Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya KIlimo. Hotuba ambayo kwa kweli inatia matumaini makubwa ndani ya Taifa letu. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa kuthubutu na kusimamia haki na biashara za kilimo. Hongera sana Mheshimiwa na timu yako kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri ametaja mikakati yake katika hotuba yake, lakini amezungumzia Mkoa wetu wa Simiyu. Simiyu ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa pamba, ametaja kiwanda cha vifaatiba, lakini ametaja na kuwa na mpango mzuri wa kujenga kiwanda cha kuongeza thamani ya zao la pamba. Sisi Wana-Simiyu na wananchi wa Mkoa wa Simiyu tunakusubiria kwa hamu sana na tuko tayari kuupokea na kufanya kazi hiyo kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuwa kwa haya mazuri yote Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais alikuja Simiyu akielekeza kuwa na kiwanda cha vifaatiba na sasa hivi upele una mkunaji na mkunaji ni Mheshimiwa Rais na wewe msaidizi wake ambaye sasa umeonesha nia na matumaini makubwa. Tunaamini tutafanya kazi vizuri na tutawabadilisha Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana Mheshimiwa Bashe kwa mikakati mizuri hasa kwenye suala zima la vijana wa BBT. Nchi hii kuna Maafisa Ugani wapo vijijini, lakini wamezidiwa kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge wote tuliomo humu ndani tunatoka kwenye Mabaraza yetu tunajua changamoto zilizopo kwenye halmashauri zetu. Ushauri wangu maafisa vijana hawa wanaotokana na BBT tuwapeleke katika mazao yote ya kimkakati. Kila taasisi ambayo inashughulika tumbaku, korosho, kahawa, mazao yote ambayo umetuorodheshea zaidi ya tisa, tuwapeleke hawa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukishawapeleka hawa vijana, Serikali kupitia halmashauri na Serikali za mkoa waunganishe iwe chain moja ya kufanya kazi kwa sababu lengo ni moja, ili tusikinzane na D by D ambayo ni ya kisheria zaidi ili wewe Waziri ukitoa maelekezo yashuke mpaka huku chini, wasaidiane taasisi na taasisi binafsi ili kusukuma uzalishaji wa mazao haya ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia tu kwenye mfano wa tumbaku na mfano wa pamba, mwaka 2023 tulishuka uzalishaji mpaka tani 142. Mwaka jana tukavuka baada ya kuingiza mpango wa Mheshimiwa Bashe ambao aliuanzishia Dodoma, lakini akachukua mawazo yetu, ameshusha mpaka kule chini. Tunakupongeza kwa kuendelea kutusikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imetoka kwenye 140 tumekwenda kwenye 282. Mwaka huu tuna matarajio ya kupata 500 hili ni jambo ambalo linatia matumaini. Nini kifanyike?

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa ambao umewaleta kupitia BBT tuendelee kuwajali na kuwaajiri, tuwaingize kwenye mifumo kadri bajeti ya ajira inavyopatikana ili kutia moyo na kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, umenunua matrekta zaidi ya 500 na ya karibu 70% yamekuja katika mkoa wetu wa Simiyu. Matrekta haya yatafanya kazi vizuri yakirasimishwa kwenye vikundi ambavyo wakulima wako tayari kununua ili kusudi Serikali iendelee na jukumu lingine la kuendelea kuongeza matreka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, linguine ni kuwa matrekta haya kwa mazingira ambayo kule kijijini kwenye utaratibu ambao mmeshauanzisha kule Serikalini kwamba itoke control number ndiyo aende akalime, kwa hiyo kalenda yetu itakuwa inatupita, lakini ni mpango mzuri, mimi ninakuomba sana, ziko AMCOS ambazo ziko imara, ziuziwe yale matrekta, wakulima wale waendelee kulima, waendelee kushindana, hasa kule Usukumani tuna tabia ya kushindana. Nikiona trekta yangu na mwingine na mwingine mwaka unaofuata atanunua. Ndiyo kazi kubwa ya Serikali kuhakikisha kwamba mnawainua kiuchumi na kuweza kuongeza Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la pembejeo; pembejeo zetu zinapatikana katika kipindi cha awamu kama tatu/nne hivi, wakati mwingine inaathiri mazao yetu ya pamba na mazao mengine. Ninaomba kama ilivyo kwenye hotuba yake ameelezea kuwa na malori, magari ya kubebea na vitu vingine, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri, pembejeo hizi ziwe zinaingia nchini kuanzia mwezi wa sita na mwezi wa saba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima anapochukua mbegu aondoke na pembejeo yake, pale ndiko mtakapofahamu kwamba mkulima yupi anayelima na mkulima gani ambaye Halimi, lakini sasa hivi kwa ugawaji wa pembejeo zinakuja mpaka mwezi wa 12 ama mwezi wa kwanza, tayari watakuwa wameshamaliza hiyo kazi. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili ni muhimu uweze kutusaidia sana katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ilituelekeza kuimarisha ushirika na kazi hii imefanyika vizuri sana, ninakuomba Mheshimiwa Waziri na timu yako, hebu tuendelee wafanye kama inavyofanya KACU, wafanye kama inavyofanya SIMCU, wafanye kama inavyofanya ile ya Chato ili kusudi ushindani uwepo katika maeneo. Tuondokane na dhana ya kuwa na chombo ambacho chenyewe kinasubiria kuletewa vikamisheni vidogo vidogo ambavyo havina maana, waingie sokoni kama hawa watu wengine na italeta tija kubwa sana kwenye mfumo mzima wa soko huria ambao utakuwa umefanyika. Kwa hiyo, ninaendelea kushauri jambo hili ni muhimu likafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, Mheshimiwa Waziri, mazao yetu haya ambayo umebinafsisha kwenye COPRA tunakushukuru, tumeyaona kabisa mabadiliko yanavyokwenda, lakini elimu iendelee kutolewa katika maeneo yetu tunakotoka hususan kwa viongozi ngazi za wilaya na ngazi za kimkoa. Tunaamini Wizara mnakuwa na masikio mengi, mnashiriki katika makongamano mbalimbali ya kidunia, lakini waliopo kule chini hawajapata hii elimu, kwa hiyo, unapokuja na majukumu ya moja kwa moja, unakuwa ni ukinzani kati ya Serikali kwa Serikali, lakini kama watu wote mnaimba wimbo unaofanana, ninaamini kabisa COPRA na wengine watakuwa ni sehemu ya kutafuta masoko na kueneza jitihada nzima za Wizara yako ili kufanya kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi ninaungana na mchangiaji aliyemaliza Mheshimiwa Ditopile kwamba yote haya tunayafanya ni kwa sababu msimamizi wetu Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha mazao yote ya kimkakati na kilimo na ukizingatia 60% ya Watanzania ni wakulima na wafugaji, jambo hili Mheshimiwa Rais tunampongeza sana, lakini tunakupongeza wewe kwa uthubutu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maneno ni mengi, ninakuhakikishia Mheshimiwa Waziri na timu yako chapa kazi, maneno yatakuwepo na tutakusifu muda wote, tunaamini ukianzisha jambo wapo maadui wengine wasiotaka maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)