Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitangulie kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na afya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu hili kuweza kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikushukuru wewe binafsi kwa kunipatia fursa hii. Kipekee ninaomba niungane na wenzangu waliotangulia kuchangia kuunga mkono bajeti ya Wizara ya Kilimo kwani tumejionea sisi. Miaka minne ya uongozi shupavu wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, umewatendea haki wakulima wa nchi hii. Ongezeko la bajeti tangu bajeti yake ya kwanza mpaka leo ni kweli inaakisi mahitaji ya wana kilimo wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimesimama hapa unajua ndio tunaelekea ukingoni mwa Bunge hili la Kumi na Mbili. Siku siyo nyingi tutarudi kwa wananchi kwenda kuwaelezea ni nini tuliyoyaahidi mwaka 2020, yapi tumeweza kufanya na wapi tunaenda kuyaendeleza iwapo watatupatia tena ridhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Bunge hili siyo sana la kushauri shauri pamoja na kazi ya kupitisha bajeti, lakini tunatumia fursa hii kuelezea yale mema na makubwa yaliyofanywa na Serikali yetu wa Awamu ya Sita, lakini kwa ushauri, usimamizi na utekelezaji wa Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninao ujumbe kutoka kwa wakulima wa nchi hii na wanasema hivi; wanatambua Chama Cha Mapinduzi kimeshampitisha rasmi Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya Urais kwa uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba, 2025. Wanasema hivi; wao Tanzania hii wapo zaidi ya milioni nane na tena wamesajiliwa na wamejiandikisha kupiga kura. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo atoe mashaka kura zote za wakulima ndani ya nchi hii zitaenda kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wanasema nia wanayo, uwezo wanao na sababu za kwenda kumuunga mkono wanazo. Kwa uchache kutokana na ufinyu wa muda nitazielezea kwa uchache sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja utashi wake wa kisiasa kama kiongozi wa nchi yetu, lakini binafsi yeye mwenyewe Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mtu ambaye ameonesha imani kubwa kwenye kilimo kwa sababu anayo mapenzi ya dhati kwenye sekta yake ya kilimo. Kwanza yeye mwenyewe ni mkulima kwa vitendo, anayo mashamba hapa Dodoma na kule Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunasema hivi, tumegundua kumbe mume wa Rais wetu kipenzi Mzee Ameir Hafidhi kwa utaalamu wake ni mtaalam wa mambo ya kilimo. Ukiachilia mbali yeye mwenyewe ni kilimo. Kwa hiyo, sisi wakulima wa nchi hii pamoja na kumtambua Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Rais wetu kipenzi, lakini sisi tunamtambua kama shemeji yetu, wifi yetu na mkwe wetu. Kwa hiyo, ni sababu kubwa ya sisi kumuunga mkono itakapofika mwezi Oktoba, 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, imekuwa ni kilio cha wakulima tangu Uhuru wa nchi yetu tunasikitika, tunalia kwamba mbona Serikali haituungi mkono? Keki hii ya Taifa mbona haifiki kwetu? Kwa kweli utashi wake Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani tumeona namna anavyohangaika kuhakikisha keki ya Taifa hili inawagusa wakulima, inawafuta machozi na inaenda kuwainua. (Makofi)
Mheshimiwa Rais tunakushukuru sisi wakulima, leo siyo tu kwamba umesikia kilio chetu, lakini tukuhakikishie leo tunatabasamu na kucheka sisi wakulima. Leo hoja za wakulima zinajadiliwa na sekta binafsi, Serikali na kila mtu katika nchi hii. Ongezeko la bajeti limekuwa kubwa na hiyo ndio sababu kubwa ya sisi kumuunga mkono. Tukienda kupiga kura tunaenda kupiga kura kwa ajili ya ruzuku kwenye maeneo mbalimbali na mazao mbalimbali ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kuna ruzuku kwenye korosho zaidi ya shilingi bilioni 200. Leo kuna ruzuku kwenye pamba ambayo mkulima wa pamba kwenye msimu huu wa kilimo ameenda kulimiwa kwa ruzuku ekari moja kwa shilingi 35,000, huko nyuma alikuwa analimiwa kwa shilingi 70,000 mpaka shilingi 100,000. Nani kama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wakulima? Lakini hakuishia hapo, kapeleka ruzuku kwenye tumbaku zaidi ya shilingi bilioni 21, leo hii tunasimama kidete kusema Tanzania nchi ya pili Afrika kwa kuzalisha tumbaku. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda kupiga kura kwa ajili ya uimarishaji, tulifika hatua tukakata tamaa kwenye ushirika, lakini leo siyo tu kwamba ushirika umekuwa imara, leo hii tuna Benki ya Ushirika. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? Leo tukienda kupiga kura tunapiga kura kwa ajili ya mashamba makubwa ya pamoja ambayo yanaajiri vijana na akina mama. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilimo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kupiga kura tunapiga kura kwa ajili ya miradi mikubwa ya umwagiliaji, mabwawa pamoja na miundombinu. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilimo? (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii siyo ruzuku tu kwenye mbegu na kadhalika, ruzuku mpaka kwenye kununua mazao yetu. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? Tunashuhudia wenyewe tukipiga kura tunaenda kupiga kura kwa ajili ya kukua kwa kilimo chetu kutoka 2.7% mpaka 4.2%. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilimo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kupiga kura, tunaenda kupiga kura kwa sababu Dkt. Samia Suluhu Hassan ametujali wakulima wadogo ndani ya nchi hii na wakati anaingia madarakani kuna mkulima alikuwa anavuna magunia mawili tu, lakini leo kutokana na uwekezaji wake tunavuna zaidi ya gunia 30 kwa ekari moja. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, lakini nipende kumshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara yake na taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Kilimo hawajatusahau Dodoma, pia hawajatusahau Halmashauri ya Kondoa Mji kwa miradi mikubwa ya umwagiliaji ya BBT, pamoja na kutuchimbia visima kwa wakulima wadogo ndani ya Halmashauri ya Kondoa Mji, ahsante sana. (Makofi)