Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa (Mbunge) na Naibu wake Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mbunge), Profesa Godius W. Kahyarara - Katibu Mkuu, Bwana Ludovick J. Nduhiye - Naibu Katibu Mkuu, watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa wanazofanya kwenye kusimamia Wizara ya Uchukuzi hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa leo utahusu mradi wa Standard Gauge Railway (SGR) hapa nchini Tanzania na changamoto zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchumi wa nchi yoyote ile duniani, sekta ya uchukuzi na usafirishaji ni muhimu sana katika maendeleo ya kiuchumi. Hivyo basi, Serikali iliyo makini huchukua hatua madhubuti za kuimarisha sekta ya usafirishaji kwa kujenga miundombinu mbalimbali ya usafirishaji kama vile reli, kuimarisha usafiri wa majini na angani ili kuifungua nchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu iliyo na viongozi makini, ilichukua maamuzi ya kimkakati kujenga reli ya kisasa ya SGR kusafirisha mizigo na abiria huu ukiwa ni mwarobaini wa kutatua changamoto ya usafirishaji na kulinda usalama na maisha ya barabara zetu hapa nchini. Pamoja na gharama kubwa za mradi huu, reli hii ya SGR ikikamilika itafanya mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji kwa maslahi makubwa ya kiuchumi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali kwa uamuzi huu makini wa ujenzi wa reli ya hii ya kisasa ya SGR. Historia inaonesha kwamba ujenzi wa reli ya kwanza hapa nchini ulifanyika mwaka 1912 takribani miaka 113 iliyopita ambapo Serikali ya kikoloni nchini iliamua kuimarisha sekta ya usafirishaji na kujenga reli kwa lengo la kuunganisha miji katika maeneo ya kilimo, uzalishaji na kibiashara ambapo reli hiyo iliunganisha Dar es Salaam yenye bandari na miji ya Mwanza, Kigoma, Tanga na Arusha. Reli ya pili ya TAZARA ilijengwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SGR ni mradi mkubwa wa kihistoria ambao unatekelezwa na Serikali kwa kutumia fedha za walipa kodi wake kwa gharama ya shilingi trilioni saba. Mradi huo ni mkubwa na uwezo wake ni wa juu na sasa matatizo ya usafarishaji nchini yatapata suluhu kubwa kwani unakwenda kuimarisha na kulinda miundombinu ya barabara zetu zilizokuwa zimeelemewa na mizigo kupitia malori makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika sekta hii ya uchukuzi umeimarisha sana usafirishaji wa abiria kwani SGR yenye kasi ya kilometa 160 kwa saa inachukua saa tatu kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na inakadiriwa itachukua saa nane kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza. Reli hii imeleta furaha kubwa kwa watu kwani wasafiri walikuwa wanatumia saa tisa hadi 10 kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mizigo, tunaishukuru Serikali kwani katika hotuba ya bajeti iliyosomwa leo tarehe 15 Mei, 2025 Serikali imesema huduma hiyo itaanza mwezi Juni, 2025. Reli hii ya SGR itakuwa na uwezo wa kubeba tani milioni 10,000, kwa mkupuo sawa na malori 500 yenye tani 20, treni tano zenye tani 10,000 na kuwa na kasi kubwa ya kilometa 160 kwa saa, tofauti na ya sasa ambayo ina kasi ya kilometa 30 kwa saa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasemekana kwamba katika Bara la Afrika itakuwa ni reli pekee yenye uwezo mkubwa kama huo, tani milioni 10 -17 zitasafirishwa kwa mwaka, kwa hiyo, SGR itakuwa mwamba katika sekta ya usafirishaji hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya SGR inaweza kuwa njia rahisi na nafuu ya kusafirisha mazao kwenda masoko ya ndani na nje ya nchi. Kwa yale mazao yanayoharibika haraka, ni muhimu Serikali iwekeze kwa kununua mabehewa ya kubeba mazao haya na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi mazao yanayosafirishwa nje kama mbogamboga au nyama ili kuhifadhi ubora. Katika zile stesheni za kimkakati, ni vyema Serikali ikajenga cold rooms zitakazotumia kuhifadhi mazao yanayoharibika haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya usafirishaji wa mizigo hasa ile mikubwa inayotoka bandarini kwenda sehemu zingine za nchi na nyingine nje ya nchi, uwepo wa reli imara kama hii ya SGR itasababisha utendaji kazi wa bandari zetu za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Zanzibar kuwa na ufanisi mkubwa. Ufanisi wa bandari hizi unategemea sana uwepo wa miundombinu imara kwa upande wa nchi kavu, kama reli imara. Serikali yetu yenye viongozi imara imeliona hilo ndiyo maana ikatekeleza ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa reli ya SGR umetupeleka kwenye teknolojia mpya kabisa ya reli na katika sekta ya usafirishaji, kwani matatizo mengi ya barabara yanatokea kwa sababu ya mizigo mizito na ilikuwa hakuna reli imara ya kubeba mizigo hiyo. Kwa hiyo, ujenzi wa reli hii ni maamuzi sahihi yaliyofanywa na Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yetu kwa maono haya. Ili kwenda sambamba na teknolojia hii mpya. Naishauri Serikali kuwapa mafunzo wataalam wa ndani watakaosaidia kutatua changamoto za kiufundi kwenye uendeshaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hiyo ambayo inatumia nishati ya umeme imekuja wakati muafaka ikiwa Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Mto Rufiji (Rufiji Hydroelectric Power) wenye kutoa megawati 2,115, kwa hiyo, kama mipango itawekwa sawa, treni hiyo itapata umeme wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza sana Serikali kwani hadi sasa ujenzi wa kipande cha kuanzia Dar es Salaam - Morogoro - Dodoma kimekamilika na kuanza kutumika. Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa mradi huo kuelekea Mwanza (kilometa 1219) na baadaye Tabora - Kigoma (kilometa 506), na Uvinza - Musongati (kilometa 240). Ninaishauri Serikali iendelee kuwekeza kwenye mradi huu kama ilivyopangwa ili tupate suluhisho la usafirishaji abiria na mizigo kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na nchi jirani za DRC Congo, Burundi, Rwanda na Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na ufanisi mkubwa kwenye sekta ya usafirishaji nchini kwa kubeba mizigo tani nyingi, lakini pia kasi yake katika kusafirisha abiria, kutoka Dar es Salaam - Dodoma ambapo treni inafanya safari mara nane kwa siku, hivyo kuleta mafanikio makubwa katika sekta ya usafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mradi huu kuelekezwa Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa, ninaiomba Serikali ijenge reli ya SGR itakayounganisha Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro na Arusha). Ninaleta ombi hili kwa sababu upanuzi wa reli kuelekea Mikoa ya Kaskazini italeta faida kubwa sana za kiuchumi. Mikoa ya Kaskazini ina malighafi za kutengeneza cementi (gypsum), madini ya soda ash ambayo inasemekana yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 100. Usafiri wa uhakika unahitajika kubeba shehena za mizogo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa upande wa utalii kuna vivutio maarufu kama Milima ya Kilimanjaro na Meru, mbuga maarufu za wanyama za Kilimanjaro, Arusha, Tarangire, Mkomazi, Manyara, Serengeti na Ngorongoro. Ujenzi wa reli ya SGR itakuwa chachu ya maendeleo kwa Mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwa kurahisisha kusafirisha mizigo na watalii kwenda maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio tuliyoyapata, ninaishauri Serikali iboreshe mambo yafuatayo ili kuondoa baadhi ya kero zilizojitokeza kwenye kuwahudumia wasafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida kitu kipya mara nyingi huwa na changamoto. Huduma za usafiri wa SGR zimekabiliwa na changamoto za kukatikakatika umeme mara kwa mara. Ninaishauri Serikali ihakikishe kuwa umeme unakuwa wa uhakika katika mradi huu wa kielelezo ili usiwe mradi wa kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vituo vya kupanda na kushusha abiria, maeneo ya kukaa abiria ni madogo sana. Hii imekuwa kero na inasababisha msongamano mkubwa wa watu jambo ambalo siyo jema kiafya. Ninaishauri Serikali ijenge maeneo ya kutosha kwa ajili ya abiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye stesheni za SGR kuna viti vichache vya kukalia abiria. Kwenye vituo hivi kuna abiria wengi ambapo wengine hawawezi kusimama muda mrefu kutokana na umri au magonjwa. Ninaishauri Serikali ihakikishe kila stesheni inakuwa na viti vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wasafiri wengi wa SGR wanaopenda kusafiri na mizigo, lakini menejimenti ya SGR imeweka kikwazo cha kusafiri na mizigo ya ziada. Ninaishauri Serikali iruhusu mizigo kwa kulipia kila uzito unaozidi kama wanavyofanya kwenye ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kubwa ni ile ya ukosefu wa usafiri wa uhakika na unaoeleweka wa kuchukua na kuleta abiria stesheni. Kuna malalamiko makubwa ya shida ya usafiri kutoka na kuingia vituo vya SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali ishirikishe wadau mbalimbali ili wachangamkie fursa hii ya kuondoa shida ya usafiri wa kuingia na kutoka katika vituo vya SGR. Ni vyema viongozi wa mikoa husika ambako SGR inapita wahakikishe unakuwepo usafiri wa uhakika ili wananchi wasipate shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe kwa kusema kwamba ujenzi wa reli ya SGR unaenda kuimarisha sekta ya usafirishaji hapa nchini. Tumeonesha kwamba nchi yetu inaweza kufanya makubwa ikiwa tutajipanga vizuri. Ujenzi wa reli hii ukikamilika, Taifa litanufaika kwa kiwango kikubwa. Nisisitize kwamba kuna umuhimu wa kujenga reli ya SGR kuelekea mikoa ya Kanda ya Kaskazini ili pia iwe chachu ya maendeleo katika maeneo haya na nchi yetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.