Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Katani Ahmadi Katani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tandahimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Allahu Tabāraka wa Ta‘ālā. Pia nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mkulima, kwa hiyo ninapochangia kilimo, ninachangia kitu ninachokifahamu sana kwa sababu ninaishi nacho. Transformation aliyoifanya Rais Samia kupitia Waziri Mheshimiwa Bashe, ninadhani ni ya kuigwa Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo matatu kwa sababu ninatoka kwenye korosho na nikukumbushe kwa sababu tulikuwa wote. Kuna wakati tuliua hapa export levy, tukaifuta, lakini kwa utashi wa Mheshimiwa Rais mwaka jana tumerejesha export levy yote na irudi kwenye korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kubwa lililofanywa na Mheshimiwa Rais kupitia Waziri Mheshimiwa Bashe ni suala la ruzuku ya pembejeo ya kilimo. Tangu ninazaliwa kwenye korosho hakukuwahi kupatikana ruzuku ya kilimo, lakini tangu Rais Dkt. Samia amechanguliwa wakulima wa korosho wa Taifa hili wanapata pembejeo bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la kifedha, kwa mara ya kwanza Rais Dkt. Samia tarehe 28 Aprili amezindua Benki ya Ushirika ambayo inakwenda kutoa mikopo kwa wakulima chini ya 10%. Haya ni mambo ambayo yanamchanganua Mheshimiwa Rais na dhamira yake ya dhati kwa wakulima wa Taifa hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwenye korosho kuanzia mwaka 2021/2022 Serikali ya Mama Dkt. Samia imetupatia fedha shilingi bilioni 59.4; mwaka 2022/2023 ikatupatia fedha shilingi bilioni 96.8; mwaka 2023/2024 ikatupatia shilingi bilioni 189 ya ruzuku ya pembejeo; na mwaka 2024/2025 tukapata shilingi bilioni 281. Hii ruzuku tunayoisema ni utashi wa Mheshimiwa Rais na akaamua kurejesha export levy ili fedha yake yote iende ikahudumie wakulima wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha; pamoja na jitihada za Mheshimiwa Rais anazozifaya kwa Taifa hili kwa wakulima, pamoja na jitihada za Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kuona wakulima wanapata pembejeo bure, leo fedha zimekusanywa na TRA zimeenda Hazina. Mpaka leo tunapozungumza zaidi ya shilingi bilioni 194 hawajarejeshewa Bodi ya Korosho kulipa wazabuni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mashaka kwa kazi kubwa inayofanywa na Waziri Mheshimiwa Bashe na tunakwenda kuvunja Bunge tarehe 27 Juni, Mungu si Athuman kwa kazi anazofanya anaweza akatolewa pale akapewa nafasi kubwa zaidi. Je, atakuja Waziri mwenye maono kama Waziri Mheshimiwa Bashe? Je, hawa wanaodai fedha, maana Waziri Mheshimiwa Bashe anakesha usiku na watu wa benki kuona namna gani wazabuni zote wa kilimo walikuwa hawakopesheki. Kwa utashi wa Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Bashe alikuwa anakutana na wa benki mpaka usiku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikitokea leo Mheshimiwa Bashe amepewa nafasi kubwa, hizi fedha atakuja Waziri mwenye maono ya wakulima? Hawa waliosambaza pembejeo kwa miaka minne hawajapewa fedha, watalipwa na nani? Niombe sana kama uwezekano wa fedha kukusanywa na TRA imekuwa ni shida, mlete sheria hapa fedha zikusanywe na Bodi ya Korosho yenyewe kwa sababu ndio inatoa export permit ya korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa ni rahisi sana anayekwenda kuchukua export permit analipa na export levy na fedha zitakwenda kutumika kwa ajili ya korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wazabuni wa pembejeo wengi wanadaiwa na benki, lakini tuna shilingi bilioni 194, hivyo kwa hesabu ya mwezi Machi ninaamini kwa korosho zilizosafirishwa mpaka sasa maana yake TRA kwa maana ya Hazina wamekusanya zaidi ya shilingi bilioni 200 ya korosho. Tunadaiwa na wazabuni zaidi ya shilingi bilioni 356. Wazabuni hawa ni Watanzania wenzetu, wameipatia Serikali pembejeo za zaidi ya shilingi bilioni 626. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana kwa hekima zako uone jambo hili ni namna gani Serikali inaweza kufanya intervention ili fedha zipelekwe Bodi ya Korosho, wazabuni walipwe pembejeo. Tunaposema leo tumezalisha tani 528,000 maana yake tangu tumepata uhuru wa Taifa hili hatujawahi kuzalisha korosho tani 528,000. Hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania kwa kutoa pembejeo bure. Kama wazabuni hawakupewa fedha, nani ataendelea kuleta pembejeo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wanaolima korosho sana na mikoa ya Pwani, Tanga tuna matumaini makubwa na kazi inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan. Sasa hizi fedha ambazo tumekubaliana na tumepitisha sheria hapa na zimeshakusanywa...
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Serikali na Mheshimiwa Rais, ninadhani wasaidizi wake wanasikia, aone namna ya kuingilia kati jambo hili ili fedha wapewe Bodi ya Korosho, wazabuni walipwe fedha na wakulima waendelee kupewa pembejeo bure kama dhamira ya Mheshimiwa Rais inavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija Mtwara kazi inayofanywa na Waziri Bashe, leo tuna kongani ya viwanda inajengwa pale Malanje. Katika fedha zinazokusanywa ni pamoja na hizo fedha ambazo zinakusanywa kwenye korosho. Niombe sana Mheshimiwa Rais kama Waziri Bashe haendi mbele umuache kwenye kilimo hapa awasaidie Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii mikakati mlioanza akija mtu mwingine isije sisi watu wa korosho tukaja tukalia tena hapa. Sisi tulishakombolewa, hatuna habari ya kulia tena hapa. Sisi hapa ni kupongeza na kusubiri bei bora ya korosho kama ilivyotokea mwaka jana, shilingi 4200 na zaidi, hii ni heshima kubwa kwa wakulima wa zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja. (Makofi)