Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya, lakini ninawashukuru na wenzangu wote humu Bungeni, sasahivi ninawaona wako wazima na wana afya njema sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Waziri wangu, kaka yangu, Makame Mnyaa pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa anayoifanya katika Wizara hii; mimi niko Kamati hii ya miundombinu, nimetembelea mambo mbalimbali katika miundombinu. Nimetembelea bandari, nimetembelea viwanja vya ndege, lakini pia nimetembelea treni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana ndugu yangu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua kubwa aliyoichukua na anaendelea kuchukua. Ni Mheshimiwa mwenye maono, anayeona mbali na kisha anatekeleza. Mwenyezi Mungu amwondolee shari na ampe heri, amjalie uzima yeye na wanaoongoza nyuma yake, ili aweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wengi wamezungumzia mazuri sana na mimi niseme ukweli, mazuri yapo, lakini kitu chochote kilicho kizuri hakikosi kasoro. Kitu kikiwa kizuri ni lazima na kasoro itakuwepo, mimi katika kusafiri kwangu, sasahivi ninatembelea sana treni, ninatoka hapa mchana ninaingia kwenye treni jioni na usiku; ukiingia treni ya usiku tu unaambiwa uvutaji wa sigara hautakiwi, lakini pombe inanywewa na inakuwa hatari. Sijui hii Serikali kama inalitambua hili jambo au vipi? Kutuharibia katika safari zetu za treni! Tunapendeza mule wenyewe tukikaa, vichwa vinatulia tu mpaka usingizi unakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pombe mule imezidi, Mheshimiwa Waziri unanisikia? Kaa kitako na wenzio, wafanyakazi, uwaambie watulie, wanywaji wanapiga kelele na wanacheza ngoma wala hazimo! Mheshimiwa Waziri hili nimeliona, changamoto hii ni kubwa katika treni zako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kweli, wenzangu wamezungumza treni zinafanya kazi vizuri, ni za kisasa na wala hapa Tanzania haijapata kutokea. Yote hayo msimamizi ni Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan.
MBUNGE FULANI: Endelea, endelea.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ninazungumzia kuhusu ndege. Ndege zetu sasahivi hazina matatizo, zinakwenda vizuri. Yaani utasema hizi ndege ni kama zinajipangilia kwa sababu, wanaona kuna ushindani wa safari. Watu wengi wanakwenda kwenye treni na huku ndani ya ndege sasahivi hata zile nauli kidogo zimepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna huku ku-delay, ndege unaambiwa saa tatu, unaenda, matokeo yake huondoki mpaka saa tano za usiku, hili nalo lirekebishwe. Ndiyo maana nikasema panapo uzuri hapakosi kasoro, hiyo ndiyo kasoro niliyoiona katika ndege sasahivi. Unaenda safari yako ufike kwa wakati, lakini hufiki kwa wakati, unabaki kukaa pale mpaka unachoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inakuja ndege pale saa tano ndiyo unaondoka unaenda zako nyumbani, hilo ndilo nililoliona. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ukae kitako na wenzio wajitahidi, hizi ndege zinapotoka hizo safari zije huku kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu, ni kuhusu bandari: bandari zetu zimesifiwa hazina wasiwasi. Kuna bandari za nchi kavu, lakini pia kuna bandari za baharini. Hapa kwenye Bunge lako Tukufu lilitoa suala la kuhusu habari ya maboti na Naibu Waziri Kihenzile akaniambia kuna maboti yatatengenezwa na kuletwa tuondokane na urasimu wa maboti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aboti tunatoka nayo Zanzibar kuja nayo huku Dar es Salaam yanajaa sana, mtitiriko wa maboti haujawahi kutokea nalisema hili na wenzangu wanalijua ni kweli. Kwa hiyo, tunafika pale mbanano watu hawatulii kwenye maboti wamesimama, hata tukifika pale taabani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali hilo boti walililotaka kutulea la kuanzia bahari ya maziwa mpaka kuja kwenye bahari hii watuletee itakuwa ya Serikali, labda itakuwa afadhali na upandaji wetu itakuwa afadhali. Halafu na wale wasimamizi wanaoangalia yale maboti kwa sababu niliuliza, je, hawa watu wanaoangalia haya maboti hawapo au hawafanyi kazi vizuri? Kwa hiyo, Naibu Waziri, Kihenzile akaniambia hawa watu wapo na hii meli haiwezi kuondoka kama haijaangaliwa lakini naona si kweli hawapo! Kwa hiyo, tuletewe meli yetu tuingie mle kwa usalama na amani ili tuweze kusafiri vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, 100% ahsante sana Waziri, ahsante sana Naibu. (Makofi)