Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa fursa hii adhimu ya kutoa mchango wangu katika Bajeti Kuu ya Serikali. Kampuni ya utengenezaji wa simu maarufu ya Samsung ya Korea Kusini ina kauli mbiu yake muhimu sana inayosema; “We have a shortage of natural resources, but creativity in abundance.” Hatuna rasilimali za kutosha, lakini tuna ubunifu wa hali ya juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii inasadifu maneno aliyowahi kuyasema Mheshimiwa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Hayati Edward Lowassa. Alisema akipewa nafasi ya kutaja vipaumbele vikuu vitatu vya mipango ya maendeleo ya Taifa, basi angetaja kipaumbele cha kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoitafsiri kauli hii utabaini kwamba elimu inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza na sekta kiongozi katika mipango ya maendeleo ya Taifa letu. Hata hivyo, ninatambua kuwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuwa na Mawazo tofauti. Wengine watasema kipaumbele cha kwanza ni kilimo, wengine maji, wengine miundombinu, wengine afya, wengine umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi ambalo tunapaswa kujiuliza kama viongozi, je, miradi hiyo mikubwa itatekelezwa na nani? Kama itatekelezwa na wakandarasi kutoka nje, basi jambo hili halina afya kwa maendeleo ya Taifa letu, kwa sababu tutakuwa tunahamisha fedha za Taifa letu kuzipeleka nje. Hapa ndipo ile hoja ya kuwekeza katika sekta ya elimu hasa sayansi na teknolojia pamoja na utafiti inapokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapotafakari kwa makini, mipango yetu ya maendeleo na bajeti, ninaona kiwango cha fedha kinachowekezwa katika sekta ya elimu, hasa sayansi na teknolojia, utafiti na uvumbuzi hakilingani na dhamira ya Taifa letu ya kujenga uchumi ulio shindani. Huwezi kujenga uchumi ulio shindani kama hujawaandaa vizuri rasilimali watu ukawapa maarifa na ujuzi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina Chuo cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia, chuo ambacho kimeanzishwa kwa madhumuni ya kutoa shahada za juu za teknolojia ya habari, sayansi ya tiba na kilimo. Chuo hiki kwa bahati mbaya sana hakina maabara za kisasa ambazo zinaweza kufanya ugunduzi, uvumbuzi na utafiti wa kiwango cha Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu, iwapo tutawekeza kwenye chuo hiki, chuo hiki kinashika hatma ya Taifa letu. Kwa nini ninasema hivyo? Ni kwa sababu chuo hiki kinatoa mafunzo ya akili bandia pamoja na data science, taaluma ambazo ni muhimu sana katika mapinduzi manne ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana shaka sote tunakubaliana kwamba katika karne ya 21 sayansi ya data itakuwa ndiyo mgodi wa karne hii. Soko la matumizi ya data duniani yanaongezeka na soko lake ni kubwa sana. Nitatoa mfano hapa; China kuna watu bilioni 1.4, India kuna watu bilioni 1.4 na Afrika kuna watu wapatao bilioni 1.2; jumla yake ni bilioni nne. Hili ni soko kubwa sana ambalo linahitaji matumizi makubwa ya data hasa katika sekta za biashara, kilimo, afya na elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakubaliana nami kwamba nchi zilizopiga hatua ya maendeleo ya kiuchumi zimewekeza kiasi kikubwa sana cha fedha katika utafiti wa kisayansi na masuala ya sayansi na teknolojia kwa ujumla wake. Nitatoa mifano ya nchi tatu hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya kwanza ni India. Mwaka 1966 Waziri Mkuu wa wakati ule Jawaharlal Nehru aliamua kuwekeza katika vyuo vya teknolojia pamoja na vyuo vya sayansi ya tiba. Leo ninapozungumza, nchi ya India ni moto wa kuotea mbali katika teknolojia ya habari na matibabu. Watu wanatoka sehemu mbalimbali za dunia kwenda India kutafuta matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili; China wakati wa uongozi wa Deng Xiaoping waliwapeleka vijana wao Marekani wapatao 100,000, mwaka 1978 ili kujifunza masuala ya sayansi pamoja na teknolojia ya kisasa. Leo tunajua sote Taifa la China lilipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa tatu ni Vietnam. Nchi hii mwaka 1980 ilikuwa maskini wa kutupwa, na pato la Taifa la Vietnam wakati ule lilikuwa ni dola bilioni 18. Leo baada ya kufanya mapinduzi ya sayansi na teknolojia, pato la Taifa la Vietnam ni bilioni za Kimarekani 476 wakati Tanzania sisi pato la Taifa ni takribani kama bilioni 90 hivi. Tunaweza kujua kwa kiasi gani wenzetu wa Vietnam wameweza kupiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niseme mambo mawili kwa msisitizo mkubwa. Kwanza, ninatambua sana kwamba nchi yetu ni maskini, hauwezi kukidhi mahitaji yote ya sekta ya elimu. Hata hivyo, ukombozi wa uchumi ni kama vita, na vita hivi vinahitaji silaha, na silaha ya ukombozi wa uchumi ni sayansi na teknolojia pamoja na utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili. Mzee wetu Nelson Mandela aliwahi kusema kwamba elimu ndiyo silaha madhubuti tunayoweza kuitumia kuubadili ulimwengu. Kama Taifa langu la Tanzania linataka kubadili maisha ya Watanzania, kubadili maisha ya Waafrika na kuubadili ulimwengu, basi jambo pekee la kuwekeza kwa msisitizo mkubwa ni sekta ya elimu hasa katika masuala ya sayansi na teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme jambo moja. Wako wataalamu wa masuala ya elimu wanaosema kwamba katika karne hii ya 21 vita havitapiganwa tena kwa kutumia mizinga, bali vita vitatumiwa kwa cyber na masuala ya teknolojia ya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ninafikiri Tanzania, kama nilivyosema, tunayo nafasi hiyo ya kupambana kwa kutumia akili badala ya kutumia mizinga kwa sababu hatuna nguvu hizo; lakini akili Mwenyezi Mungu katupa. Tufanye hima basi kuziendeleza kwa maslahi ya nchi yetu na kwa maslahi ya Afrika. Ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)