Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namtanguliza Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri mno inayofanywa nchini kutokana na Wizara ya Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii Profesa Mbarawa kwa kuongoza Wizara na utekelezaji wa miradi mbalimbali na kazi nzuri tumeiona. Hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee na pongezi nyingi kwa Naibu Waziri David Kihenzile, pia Katibu Mkuu, Naibu Katibu na watendaji wote wa Wizara hii. Hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitaanza na ujenzi wa viwanja vya ndege nchini; pongezi nyingi sana kwa Serikali kwa ujenzi wa viwanja vya ndege nchini kikiwepo kiwanja cha ndege cha Iringa, hongera sana. Tunaiomba sasa Serikali kabla haijaanza ujenzi wa viwanja vingine ufanyike upembuzi yakinifu ili kukamilisha majengo ya abiria. Uwanja wetu wa Mkoa wa Iringa umekuwa na abiria wengi sana na kumekuwa na changamoto kwa abiria hasa miundombinu ya vyoo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ATCL napongeza uteuzi wa kiongozi wa shirika hilo Bwana Simbaulanga, kwa kipindi kifupi amefanya kazi nzuri sana na kwa niaba ya wananchi wa Iringa tunashukuru kwa kuanza kuleta ndege ya abiria katika kiwanja chetu cha Iringa, lakini hayo marekebisho yafanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa ushauri wangu hapa Dodoma ni makao makuu ya nchi yetu, ni vizuri ndege zote kuwe na safari za kuunga kutoka Dodoma mfano Mwanza - Dodoma, nia ya ushauri wangu kuwepo na ndege za kutoka maeneo yote lakini connection iwe hapa Dodoma ili kuwapa wepesi abiria wa maeneo yote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa nchini ya SGR; pongezi nyingi sana kwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Reli Bwana Kadogosa kwa kazi nzuri sana aliyoifanya katika shirika hili kwa sababu ujenzi wa reli nchini unakwenda kuponya hata barabara zetu, pia kuleta urahisi kwa huduma za usafiri na usafirishaji. Tunaomba sasa ujenzi uendelee kwa kasi kubwa na niungane na Kamati kuomba sasa Serikali inaaza ujenzi wa reli ya kisasa na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo baadhi ya malalamiko kwa abiria tunaomba yaangaliwe na yafanyiwe kazi ikiwemo mizigo inayozidi bei ni kubwa kuliko hata bei ya ndege, hili liangaliwe upya. Pia ikiwezekana kuwe na open ticket kama katika nchi nyingine ili kama utachelewa treni na hakutumia tiketi iweze kutumika kwa kubadilisha tiketi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niombe reli ya TAZARA ipewe kipaumbele kusimamiwa, pia naomba kujua yale malipo ya wafanyakazi wa TAZARA yalifikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kubwa sana kwa Serikali kuhusiana na uendeshaji bandari yetu kwa kweli ni mapinduzi makubwa sana, tumeona ongezeko kubwa la mapato. Hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.