Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkoani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninaomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana katika hili Bunge letu Tukufu la Bajeti ili kukamilisha kazi tuliyoanza leo asubuhi ambapo niliwasilisha hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kuanza kumshukuru Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe na Wenyeviti wote wa Bunge kwa jinsi mlivyoongoza na kusimamia majadiliano haya, hii ni pamoja na hoja nyingine zilizotangulia. Aidha, nichukue fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa wazi na kutoa michango yao ya kina wakati wa majadiliano haya yaliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninathibitisha kwamba michango ya Waheshimiwa Wabunge yote tumeichukua kwa uzito mkubwa na tunakwenda kuifanyia kazi ili iendelee kuleta ufanisi kwenye sekta ya uchukuzi pamoja na sekta ya usafiri na usafirishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia kipekee nimshukuru Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Sulemani Moshi Kakoso na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa maoni yao mazuri waliyoyatoa pamoja na michango yao. Ninakiri kwamba hoja hizo na maoni yao ni muhimu sana kwa maendeleo na ukuaji wa miundombinu, huduma za usafiri na usafirishaji hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutumia fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika bajeti hii. Waheshimiwa Wabunge 15 wamechangia wakati wa majadiliano ya hoja hii, ambapo Waheshimiwa 14 wamechangia kwa kuaongea na Mheshimiwa mmoja amechangia kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda mchache uliopita Mheshimiwa Naibu Waziri amemalizia kuchangia na kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa ufasaha na weledi mkubwa. Ninakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo umejibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge na mimi nitajikita zaidi kuzungumzia hoja zilizosalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nianze kuhitimisha hoja yangu kwa kutoa ufafanuzi wa kiujumla kwa maoni ya Kamati ya Miundombinu na baadhi ya maoni ya Waheshimiwa Wabunge. Tunafahamu kwamba sekta ya uchukuzi ni muhimu sana, katika mwaka wa fedha 2024/2025, sekta ya uchukuzi iliendelea kutoa mchango chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Mchango huo umewezesha kuendelea kukua kwa sekta nyingine za uzalishaji kama vile sekta ya kilimo, madini, utalii, viwanda na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2023 sekta hii ilikua kwa 4.1% na kuchangia takribani Pato la Taifa 7.2%. Aidha, kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2024 – Machi, 2025, sekta ya uchukuzi ilichangia mauzo ya kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 2.48 ya fedha za kigeni, sawa na ongezeko la 8.30%, ikilinganishwa na dola za Kimarekani bilioni 2.29 zilizopatikana katika mauzo ya kipindi kama hicho mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nijikite kwenye maoni ya Kamati yetu ya Kudumu ya Miundombinu. Kwanza, tumekubali kwamba tumeyachukua na tunaenda kuyafanyia kazi, ni maoni mazuri. Pia, kuna maoni machache ambayo ninatamani niyazungumzie kwa ufupi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza kuhusu kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege. Kamati yetu imetoa maoni ya kukamilisha zoezi la upatikanaji wa hati. Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeendelea na jitihada za upangaji, upimaji na ukamislishaji wa maeneo katika maeneo ya viwanja vya ndege nchini, ambapo hadi hivi sasa imefanikiwa kupata jumla ya hati ya vya ndege 35. Aidha, zoezi la upimaji na upangaji wa viwanja vya ndege Nane vya Tabora, Dodoma, Manyoni, Kondoa, Ngara, Mwanza, Mafia, na Masasi lipo katika hatua ya mwisho ambapo hatimiliki za viwanja hivyo zinatarajiwa kupatikana kabla ya mwisho wa huu Mwaka wa Fedha 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni ya pili ilikuwa ni kuboresha miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha KIA. Katika kuhakikisha kwamba miundombinu ya Kiwanja cha Ndega cha KIA inaboreshwa ili kuendana na ubora wa kimataifa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika kiwanja cha ndege hicho. Kwanza, mradi ambao tunaendelea kuujenga ni ukarabati mkubwa wa njia ya kurukia na kutua ndege ili iendane na ndege kubwa zinazokuja sasa hivi. Kazi ya pili inayofanyika ni; ujenzi wa Jengo Wageni Mashuhuri (VIP na CIP). Mradi wa tatu utakofanyika hapo ni ujenzi wa jengo la kuhifadhia mizigo pamoja na ukarabati mpya wa jengo la abiria ili kuendana na hali halisi ilivyo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha yote haya kwenye bajeti ya mwaka huu tumetenga takribani shilingi bilioni 35. Tunaamini kazi ya kuwapata wakandarasi itaanza hivi karibuni na baada ya hapo kazi ya ujenzi itaendelea. Maoni ya tatu yaliyotolewa na Kamati yetu ni kuhusu uendeshaji wa shughuli za reli kwa kushirikana na sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu umeonesha hasa tukichukua bandari kwamba, sekta binafsi ndiyo inakuwa ni engine ya maendeleo ya nchi. Leo hapa Wabunge wote wamesema na kuzungumzia juu ya maendeleo na faida iliyopatikana kwa uwekezaji wa sekta binafsi katika bandari ya Dar es Salaam. Kwa hiyo, ninaomba niwahakikishie Kamati yetu kwanza na Waheshimiwa Wabunge kwamba, kwenye upande wa SGR tunakwenda kushirikisha sekta binafsi. (Makofi
