Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Nitangulie kusema kwamba ninaunga mkono hoja na pia nitapiga kura ya “Ndiyo” siku ya Jumanne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchukua fursa hii adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa neema ya kuwa Wabunge katika Bunge la Kumi na Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo sasa linafikia mwisho wake. Sisi sote tumekuwa sehemu ya mageuzi, na mafanikio makubwa ambayo yametekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo tuna sababu ya kumshukuru Mungu kwamba tumepata nafasi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Taifa wa Maendeleo ambao umesomwa wiki iliyopita ni wa mwisho katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Miaka Mitano, lakini pia ni wa mwisho katika Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo ya Miaka 25. Ni kweli kwamba nchini kote utaona kwamba kuna mafanikio makubwa yaliyotokana na utekelezaji wa Dira yetu ya Miaka 25 na hasa katika nyanja za miundombinu, usafirishaji, kilimo, huduma za maji, afya pamoja na elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunapokwenda kutekeleza bajeti hii, lakini pia na kuandaa dira ya miaka mingine 25 nilitamani kutoka ofisi ya mipango ya Taifa izingatie jambo hili moja. Katika nchi yetu, kuna maeneo ya pembezoni na maeneo haya mara nyingi yako katika changamoto ya kijiografia. Kwa hiyo, ninapenda kusema kwamba ni disadvantaged areas.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninasema hivi? Siyo bahati mbaya kwamba Mkoa wa Kigoma ndiyo uliokuwa wa mwisho katika kuwasha grid ya Taifa. Ni kwa sababu uko pembezoni mwa nchi yetu. Mfano mwingine ni maeneo yaliyo katika visiwa, katika mpango huu ambao unakamilika, kwa mfano eneo la miundombinu, tulipanga kwamba tunapomaliza dira yetu ya miaka 25 tuwe tumefanikiwa kuunganisha barabara za lami zenye viwango mkoa hadi mkoa, na ni kweli kwamba tumefanya vizuri katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuchukulie maeneo ya visiwa, wilaya zilizo katikati ya mkoa hadi mkoa zitaweza kuunganishwa na barabara hiyo, na kwa hiyo, kupitiwa na barabara, lakini haitakuwa hivyo katika maeneo ya visiwa. Hivi ninavyoongea, katika Kisiwa cha Ukerewe kuna barabara ya lami yenye urefu wa kilometa saba tu, kwa sababu gani? Ni kisiwa hakiunganishwi na mkoa mwingine. Kwa hiyo, nilidhani kwamba tunapokuwa tunapanga maeneo ambayo yanajikuta yana changamoto ya kijiografia yanahitaji kuonekana tofauti kuliko inavyokuwa inapangwa ili na wao waweze kufanikiwa na kupata matunda ya mipango hii ya Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ndivyo ilivyo katika eneo la nishati na elimu pia. Kwa hiyo, nilidhani kwamba tunapokuwa tunapanga, basi tuangalie maeneo yaliyo pembezoni; na Wabunge wengi wanapokuwa wanaongea hapa, mara nyingi wanatoa mifano ya kwamba hata watumishi wanaopelekwa katika maeneo ya pembezoni ambayo ni disadvantage areas, mara nyingi watumishi wale watatoroka kwa sababu ya mazingira ambayo siyo rafiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapopanga kama Taifa, nisingetegemea kwamba Ukererwe ambayo ni kisiwa useme kwamba leo baada ya miaka yote hii ina kilometa saba za lami tu, hii siyo sawa. Kwa hiyo, tunapopanga, tuangalie ili watu wote waweze kufanikiwa, hata wale ambao wana changamoto ya kijiografia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, hilo linaelekezwa katika Ofisi ya Mipango ya Taifa. Tuiangalie Tanzania kwa ujumla wake, tuipange na kila mtu asipate hasara kwa sababu ama yuko kwenye kona fulani ya nchi au yuko katika kisiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunakwenda kutekeleza bajeti ya shilingi trilioni 56.49. Ninapenda kuiita kwamba ni bajeti ya mwendelezo ambayo inaakisi kaulimbiu ya Kazi Iendelee. Ni bajeti ya mwendelezo kwa sababu inakwenda kuendeleza miradi mikubwa ya SGR ili kuifikisha Kanda ya Ziwa pamoja na Mkoani Kigoma. Miundombinu ya usafirishaji inapokuwa ni bora, pia ni kigezo kikuu cha nchi ambayo inapiga hatua za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuombe kwamba miradi hii itekelezwe kwa wakati kama ilivyopangwa ili tuendelee kuepuka na kukomesha kabisa riba inayotokana na miradi kutotekelezwa kwa wakati. Inaendelea kula fedha zetu jambo ambalo siyo la msingi kwa sababu ya ucheleweshaji wowote ule ambao unaweza kutokea. Ni bajeti ya mwendelezo kwa sababu inakwenda kuendeleza kilimo na sekta nyingine za uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka niangazie kidogo kilimo na ni kwa sababu bajeti hii imeondoa VAT katika viuatilifu, na mbolea inayozalishwa ndani ili kuendelea kutoa tija katika eneo hilo la kilimo. Jambo ambalo ninatamani tulizingatie na ambalo limezungumzwa na wazungumzaji wawili waliotangulia ni kwamba tunatamani kuendelea kutumia utafiti katika kuleta tija katika kilimo. Kwa nini ninasema hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la utafiti sitaki kulizungumzia katika sekta ya kilimo peke yake, lazima tufanye utafiti katika utekelezaji wote wa shughuli za Serikali pamoja na elimu. Mfano sasa hivi tunasema kwamba tunanunua ndege ya mizigo ili tuweze kusafirisha mazao yetu ya kilimo, matunda na mboga katika nchi za nje, lakini bado katika nchi ya Tanzania ukichukua mti wa mwembe au mchungwa, mti huo huo unatoa matunda yaliyoiva, mengine machachu na mengine matamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua zabibu ukasema kwamba ni zabibu zilizoiva nyingine ni chachu, na nyingine ni tamu, sasa unavuna matunda ya jinsi hiyo umuuzie nani? Yaani mtu afike achukue matunda ambayo mengine ni makali na mengine yameiva, ni matamu katika mti huo huo? Hatuwezi kutoboa. Hatuwezi kuuza nje kwa mtindo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwaombe watu wa kilimo waendelee kuwatumia watafiti wetu ili tuweze kupata ile ladha uniform inayotoka katika mazao yetu hasa ya matunda pamoja na mboga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watafiti wasaidie katika hali hii lakini kama Serikali na kama alivyopendekeza Mheshimiwa Prof. Muhongo pamoja na mzungumzaji aliyetangulia kwamba hatuwezi tukaacha utafiti katika kupata tija katika utekelezaji wa shughuli zetu za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwenda kuteleza bajeti yetu na kuendelea kujenga uchumi wa nchi yetu, ninatamani sana jambo ambalo limependekezwa liweze kufanyiwa kazi kwa uaminifu mkubwa, na jambo hili ni la kuwafanya wazawa wa Tanzania waweze kuwa ndio wamiliki wakubwa wa uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haipendezi kwamba hivi tunavyoongea katika eneo la uchimbaji mdogo leseni ya PML imedhamiriwa kwa ajili ya wazawa lakini ukienda katika migodi ya wachimbaji wadogo kuna raia wa kigeni ambao ndio wanaoendesha shughuli hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwisho wa wakati huku tukitoa leseni ya PML kule madini kwamba ni ya wachimbaji wadogo, lakini uchimbaji wote unafanywa na wageni. Uchumi huo maana yake hautawaendea tena wazawa, badala yake utaenda kwa wageni. Hali ni hiyo katika biashara za uchuuzi Kariakoo pamoja na maeneo mengine ya sekta za uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kile ambacho tumekipendekeza hapa, tunaomba Wizara ya Kazi pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakae chini ili waone kwamba hawatoi vibali wala hawatoi ruhusa kwa shughuli ambazo zinapaswa kufanywa na wazawa, halafu zikafanywa na watu wa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuiombe sana Serikali yetu ikubali kwamba kilimo, uvuvi, ufugaji, na misitu, shughuli hizi kwa sehemu kubwa zifanywe na wazawa kwa sababu ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu. Kama kutahitajika wageni, wawe ni kwa ajili ya teknolojia, lakini sehemu kubwa ya shughuli hizi ziweze kufanywa na wazawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu uzoefu mkubwa ambao tumeupata katika utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati. Ningetamani kwamba iwe ni chachu ya kuandaa wataalamu ambao watakuja ku-take over baadaye, tusi-attach watu kwa ajili ya kupata mshahara. Tu-attach watu ambao tuna mkakati ndani ya nchi strategically kwamba hawa watu tumewa-attach katika miradi mikubwa, lengo letu likiwa ni kwamba wachukue uzoefu ambao baada ya hapo watakuja ku-take over katika utekelezaji wa miradi hii mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi tukaruhusu kwamba tunazalisha uchumi ambao tunasema kwamba sasa unakua lakini uchumi huo ukiangalia kampuni kubwa zinazotekeleza miradi nchi hii, ni kampuni za kigeni. Kwa hiyo, ni sawa na kwamba umezalisha fedha nyingi ndiyo, na uchumi wako umekua ndiyo, lakini ni nani? Who is the recipient of that economy? Utakuta ni kampuni kubwa za kigeni ambapo sasa unafanya kazi hapa, lakini wao ndio wanaofaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, kwa hoja hiyo hiyo ndiyo maana ninapendekeza kwamba katika utekelezaji wa bajeti hii na katika dira yetu tunayokwenda kuiandaa huko mbele, tukubali kwamba tuna sababu ya kuimarisha mashirika yetu ya umma ili yaweze ku-takeover. Kwa mfano, hapa tunataka kufanya LNG facility pale Lindi tukitumia Equinor ambayo ni Kampuni ya Mafuta ya Norway. Ni ya Taifa la Norway ile kampuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tungetamani hata hapa Tanzania tujenge mashirika makubwa ambayo nayo yatakwenda kufanya shughuli nyingi ambazo uchumi unaendelea kubaki hapa ndani. Kinyume na hapo, tutakuwa tunaweka bajeti, lakini mwisho wa siku wanaofaidika na uchumi mkubwa wa shughuli kubwa ni kampuni za nje na hivyo unakuta sisi tunaendelea kupata zile ambazo ni masalia na mabaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilidhani kwamba niyaseme hayo kwamba tuendelee kuyaimarisha mashirika yetu ya umma na hasa mashirika kama ya TPDC. Kwenye upande wa mafuta, yapewe nyenzo muhimu ya kuweza kufanya kazi hiyo. Shirika letu la Madini (STAMICO) tuendelee kulifanya liwe shirika ambalo litafanya kazi hiyo kwa ushindani mkubwa, badala ya kuacha kampuni za nje kuja kuchimba madini. Faida kubwa inayopatikana itarudi kule ambako ndiyo origin ya hiyo nchi, lakini kama ni TPDC, au STAMICO maana yake ni kwamba hela hiyo inabaki hapa ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)