Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Francis Kumba Ndulane

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kuhusu Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitangulie kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya katika sekta hii ya uchukuzi. Kwa kweli Serikali yetu ya Awamu ya Sita imetumia fedha nyingi kuwekeza katika Bandari ya Mtwara, Dar es Salaam pia bandari zilizoko katika maziwa makuu kwenye upande wa usafirishaji, vyombo vya usafiri kama meli pia hata bandari zenyewe na mazingira yake pamoja na viwanja vya ndege vimeboreshwa. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Daktari Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupongeze Mheshimiwa Waziri, wewe ni Waziri Makini, Profesa Mbarawa umefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na msaidizi wako Mheshimiwa Kihenzile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo moja kubwa la msingi ni kuhusu shughuli za usafirishaji na usafiri katika mikoa ya Kusini. Kwa muda mrefu hadi Bunge hili tulipokuwa tunachangia kwenye Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na bajeti zingine ikiwemo ya Wizara ya Ujenzi. Wabunge wengi wa mikoa ya Kusini tulikuwa tukihimiza kwamba, kipaumbele chetu cha kwanza katika huduma ya uchukuzi ni suala la barabara. Kipaumbele cha pili tulisema ni barabara, kipaumbele cha tatu ni barabara. Na hii ilitokana na kutokuwa na usafiri wa aina nyingine katika hiyo mikoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nafikiri sasa kupitia Wizara ya Uchukuzi, twende na vipaumbele vitano. Kipaumbele chetu cha kwanza kibaki kuwa barabara, kipaumbele cha pili, kiwe ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Mtwara, kutoka Mtwara mpaka Mbamba bay. Pia, kuwe na branch kutoka kule Mbamba bay kwenda Liganga na Mchuchuma, kwenda Songwe hadi Kiwira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu wilaya zetu za Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma sasa hivi zina resources nyingi na kuwepo kwa usafiri wa barabara peke yake tulishuhudia mwaka jana 2024 na mwaka huu 2025, barabara yetu ikiwa imekatika sana, imeharibika mara kwa mara na kwa hivyo kusababisha shughuli za usafiri kusimama kwa wakati fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia volume au wingi wa mizigo umekuwa ukiongezeka hasa baada ya kufunguliwa Kiwanda cha Cement cha Dangote lakini yanapatikana madini ya jasi kule Kilwa kwa wingi sana yanatumia barabara hiyo hiyo. Pia hata makaa ya mawe yanayopatikana kule Ruvuma nayo yanapita katika barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii imesababisha barabara kuchakaa mapema na kuharibika mara kwa mara hasa baada ya tufani ya Kimbunga Hidaya na Mvua za El Nino. Kwa hiyo, niombe wizara iangalie haya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa SGR kama nilivyosema hayo maeneo yaangaliwe kwa mara ya kwanza tupate SGR inayotoka Lindi kwenda mpaka Mtwara kupitia Kilwa. Itaweza kubeba hizo rasilimali zote zilizopo pamoja na mazao ya korosho na ufuta kuweza kuyapeleka bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa bandari, tunayo bandari yetu ya Kilwa ya uvuvi ya kisasa kabisa inajengwa pale na iko zaidi ya 80% imeishakamilika. Wizara yetu ya Uchukuzi iliwahi kutufahamisha Wanakilwa kwamba ile bandari itajengewa gati ya kuweza kuchukua abiria na ikipatikana ile gati itakuwa na umuhimu mkubwa kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo na abiria kwenda nchi ya jirani ya Comoro. Pia itawezesha usafirishaji na usafiri kwenda Mafia, Zanzibar, Pemba, Dar es Salaam, Tanga na mwambao wote wa Bahari ya Hindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hotuba yako tunaomba utupe neno kidogo litakalowaletea faraja wana kusini kupitia bandari hii. Gati hii mpya ambayo ilipangwa kujengwa katika Bandari ya Kilwa. Lakini pia Bandari ya Lindi kwa miaka mingi hatujaona ikifanyiwa uendelezaji niombe Serikali iangalie pia Bandari ya Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye usafirishaji uundaji wa meli. Hizi bandari zote zinazoboreshwa nyingi Taasisi yetu TASHICO imekuwa ikitumika kujenga meli hasa kwenye maziwa makuu, kule Ziwa Victoria kuna meli mbili zipo katika hatua mbalimbali za uundaji wake. Ukienda Ziwa Tanganyika MV Liemba inakarabatiwa lakini kuna MV Mwongozo inafanyiwa matengenezo. Kwa hiyo, msisitizo kupitia taasisi yetu ya TASHICO pia ijenge meli katika Mwambao wa Bahari ya Hindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili hizi bandari tunazozijenga ikiwemo ya Dar es Salaam, Tanga na uhimarishaji wake unaofanyika, ukarabati wake unaofanyika uweze kuleta tija kubwa zaidi kwenye usafirishaji wa mizigo, abiria na kadhalika ili kupunguza lile tatizo barabara ikikatika basi mambo yanakuwa hayaendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la viwanja vya ndege. Nimesoma hapa katika Paragraph No. 126 sijaona Viwanja vya Ndege vya Kilwa, Nachingwea, Lindi kama kuna chochote kimetengwa kuhusiana na hivyo viwanja. Imezungumzwa tu kwa ujumla wake maboresho ya ITCL tunashukuru yanaenda vizuri na mambo yanakwenda vizuri. Lakini bado nilifikiri Serikali ingekuja na jambo katika viwanja vya ndege hivi nilivyovitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ukienda pia kwenye viwanja vya ndege tunashukuru wenzetu wa TAWA kule Miguruwe – Kilwa Kaskazini wanajenga kiwanja chao cha ndege. Lakini pia nilifikiri wanapaswa kuungwa mkono na Wizara ya Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla nilikuwa na hayo naipongeza sana Serikali, nampongeza sana Mheshimiwa Rais na niwaombe Watanzania wote tukampe miaka mitano tena Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nasema naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)