Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika wa Bunge letu Tukufu awali ya yote ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata hii fursa ya kuchangia hii Wizara ya Kilimo ambayo ni Wizara nyeti sana kwa ustawi wa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Taifa letu la Tanzania, Afrika na Duniani kwa ujumla. Pia, nimpongeze yeye Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwa mgombea pekee wa Chama chetu Cha Mapinduzi. Tanzania inamwamini, Watanzania wanamwamini na wanamwamini kwa kazi nzuri ambazo anazifanya katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu na ni imani ya Watanzania wote kwa ujumla kwamba kama tunavyojua mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi. Kwa kuwa ni mwaka wa uchaguzi kutokana na kazi kubwa na ni nzuri ambayo ameifanya katika nyanja mbalimbali na hasa katika hii Wizara yetu ya kilimo, hatuna mashaka hata kidogo kwamba Watanzania watamchagua kwa kura nyingi na kwa kura za kihistoria kwa mabadiliko au kwa mapinduzi makubwa aliyoyafanya ndani ya Wizara yetu hii ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nimpongeze Dkt. Emmanuel Nchimbi; nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango; nimpongeze Rais Mwinyi wa Zanzibar; na nimpongeze msimamizi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Kassim Majaliwa Majaliwa; pamoja na Naibu Waziri Mkuu, Mhesimiwa Dkt. Doto Biteko bila kusahau Watendaji wa Wizara ambao wanaongozwa na Mheshimiwa Hussein Bashe. Mheshimiwa Hussein Bashe ni jemedari aliyeshika makali. Hatuna mashaka na ndugu huyu, Ndugu Hussein Bashe kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya katika hii Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ninaamini Hotuba hii ambayo leo Mheshimiwa Bashe ameitoa imesikilizwa na wWtanzania wote. Watanzania wameona kazi nzuri iliyofanyika katika hii Wizara, hongera sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa hii Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema imesikilizwa na Watanzania wote, Mheshimiwa Bashe haukuacha kipengele hata kimoja, umeeleza kwa mapana yake. Haya yote uliyoeleza ni kutokana na maagizo ambayo tarehe 22 Aprili, 2021 Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa ndani ya Bunge hili ametoa maelekezo jinsi gani ya kufanya, jinsi gani ya kuleta mapinduzi ya kilimo katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ameeleza hali ilivyokuwa mwaka 2021 wakati Mheshimiwa Rais anasema na baadhi ya mambo hayo ni mikopo midogo, uhaba wa maafisa ugani, ushiriki mdogo wa wanawake na vijana, mfumo dhaifu na mambo mengine yote Watanzania wameyasikia. Ulipokabidhiwa wewe Wizara hii, umeifanyia haki. Maeneo ya umwagiliaji yalikuwa ni machache, sasa hivi maeneo ya umwagiliaji yameongezeka. Ukitaka uwe na chakula cha uhakika ni lazima uongeze tija kwenye umwagiliaji. Maeneo ya umwagiliaji yameongezeka kwa kiasi kikubwa, hongera sana. Mama Samia umetizima ndoto zako kwa kufanya Tanzania iwe ni eneo la pekee katika Taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la ongezeko la chakula tulikuwa tunazalisha mahindi kidogo, leo hii kwenye chakula tunajitosheleza. Ukitaka uondokane na umaskini na suala zima la usalama wa chakula ni lazima uwe na uhakika wa chakula. Leo chakula tunazalisha kwa 100% na tunajitosheleza, hongera Mheshimiwa Waziri Bashe, hongera Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chakula ni jambo la msingi, kulikuwa na suala la chakula, kulikuwa na suala la mafuta hapa na ikifika wakati na hasa katika mwezi ule ambao sisi kama waislamu tunaamini ilikuwa ni changamoto, sukari hakuna. Leo hii hatuzungumzii tena, tunazungumzia changamoto kwa kiasi kidogo sana, hongera sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunataka tuzungumzie suala la mbegu. Kuhusiana na suala zima la mbegu sasa kama nchi, kama Taifa tunazalisha wenyewe mbegu zaidi ya 80%, asilimia iliyobaki ni kidogo tu ambayo tunaomba kutoka nje. Mbegu ndiyo kila kitu katika usalama mzima wa chakula, hongera sana kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuhusiana na suala la uzalishaji wa mbegu, lakini mbegu hizi ambazo tunazalisha kama tunavyosema tunazalisha wenyewe na nyingine zinatoka nje. Kuna suala zima la mbegu zetu za asili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbegu za asili ni kitu muhimu kwa nchi na ni kitu muhimu kwa Taifa lolote lile. Kila mtu lazima awe na kitu chake, wakoloni walipokuja kututawala walitugawa katika mataifa na walipotugawa katika mataifa walisema vitu vyote sisi havina maana, vitu vyote ni vya kishenzi. Sasa kutokana na hili hata kwenye suala la mbegu wametutengenezea mikakati tusiwe na vyetu. Kwa hiyo, leo tukiwa na mbegu zetu itatusaidia sana kuondokana na ule utumwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunisikiliza, ninaunga mkono hoja kwa 100%. Ninaipongeza sana Serikali, ninampongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan. Tunaingia kwenye uchaguzi, tunakuombea urudi tena, tunawaombea Wabunge wote warudi tena ili tuendelee kuchapa kazi kwa maendeleo ya Taifa letu la Tanzania. Ahsanteni sana. (Makofi)