Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia.
Awali ya yote na mimi ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha siku ya leo kuchangia katika Bunge letu Tukufu ambalo ndiyo tunaendea ukingoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kwenye nchi yetu nzima hususan kwenye Wizara hii ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wametangulia wamesema bajeti iliyokuwepo ya kilimo katika nchi hii, lakini leo tunaenda kwenye shilingi trilioni 1.2. Hili ni jambo kubwa na ni jambo la kihistoria na jambo hili haliwezi kusahaulika kabisa. Inaenda kuinua wakulima wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe, ninampongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo pamoja na Wakurugenzi wao wote wa taasisi hii ya Kilimo ambao wameweza kuweka historia ya Wizara ya Kilimo. Wizara hii zamani ilikuwa kama ni bench fulani, lakini leo wamefanya kazi kwa ushirikiano na kuiona Wizara ya Kilimo ilivyokwenda kuinua Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo wametimiza slogan yao ya kilimo ni biashara, walikuwa wanasema kilimo ni biashara lakini leo tumeona Watanzania wote wanakwenda kwenye kulima. Zamani ulikuwa ukilima unaonekana kama ni mtu maskini, hauna uwezo, lakini leo kila mtu anatamani kulima kwa kazi kubwa ilivyofanywa na Wizara ya Kilimo. Kwa kweli, tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijikite sasa kwenye kilimo chetu cha tumbaku. Toka tumepata uhuru hatujawahi kuona mabadiliko makubwa kwenye kilimo cha tumbaku kama kipindi hiki. Ninaipongeza sana Wizara ya Kilimo hasa Mheshimiwa Waziri na timu yake yote. Tulikuwa tunalima kilo 39,000 kabla Rais Samia hajaingia madarakani, sasa hivi mwaka jana tumepata kilo 122 na tunakwenda kwenye kilo 160,000. Hili ni jambo kubwa sana halijawahi kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala zima la bei, tulikuwa na dola 1.65 sasa hivi tunakwenda kwenye wastani wa dola 2.4 mpaka dola 2.8. Wakulima wameanza kuuza tumbaku yao na wanafanya sherehe kuona wanauza kwa bei kubwa ambayo hawajawahi kuitarajia. Nani kama Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan? (Makofi)
WABUNGE FULANI: Hakuna.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na kiwanda kimoja cha tumbaku tu cha Alliance One, tulikuwa na TLTC, lakini walivyojitoa Mheshimiwa Waziri amefanya jitihada za makusudi tumepata mwekezaji mzawa ambaye ni Mkwawa. Amejenga kiwanda kikubwa cha tumbaku, anachakata kilo 60,000 mpaka kilo 120,000. Hicho ni kitu kikubwa sana kwenye wakulima wa tumbaku, tunampongeza sana huyu mwekezaji Mkwawa kwa kazi nzuri anayoendelea kutufanyia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwekezaji Mkwawa amejenga kiwanda kikubwa cha tumbaku ambacho hakipo Afrika Mashariki nzima ambacho sasa tumbaku yetu itapata soko kubwa na itahitajika zaidi. Tunaendelea kupongeza Serikali kwa jitihada zao za kuinua zao hili la tumbaku. (Makofi)i
Mheshimiwa Naibu Spika, nisiwaache TFC, hii taasisi ilikuwa imekufa lakini Rais amefanya maamuzi magumu ameifufua, leo TFC imegawa mbolea kwa wakati, siyo tu kugawa mbolea kwa wakati pia imeshusha bei kutoka dola 72.45 mpaka dola 63. Tunampongeza sana kaka yetu Mshote na watumishi wake wote wa taasisi yake kwa kazi nzuri waliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatujawahi kupata ruzuku ya mbolea, ndiyo mara ya kwanza, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa ruzuku ya mbolea. Pia wale wote waliokuwa wanadai ruzuku za nyuma zimeanza sasa kulipwa, changamoto ni ndogo, wapo wanaolipwa mara mbili na wapo ambao hawajalipwa kabisa, kwa hiyo, ninaiomba Wizara izikague hizi changamoto na kuzimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mwizi wa fadhila nisipomsifia Mkurugenzi wa Benki ya Kilimo (TADB) kaka yetu Nyabundege kwa kazi nzuri aliyoifanya. Wakati wanaanza kufufua vyama hivi vya ushirika ambavyo kama vilikuwa vimekufa, ali-risk na kuvikumbatia vyama vya ushirika akatoa shilingi bilioni 36 kwa ajili ya kuvifufua vyama hivi vya ushirika na hatimaye leo ushirika unaendelea mpaka kufikia kufungua benki yao ya ushirika.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa muda wetu ni mfupi sana.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa nimesema kaa chini muda wetu ni mfupi sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika,....
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge sijakuruhusu.
Mheshimiwa Munde, endelea.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninampongeza sana Mkurugenzi wa TADB kwa kuvishikilia Vyama vya Ushirika, kuviinua na kuvikumbatia, ku-risk, leo hii mpaka wamefikia hatua ya kufungua benki yao. Ninaiomba Serikali, imefanya jambo zuri la kufungua Benki ya Ushirika, imetoa mtaji wa shilingi bilioni tano, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu, lakini wasiiache Benki ya Kilimo, waendelee kuiboresha iendelee kushirikiana na Benki ya Ushirika hatimaye wakulima waweze kufanikiwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, benki hii ya ushirika nimuombe Mheshimiwa Waziri iwe kimbilio la wakulima. Wakulima hawajawahi kuwa na kiinua mgongo. Niiombe Wizara ya Kilimo itoe elimu kwa wakulima, wanunue hisa nyingi kwenye benki yao ya ushirika, hatimaye waje wapate gawio iwe kiinua mgongo cha mkulima pale atakapozeeka atashindwa kulima, lakini awe na gawio lake linatoka kwenye Benki ya Ushirika.
Kwa hiyo, tuiombe benki hii ya ushirika iwe ndiyo kimbilio la wakulima na iwe ndiyo wanaweza kupata kiinua mgongo chao pale wakizeeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, taasisi zote Serikali, Wabunge tunapata kiinua mgongo, wakulima huwa hawapati kiinua mgongo. Benki hii ya Ushirika ije ifanye jambo hilo kwa wakulima wetu na kuendelea kuacha legacy ya Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa wakulima wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza sana NFRA, safari hii wakulima walilima sana hasa mazao ya mahindi na NFRA ilinunua mazao yote kwa bei nzuri na kuhakikisha wakulima wetu wanaendelea kunufaika. Hili ni jambo kubwa sana, tunampongeza sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan na tunasema kwa umoja wetu, Samia Suluhu Hassan anastahili kupita bila kupingwa hata Oktoba, acha ndani ya Chama Cha Mapinduzi tumempitisha bila kupingwa, lakini tunawaomba wapinzani ambao ni watani wetu wa jadi waache nafasi ya Urais, agombee Samia peke yake kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya nchi hii, anastahili kupewa hiyo heshima kwa kazi kubwa aliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie tu wenzetu wa upande wa pili, reforms zetu ziko vizuri, tunasubiri uchaguzi tuje tufanye uchaguzi wa kweli na haki. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshajiandaa, tuna reform nzuri na za kutosha. Kwa hiyo, wale wanaosema no reform sisi hatuelewi kwa sababu sisi tayari tuna reform nzuri na za uhakika. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili tayari Mheshimiwa Munde.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)