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Sheria ya Open Access tulishapitisha hapa Bungeni na sisi Wizara tayari tumeshatayarisha Kanuni za Open Access kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Tayari wapo Kampuni za Watanzania mbalimbali ambao wameonesha nia ya kufanya kazi ya uendeshaji wa SGR ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma hasa kwenye eneo la mizigo, kwa sababu biashara kubwa sana ipo kwenye mizigo. Kama nilivyosema kwenye hotuba yangu kwamba itakapofika Mwezi Juni, kazi hiyo ya usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini Dar es Salaam – Dodoma itaanza rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni ya Kamati pamoja ya baadhi wa Wabunge wamezungumzia kuhusu Reli ya Kusini. Reli ya Kusini ni muhimu sana kwa sababu kule kuna madini mengi na ninaamini tukijenga reli hiyo itafungua sana uchumi wa nchi yetu hasa kwenye sehemu ya upande wa kusini. Jambo hili tunalifahamiu na tumeshalifanyia kazi, tumeshafanya feasibility study. Hivi ninavyozungumza Serikali ipo katika hatua ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa hiyo Reli ya Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Wabunge wengi waliochangia kuhusu SGR. SGR kwa sasa kutoka Dar es Salaam – Dodoma imebadilisha maisha ya watanzania. Zamani watanzania walikuwa wanatumia saa Tisa Dar es Salaam – Dodoma, leo wanatumia saa tatu. Hii ni rekodi mpya ninafikiri kwenye Nchi za Afrika ukiondoa Morocco kwa sababu wana high speed train, lakini nchi zote nyingine hizi speed ya treni ya Tanzania ipo juu sana. Watanzania wote wanafurahia, sisi sote Wabunge karibu kila siku hapa tunapanda SGR kutoka Dar es Salaam – Dodoma na Dodoma – Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua faida hizo, Serikali inaendelea kujenga kwa kasi vipande vilivyobakia, hasa kipande cha kutoka Makutopora – Tabora ambayo sasa hivi ipo 14.53%; kipande cha nne cha kutoka Tabora – Isaka ambacho kipo 6.5%; na kipande cha tano kutoka Mwanza – Isaka ambacho kipo 63.16%. Vilevile, kipande cha Tabora – Kigoma ambacho kipo 7.88%. Serikali inaenda kujenga na kwenye bajeti hii wote ni mashahidi. Serikali imetenga takribani Shilingi trilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa vipande hivyo. Tunaamini kila Wakandarasi watakavyomaliza kufanya kazi yao, wakileta certificate tutalipa kwa wakati ili kuhakikisha kwamba mradi huo unamalizika kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye hotuba yangu kwamba Mwezi wa Juni tutaanza kazi ya usafirishaji mizigo kutoka Dar es Salaam – Dodoma. Tumejipanga vizuri, mabehewa yapo na tunaamini tukifanya hivyo tutapunguza sana ule msongamano kwenye Bandari pamoja na Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi katika miundombinu. Ushirikishwaji wa sekta binafsi ndiyo njia pekee ambayo itatutoa hapo tulipo. Kwenye bandari tumefanya na tumeona mafanikio makubwa. Kama nilivyosema kwenye TRC tunakwenda kufanya hivyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nigusie haraka Mheshimiwa Mnzava alikuja na hoja barabara ya Tanga – Handeni – Kibirashi – Chemba. Barabara hii ni muhimu, Bandari ya Tanga sasa hivi imeunganishwa na barabara mbili, Barabara ya Chalinze na Arusha. Ukitumia barabara kutoka Tanga – Handeni – Kibirashi – Chemba hasa kwa mizigo inayokwenda DRC, Zambia, Burundi na maeneo mengine, unapunguza takribani kilomita 100 ukilinagnisha na barabara ya Chalinze. Kwa vile barabara hii kama Mheshimiwa Rais alivyotuelekeza tunaenda kuijenga kwa PPP, ushirikiano kati ya TPA na TANROADS. Tayari tumeanza vikao kwa ajili ya kuona jinsi gani tutaanza kuijenga lakini barabara hii ni muhimu. Tunaamini tukijenga barabara hii itajiendesha yenyewe kwa sababu mzigo upo na ni barabara ambayo italeta faida kubwa kwa watumiaji wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mnzava vilevile amezungumzia kuhusu Bandari za Trans-shipment ni kweli na sisi kwa kulitambua hilo, tumeanza Bandari ya Bagamoyo na tunaenda bandari zingine kuhakikisha kwamba, tunazijenga bandari kubwa kwa ajili tu ya mizigo ya trans-shipment kutoka eneo moja kupeleka lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Kiwanja cha Ndege cha Lindi tumeshapata Mkandarasi na gharama yake ni takribani bilioni 120. Sasa hivi tunatafuta fedha kwa ajili ya kulipa advance payment ili kazi hiyo iweze kufanyika mara moja. Kuna hoja ya viwanja vya ndege vya Mkoa wa Simiyu, Njombe, Singida na Manyara, hivi vilevile tumetenga kwenye bajeti. Ukienda kwenye kitabu chetu utakuta tumetenga bilioni 22 kwa ajili ya kazi hiyo ili kuhakikisha kwamba na viwanja vya ndege vyote vya Mikoa ya Tanzania vinajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Mwantumu kuchelewa kwa safari ya ndege ya Air Tanzania, tumelichukua na tunaenda kulifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba sasa delays zilizokuwepo hizi zimepungua. Kwa ufupi delays hasa kwa ndege kubwa zimepungua bado tuna changamoto kidogo kwa delay kwenye Q400 kunapokuwa na matatizo, lakini tumelichukua hili na tunaenda kulifanyia kazi kuhakikisha kwamba sasa delays zote zinamalizika kwa asilimia kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kilumbe yupo hapa, Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza MV Mwongozo tayari ameshapatikana Mkandarasi na kwenye bajeti ya mradi huo ni bilioni 9.1 na kwenye bajeti hii tayari tumetenga bilioni Nane kwa ajili ya kuanza kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ufafanuzi huo sasa ninaomba kutoa hoja.
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaafiki.