Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026; na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia muda. Ninadhani mawazo yaliyotolewa na mwenzangu aliyetangulia ni mawazo muhimu kweli kweli. Hakuna Taifa ambalo litakwenda mbele bila kuwekeza kwenye sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nianze mchango wangu kwa kusema hivi, tunapiga kura Jumanne ya wiki ijayo, siyo ya kesho. Kwa niaba ya wakazi wa Jimbo la Musoma Vijijini nataka niwaeleze kuwa hii bajeti nitaipigia kura ya “Ndiyo” Jumanne. Hii ni kwa sababu miradi jimboni mwangu na Mkoa wa Mara inatekelezwa vizuri kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hii bajeti ikipitishwa na tukaanza kuitekeleza tarehe moja mwezi wa saba Musoma Vijijini tutakuwa tumebakiza vitongoji 50 kati ya vitongoji 374 kufungiwa umeme. Vilevile nilimwomba Mheshimiwa Rais alivyokuja Musoma Vijijini miradi miwili. Mradi wa barabara na mradi mkubwa wa umwagiliaji. Ninatoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais, miradi hiyo imepatikana na inatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu ni kwamba wale wataalamu wa TANROADS na Tume ya Umwagiliaji tumekubaliana kwamba mwezi wa Sita wanawakabidhi wakandarasi, na kweli naona wanafanya majadiliano. Kwa hiyo, mwezi wa Sita wakabidhi wakandarasi, na sisi Musoma Vijijini tunaunga mkono hii bajeti kwa nguvu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye mchango ambao ni mpana zaidi; mipango, uwekezaji na bajeti. Ndugu yangu aliyeanza kuongea tulikuwa hatujasemezana, kwa kuwa muda huwa ni mfupi, mimi ninaanza na mapendekezo mawili, na naomba yachukuliwe kwa uzito. Nimeanzia mwisho baadaye nitarudi huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo langu la kwanza ni kwamba tuwekeze zaidi kwenye elimu na taasisi za elimu na hasa sayansi teknolojia na innovation. Nimekuja na hesabu. Hizi hesabu siyo za kufikirika tu. Tutumie percent mbili hadi percent tatu ya GDP yetu tuwekeze kwenye elimu na taasisi zake zote, na uzito mwingi kwenye elimu ya sayansi. Hii ni kwa sababu sisi Tanzania tumefanya kazi kwa karibu sana na Norway, tumekwenda kujifunza mambo mengi Norway.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wanawekeza percent 6.6 ya GDP yao kwenye elimu na taasisi zake. Wapo Watanzania wengi tunapeleka watoto kusoma Uingereza na Marekani. Uingereza na Marekani wanawekeza 6.1% ya pato lao la Taifa (GDP) kwenye elimu na taasisi zake. Pendekezo la kwanza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la pili ninaweka tarakimu kwa ndugu yangu aliyeongea, kwamba, ni lazima tuwekeze kwenye ubunifu na utafiti. Dunia ya sasa hivi siyo Research and Development, vinakuwa vitatu; Research, Development na Innovation. Sasa nchi za kiafrika tulisema angalau asilimia moja, lakini ni South Africa tu walikuwa wamefikia 0.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napendekeza Tanzania tuwekeze angalau percent moja mpaka mbili ya GDP yetu kwenye mambo ya utafiti na ubunifu. Mfano mzuri ni hapa Samsung, anafanya vitu vyote hivi nchi ya South Korea wanawekeza percent 4.8 ya GDP yao kwenye utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu China sasa hivi hizi solar panel za dunia nzima, 90% ya solar panel, wacha vitu tunavyonunua Kariakoo, vinatoka China kwa sababu wanawekeza kwenye utafiti. Wao 2.7% ya GDP yao inawekwa kwenye utafiti. Kwa hiyo, hayo ndiyo mapendekezo ya kwanza mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye bajeti. Bajeti yetu imesomwa kwa wakati mmoja ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Maana