ya Maendeleo na bado akaweza kutengeneza irrigation scheme yeye mwenyewe na baadaye akaanza kuilipa Serikali ili mradi tu tuone awe ana uwezo wa kuweza kusimamia na tayari tumeona anatekeleza, kwa hiyo katika eneo hili nalo ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo litapelekea kuwa na ustahimilivu wa uchumi wetu ni hili suala la kununua dhahabu. Tunaipongeza Serikali kwa hatua ambayo tayari wameanza kuifanya ya kuwa na akiba ya dhahabu kwenye Benki Kuu. Jambo hili tunaomba liwekewe mkakati mkubwa kwamba kila mwaka tuwe na kiasi kikubwa cha dhahabu ambacho tunakinunua. Hiki kitatusaidia sana kuwa na uchumi himilivu na stahimilivu, jambo hili ninawapongeza lakini tuweze kuliongezea nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho sababu ninaona kengele pia imegonga, ninaishukuru sana Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa bajeti iliyotangulia kwa kweli Jimbo la Kalenga nalo limefaidika sana. Miradi mikubwa imetekelezeka katika miundombinu, kwa hiyo, tunawashukuru sana Serikali ikiongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuwashukuru sana wananchi wa Kalenga kwa kuniamini na kunileta katika jengo hili, ninawaambia kwamba, kazi waliyonituma nimewafanyia vizuri na ninaomba waendelee kuniamini kwa sababu yapo mengi mazuri yapo mbele ambayo tunakusudia kuwafanyia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)