Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kwa kunipa nafasi niweze kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu ili niweze kuchangia hii Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wetu, Makame Mbarawa na Naibu wake Kihenzile lakini na timu nzima ya hii Wizara ya Uchukuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza kwa hatua kubwa hatua mbalimbali ambazo wameendeleanazo katika kuhakikisha kwamba wanatuletea mapinduzi makubwa katika hii Sekta ya Uchukuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kufanya kazi na Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa kwa kweli ni Waziri ambaye msikivu yeye hasubiri kukaa ofisini ili mtu aende kupeleka hoja. Mahali popote unapokutananae unapomweleza hoja yako wakati huo anaisikiliza na kuweza kuifanyia kazi. Mwenyezi Mungu aendelee kubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niendelee kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa namna ambavyo ameleta mapinduzi makubwa katika sekta hii na ukiangalia hotuba ambayo imesomwa na Waziri hapa kwa kweli hatuna cha kusema zaidi ya kuendelea kumuombea Mheshimiwa Rais wetu ili Mwenyezi Mungu aendelee kumwongoza. Kwa sababu sasa tunaelekea katika mapinduzi makubwa ya hii Sekta ya Uchukuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mradi wa SGR umekuwa mkombozi mkubwa sana lakini tumeona hatua mbalimbali ya kuendeleza SGR hata kule Kusini kutoka Mtwara kilomita 371 kwenda Mbamba bay pamoja na maunganisho ya maeneo mengine. Sisi kwetu tunaona kwamba ni mapinduzi makubwa na tunaamini kwamba mradi huu kadri ambavyo unaendelea na sisi wana Lindi kutoka Lindi kwenda Kibiti kuja Dar es Salaam kiunganishi cha kutoka Mtwara tutakwenda na SGR. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu ya kwamba niishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali ya kutuletea mradi huu wa Ujenzi wa Chuo cha NIT, chuo hiki tulikata tamaa lakini tunashukuru kwa hatua mbalimbali ambazo zimesimamiwa kupitia hii Wizara ya Uchukuzi na sasa chuo hiki kinakwenda kwenye utekelezaji.
Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana kwa sababu nilikuwa ninakukera sana juu ya ujenzi wa chuo hiki lakini sasa nimeona katika taarifa ambayo leo umeisoma sasa tunaelekea kwenye utekelezaji wa ujenzi wa chuo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wana Lindi tunaona kwetu ni mapinduzi makubwa, kwa sababu tulikuwa na kilio cha muda mrefu Lindi tangia ianze ilikuwa haina chuo hata kimoja. Lakini leo tunazungumza tuna vyuo karibia vinne, vitatu viko katika hatua mbalimbali za ujenzi lakini tuna chuo cha madaktari pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kwetu tunaona kwamba tunaendelea kupiga hatua mwaka hadi mwaka na tunasema ya kwamba sisi tuna deni kubwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. Dkt. Samia Suluhu Hassan siyo wakuja kuomba kura Lindi, sisi wana Lindi tuna kila namna ya kuhakikisha kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan anashinda kwa kura nyingi za kishindo. Kwa sababu hatuna cha kumshukuru zaidi ya kwenda kumpigia kura nyingi na endelee kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uboreshaji wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Lindi. Nimeona katika taarifa ya bajeti na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri sasa ninaona kwamba tunaelekea kwenda kwenye utekelezaji wa uboreshaji wa uwanja huu, kwa sababu kwa miaka minne mfululizo unawekwa ndani ya bajeti lakini utekelezaji wake hauonekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe uwanja huu una historia yake. Kwanza tumerithi kutoka kwa wakoloni lakini uwanja una run way nane ni uwanja mkubwa kuliko uwanja mwingine. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri ninajua kwamba anatamani kuhakikisha kwamba uwanja ule unaboreka. Changamoto kubwa iliopo ni upatikanaji wa fedha lakini ninaamini kwa sababu sasa hivi upo katika hatua nzuri ya utekelezaji na umeishapitia hatua mbalimbali, maana yake sasa unakwenda kwenye utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Ndulane ameongea, kipaumbele chetu cha Wabunge wote wa Mkoa wa Lindi na Mtwara ni Barabara. Sisi tuna changamoto kubwa sana ya barabara na hatuna njia nyingine mbadala ya kusafiri kwa sababu hatuna ndege inayokuja Lindi na uwanja haueleweki. Lakini hatuna bandari japokuwa bandari ipo. Miaka ya ukoloni ya nyuma ilikuwa MV Mapinduzi inafunga gati Lindi lakini leo hatuna cha kuzungumza juu ya bandari ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri. Kwanza kuhakikisha kwamba barabara yetu inayotoka Dar es Salaam – Kibiti – Lindi – Mtwara tuendelee kuiboresha kwa kiwango kikubwa. Hali ya barabara imekuwa mbaya mno, watu wanashindwa kusafiri, watu wanashindwa kusafirisha mizigo pamoja na kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Sisi tuliamini kwamba sasa tunakwenda kwa hatua kubwa kupiga hatua kubwa za kiuchumi katika kuufanya Mkoa wetu wa Lindi sasa usonge mbele kimaendeleo lakini tunarudi nyuma kwa sababu ya barabara siyo nzuri hakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wadogo wadogo sasa wameamua kutumia Bandari ya Lindi, Lindi kuna meli ndogo ndogo ambazo zinafunga gati pale kupakia. Wanapakia mbuzi, kuku, nazi, maembe, mihogo na bidhaa mbalimbali zinakwenda Comoro. Kutoka Lindi kwenda Comoro ni pafupi kuliko Dar es Salaam kwenda Comoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana Serikali itusaidie kuhakikisha kwamba pamoja na udogo wake uliopo watukarabatie Bandari ya Lindi sasa tufungue fursa za kiuchumi ambazo tunazitarajia Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba uchumi wetu utakua lakini bandari yetu itatumika mapato ya Serikali yatapatikana lakini kuhakikisha kwamba ajira kwa vijana wetu zitapatikana. Kwa hiyo, nimuombe sana Profesa Makame Mbarawa aone namna gani ya kuweza kutusimamia kuhakikisha kwamba tunaboresha bandari ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nimuombe katika kuzunguka uwanja wa ndege palikuwa na wananchi ambao wamekaa kwa muda mrefu zaidi ya miaka thelathini, arobaini. Lakini wamewekeza shughuli za kilimo pale kwa muda mrefu, sasa hivi mnawahitaji waondoke wale wananchi. Niwaombe sana Serikali wafanye namna yoyote ya kuona namna gani wanawatoa waweze kwenda kutafuta ardhi maeneo mengine kufanya shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nikushukuru sana na ninaunga mkono hoja 100%. na nimtakie kila la kheri Mheshimiwa Waziri ili kuhakikisha kwamba fedha zinapatikana kwenda kutekeleza miradi ambayo imeainishwa katika kupitia kitabu chake cha Hotuba ya Bajeti. Ahsante sana. (Makofi)