yake ni kwamba, ni lazima ya kwetu kidogo tulinganishe na wenzetu wakati tunajadili ya kwetu. Hatuwezi kujijadili sisi wenyewe tu. Sasa ninaomba Waheshimiwa wanifuate taratibu hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kwa sababu bajeti ilikuwa na nchi za East Africa na mimi nitaweka kwa dola ili iwe rahisi kulinganishwa na nchi nyingine. Bajeti yetu hii tuliyosomewa ni ya dola bilioni 21.6, sasa hivi Watanzania tuko milioni 70.5 (70.5 million population). Kwa hiyo, expenditure, yaani matumizi ya bajeti tuliyosomewa kila Mtanzania ni dola 306, na pato letu (GDP per capital) sasa hivi ni dola 1,220.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kipimo kingine cha maendeleo ambacho hatukitumii sana, ninaomba Mawaziri Wawili muwe mnakiweka, msiwe mnakisahau. Ninajua mnacho, huwa mnakisahau, nacho ni hii HDI (Human Development Index). Hii GDP per capital ni ya World Bank na IMF, tunaipenda sana. Kuna ya UNDP ambayo ni nzuri zaidi, nayo inaitwa Human Development Index. Hii ni nzito kwa sababu inachukua mambo ya afya, mambo ya elimu na maisha yetu, yaani standard of living. Kwa hiyo, ukichukua hii HDI Tanzania sasa hivi ni 0.555, tuko katikati maximum ni one. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya bajeti yao shilingi bilioni 30.3, wako Wakenya milioni 57.5. Kwa hiyo, expenditure ya mtu mmoja kwenye bajeti ya Kenya ni dola 574, GDP per capital ya Kenya ni dola za Marekani 2,301. Sisi 1,220 wao 2,305 na HDI (Human Development Index) yao ni 0.628. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uganda wamesoma bajeti yao, ni shilingi bilioni 20.1. Population ya Uganda ni watu milioni 51.4. Kwa hiyo, expenditure ya bajeti yao kwa kila Mganda ni Dola za Marekani 391, GDP per capital yao ni dola 997 na HDI yao ni 0.582.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia na Rwanda. Bajeti yao ni shilingi bilioni 4.9. Warwanda wako milioni 14.6. Kwa hiyo, expenditure ya bajeti yao, kila Mrwanda atatumia dola 336 na GDP per capital yao ni dola 1,071 na HDI yao 0.548. Kwa hiyo, ukiangalia bajeti iliyosomwa kwa nchi za Afrika Mashariki, usichukue tu tarakimu, zigawanye na population, utaona kwamba Wakenya ndio wanaoongoza; kila mtu atatumia dola 574 na sisi kila mtu atatumia dola 306. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujilinganisha, nimechukua Seychelles na Mauritius, wao GDP per capital yao Seychelles ni dola 26,000; ni nchi inayohesabika kuwa imeendelea; na HDI yao ndiyo kubwa Afrika ni 0.848; Seychelles GDP per capital ya Mauritius ni zaidi ya dola 11 na HDI yao bado 0.8. Kwa hiyo, ukiangalia kwa maendeleo yetu sisi tuko katikati kwenye hivyo viwango vya HDI nchi za Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja sasa kwenye mambo ya uchumi. Uchumi wetu tangu mwaka 2000 mpaka sasa hivi 2025 kwa miaka 25 umekua kati ya asilimia tano mpaka saba. Mwaka mmoja tu 2011 uchumi ulifika 7.5%. Ndugu zangu, wataalamu wote wa uchumi duniani kote wanasema ukitaka kuondoa umaskini uchumi uende kwa asilimia nane, kumi na zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu reserve ya dhahabu ni muhimu sana. Ninashukuru na Mwenyekiti wa Kamati ameisoma ambayo hesabu yetu inayojulikana huko duniani, tuna reserve ya tani 3.7 ukilinganisha China kama wenzetu wana zaidi ya tani zaidi ya 2,200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, India wana zaidi ya tani 800. Kwa hiyo, hii dira ya maendeleo tunayoimaliza sasa, malengo yetu yalitaka GDP per capital iwe ni 3,000 US Dollars; ukichukua na population