Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Dkt. Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mbunge), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa Uchukuzi, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Uchukuzi, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimazi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miezi tisa ya bajeti inayoishia Juni, 2025 Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, imetekeleza miradi mingi ya miundombinu ya reli, bandari na uimarishaji wa safari za anga ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa hatua nzuri za utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na uboreshaji wa bandari utaimarisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu. SGR na bandari ni nguzo imara ya kiushindani katika biashara ya usafirishaji wa ndani na nchi za Maziwa Makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati. Bandari za Tanzania ni lango la usafirishaji kwa Zambia, Malawi, DR Congo, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan ya Kusini na hata Zimbabwe na Msumbiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea kwa kasi ile ile na pia napongeza jitihada za kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vya masharti nafuu kugharamia ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na huduma katika bandari zetu hususana Bandari ya Dar es Salaam ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa bandari zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Dar es Salaam inakumbana na ushindani mkubwa toka Bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji), Nacala (Msumbiji), Durban (Africa Kusini), Lobito (Angola) na Walvis Bay (Namibia). Maboresho ya bandari zetu iendane na kuondoa changamoto zingine ambazo zinasababisha gharama kubwa za usafirishaji kwa bandari zetu na kusababisha kupoteza biashara ya usafirishaji kwa bandari shindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanisi wa bandari unategemea pia maboresho ya barabara, reli ya kati (TRL), reli ya TAZARA, utendaji wenye tija wa wadau wote wa bandari na hata watumishi ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa karibu 72% ya mzigo wote wa nchi za nje unasafirishwa kwa kupitia Dar es Salaam Corridor ambapo DR Congo ni 36%, Zambia 31% na Malawi 5%. Pamoja na fursa za kijiografia ya bandari zetu, mzigo unaopita sasa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ni 50% tu ya biashara yote ambayo kwa sasa inashikiliwa na bandari shindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya kunusuru biashara hii inayopotea kwa bandari shindani, Serikali ichukue hatua za haraka kuboresha huduma za TAZARA ikiwa ni pamoja ya maboresho ya miundombinu ya reli, ununuzi wa vichwa vya reli, mabehewa na vitendea kazi vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali kwa haraka ishughulikie maboresho ya mkataba wa TAZARA na kisha kutafuta washirika kutoka sekta binafsi kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya reli na hata uendeshaji kwa mfumo wa PPP. Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa na hata mfumuko wa bei wa mafuta ya petroli, mbolea na bidhaa mbalimbali, usafirishaji wa reli ni mojawapo ya suluhisho kubwa kupunguza mzigo wa bei kubwa kwa wateja wa bandari zetu na hata wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maboresha ya reli ya TAZARA, napendekeza kuendelea na ujenzi wa Bandari Kavu Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki katika kuwezesha kupunguza gharama za kusafirisha kwa wateja wa bandari na hata kupunguza bei za mafuta ya petroli, pembejeo na mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari Kavu ya Mbeya ni njia panda kwa wateja wa nchi za Malawi, Zambia, DRC, Lubumbashi na hata kwa Zimbabwe na Msumbiji. Serikali ichukue hatua za haraka kuinusuru reli ya TAZARA hata ikibidi kurekebisha mikataba ya umiliki na uongozi ili mradi iendeshwe kwa tija. Kuna kuchukua hatua za makusudi kwa kutumia zaidi TAZARA kusafirisha mizigo ambayo imeelemea hata uwezo wa barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usafirishaji wa mizigo kwa kutumia TAZARA ilenge kupunguza gharama za mafuta ya petroli, pembejeo kwa wakulima na wakati huo kupunguza gharama za kusafirisha mazao ya wakulima. Pamoja na kuboresha TAZARA, napendekeza kukamilisha taratibu za ujenzi wa Bandari Kavu ya Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto za mfumuko wa bei za mafuta na pembejeo, kuna fursa kubwa na hasa mahitaji makubwa ya mazao ya kilimo kwa soko la ndani na nje. Uzalishaji kwa tija unategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa miundombinu ya reli na viwanja vya ndege ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa Songwe kwa usafirishaji wa mazao yetu kwa soko la ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho ya uwanja wa ndege wa Songwe uende sambamba na ujenzi wa maghala mahususi wa maua, mbogamboga, parachichi, nyama, viwanda vya kutengeza thamani za mazao na madini na EPZ/Industrial Park.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.