Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi nami nichangie Hotuba ya Waziri wa Uchukukuzi. Kwanza, nianze kwa kumpongeza sana Waziri wa Uchukuzi pamoja na Naibu wako kwa kazi kubwa mnazofanya kwenye Wizara yetu ya Uchukuzi. Pia, nimpongeze sana Katibu Mkuu na Watumishi mbalimbali waliopo kwenye Wizara hii ya Uchukuzi, kwa kweli kazi kubwa zinaonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza sana habari ya bandari, nami niungane nao kupongeza sana kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa iliyofanyika kwenye bandari yetu hasa ya Dar es Salaam. Kwa kweli, kazi kubwa imefanyika na tumeona upanuzi wa uboreshaji wa miundombinu ya bandari umeendelea kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika Mama Samia amefanya kazi kubwa, hakika Watumishi wa bandari zetu wamefanya kazi kubwa, wakiongozwa na Kaka yetu Mbosa wamefanya kazi kubwa sana kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam. Kwa kweli tunawapongeza sana na Mama Samia tunampongeza sana kwa maamuzi aliyoyachukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nilipongeza sana Bunge mwaka jana 2024, kwenye Bajeti Kuu tulipitisha kwamba makusanyo ya Wharfage sasa yaanze kukusanywa na TPA. Tumeona maendeleo makubwa baada ya makusanyo haya kuwa yameanza kukusanywa na TPA, tumeona makusanyo yameongezeka kutoka bilioni 476 kwa mwaka 2023/2024 kwa maana ya kuanzia Julai - Machi, pia kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Julai – Machi makusanyo yameongezeka kwa bilioni 22 kwa maana ya kuleta jumla ya bilioni 499. Haya ni mapinduzi makubwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam na bandari zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona uboreshwaji wa maeneo, wenzangu wamesema Bandari ya Mwanza imeendelea kuboreshwa, Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa matenki, pia gati namba moja mpaka gati namba saba, upembuzi yakinifu wa gati namba nane mpaka 11, gati namba 12 mpaka gati namba15 tunaona maendeleo makubwa sana yamefanywa na nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Mama Samia ananikumbusha hadithi moja ya Yohana Mbatizaji alipokuwa gerezani baada ya kutembelewa na wafuasi wake, na aliamini kwamba kwa kuwa Yesu anaweza kila kitu aliamini atatoka gerezani kwa miujiza. Na akauliza akawaambia wale wafuasi nendeni mkamuulize Yesu je, ni yeye au tunasubiri ajaye? Yesu akawajibu akawaambia nendeni mkamwambie wafu wanafufuka, viwete wanatembea pia vipofu wanaona. Kiongozi mzuri hapimwi kwa maneno, kiongozi mzuri anapimwa kwa kazi na Mama Samia tumempima kwa kazi kubwa na amefanya kazi kubwa kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Watanzania leo tukiulizwa kwamba, nendeni mkamuulize yeye ndiye au tusubiri ajaye tutasema yeye ndiye kwa sababu ya maendeleo makubwa ambayo tumeendelea kuyaona kwenye Taifa letu hasa kwenye bandari na kwenye SGR. Wenzangu wamechangia sana suala la SGR kwa kweli hapa ndipo tumeona maendeleo makubwa ya nchi yetu na sasa tunaenda kwenye uchumi, tunaamini kazi itaendelea kufanyika, tuendelee kumuunga mkono Mama Samia, tuendelee kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi, makubwa yanaendelea kuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja kwenye eneo la SGR. nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wako Kaka yangu Kadogosa, umeendelea kufanya kazi kubwa kwenye eneo la SGR hongera sana endelea kufanya kazi hii kwa sababu ni eneo ambalo tunalihitaji kwenye nchi yetu na kazi hii inakuhusu wewe kama maandishi ya Biblia yanavyosema Ezra 10:4 kwamba kazi inakuhusu wewe, nyanyuka nenda na kaitende. Kadogosa unafanya kazi njema sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna study zimefanyika huko nyuma za ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia Arusha kuja Makuyuni, kuja Simiyu pale Dutwa, kupita Lamadi Busega, Bunda kwenda mpaka Musoma. Study hizi sasa nendeni mkazifanyie kazi tunatamani huko mbeleni kuona mpango wa Serikali kwenye ujenzi wa reli ya kisasa kwa maana ya SGR kutoka Arusha kwenda mpaka Musoma kupitia Simiyu Mkoani kwangu, Busega Jimboni kwangu, Bunda kwa Bwana Getere na hadi Musoma. Na tunaamini ujenzi wa reli hii utakapokamilika uchumi wa wananchi utaongezeka, uchumi wa nchi utaongezeka, usafirishaji wa mizigo, usafirishaji wa mazao pia utaongezeka na utawarahisishia wananchi wetu Watanzania katika suala zima la kusafirisha mizigo na usafiri wa wao kwa wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Kaka yangu Kadogosa, niombe sana mkubwa wangu Mheshimiwa Prof. Mbarawa kuangalia study hii ambayo imefanyika huko ili tuwe na mpango wa ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia kule Arusha kuja Simiyu na kwenda mpaka Musoma. Mafananikio makubwa tutayapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakati tunasoma shule ya msingi tulikuwa tukiangalia zile sinema anakuambia hiyo trailer muziki baadaye. Tumeona trailer ya SGR hapa Dodoma kwenda Dar es Salaam, tumeona mafanikio makubwa haya, tumeona wananchi wananufaika na SGR hii. Tuna imani kubwa SGR pia ya kutoka Arusha kwenda Musoma itawanufaisha Watanzania, itawanufaisha wananchi wa Simiyu na wananchi wa Jimbo la Busega.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Dutwa kuna madini ya Nickel nafikiri pia usafirishaji utaendelea kupitia SGR na kwa sababu mapato yetu yatazidi kuongezeka kupitia aina hii ya usafirishaji kwa kutumia SGR. Ni imani yangu kubwa study hii mtakapoifuatilia na kuja na mpango sisi kama Wabunge tutawapitishia mpango na kwa sababu wananchi wa Jimbo la Busega wamesema bado wanatamba nami najua nitakuwa hapa nitaendelea kuwapitia bajeti yenu ili muende kufanya kazi ya ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia kule Arusha kwenda Musoma. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nusu dakika ni kwamba nimemuona hapa Kaimu Waziri Mkuu mzee wangu Mkuchika niseme tu jambo moja. Wizara ya Katiba na Sheria walikuja na kampeni ya Samia legal campaign.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba msimamizi wa shughuli za Serikali hapa Bungeni, siku ya tarehe 15 Juni, 2025 Derby ya Simba na Yanga tuipe jina ya Samia Derby campaign ili tuendelee kumuunga mkono Mama Samia ili tuendelee kuunga mkono michezo katika nchi yetu. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mzee wangu Mheshimiwa Mkuchika achukue hilo alipeleke mje na mpango, mje na Sami Derby Campaign na ambaye hatapeleka timu tutaona ana matatizo.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)