yetu ya watu 70 leo, hii GDP yetu inapaswa kuwa dola za Marekani bilioni karibu 210, lakini sasa hivi tuko kwenye bilioni 22. Tume-perform by 10% (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima hapo tuongeze kasi ya ukuaji wa uchumi. Umeme tumefanya vizuri. Makisio ilikuwa tufikie megawatts 5,000 ukichukua umeme wa kwenye grid na kwenye off grid, tuna megawatts 4,300. Performance yetu imekuwa ni 86% ya malengo. Kwa hiyo, tumefanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji na matumizi ya umeme ndiyo yanaonesha kwamba kweli Taifa lako ni kubwa. Mwaka 2024 umeme ambao ulizalishwa na China unazidi umeme wa Marekani, European Union na wa India ukiweka pamoja. Kwa hiyo, uone wengine wanakwendaje. Takwimu, ninaona muda hauniruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tufanyeje? Nije kwenye mapendekezo ambayo ni ya muhimu. Tufanyeje uchumi wetu ukue kwenda asilimia nane mpaka kumi? Sectors ambazo tunapaswa kuwekeza zaidi ambazo ni msingi (foundation) au tuseme primary sectors ni kilimo na uchimbaji wa madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sekta hizi na nimetoa mapendekezo mchango wa GDP, hapa lazima twende kwenye agriculture, ufugaji (animal husbandry), uvuvi huu wa vizimba, forestry tuvune misitu halafu twende kwenye uchimbaji. Kwa hiyo, hizi agriculture, animal husbandry, fisheries, forestry, and mining hizi ndizo ziwe uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi wetu, na ikifaa tuwekeze hapo, uchumi ukue zaidi, tupate mchango wa 55% (55% of our GDP) itoke huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uchimbaji hapa nitaongea na rafiki zangu; tumewekeza sana kwenye dhahabu, na ni kweli kwa sababu dhahabu imepanda bei, lakini kuna madini mengine ya muhimu sana. Kwa mfano, sasa hivi ounce moja ya dhahabu ni karibu dola 3,500, lakini kuna madini ambayo hatuyajui yanaitwa rhodium ambayo yako kwenye dola elfu tatu karibu na mia nane. Hii rhodium inaweza ikapatikana kwenye leseni tulizozitoa hizo. Sijui kama waliotoa leseni wanajua hayo madini yamo humo, sijui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza kingine kwenye pato letu la Taifa lazima twende kwenye huduma (services). Hiyo inakuwa ni secondary sector. Services hapa ninamaanisha utalii, biashara (finance) mambo ya benki, mambo ya afya, mambo ya elimu na water and electricity suppy. Hizi za huduma, hawa wachangie 30%, hizi services, 30% of our GDP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu ninamalizia, nimejipanga kuendana na muda wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa mwisho utatoka kwenye viwanda (industrial sector) yaani manufacturing na construction ituchangie 15% ya GDP yetu. Hivi nimevichukua baada ya kuangalia uchumi wa nchi mbili ambazo zimefanya vizuri ambazo ni China na India.

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka mwaka 2010 China imempita Marekani kwenye mambo ya manufacturing kwa mbali sana. Kwa hiyo, na sisi hizi sekta nimezi-check kwenye nchi zote zilizofanya vizuri, sectors ni hizi na huo ndiyo utakuwa mchango wa GDP; na soko lipo kwa sababu dira yetu ya maendeleo inatupeleka mpaka 2050. Tukifika mwaka 2050 kuna soko duniani, tutakuwa watu bilioni 10 na soko la Afrika lipo, tutakuwa watu zaidi ya bilioni 2.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pendekezo langu ni hilo, uchumi ukue kwa zaidi ya asilimia nane na hizi sekta tatu: primary sectors, secondary sectors na hizi tertiary sectors ndiko tuwekeze na tutaweza kupunguza umaskini kwa kasi kubwa, ahsante sana. (Makofi)