Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia. Nimshukuru Mwenyezi Mungu mwenye enzi na utukufu kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo moyo wangu umejawa na shukrani. Natumia fursa hii kumpongeza sana na kutoa shukrani nyingi za dhati kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Profesa Makame Mbarawa, kwa Katibu Mkuu, pamoja na mtendaji wa Mamlaka ya Bandari kwa mapinduzi na mageuzi makubwa ya Sekta ya Bandari na Uchukuzi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka ya karibuni tu Bandari ya Tanga tulikuwa tunatajwa tuna mwamba usiochimbika uliosababisha Bandari ya Tanga kujiendesha bila faida kwa sababu, meli zilikuwa hazifiki gatini, leo hii tunavyozungumza Bandari ya Tanga, ndani ya miezi sita, imezalisha shilingi bilioni 45. Moyo wangu umejawa na shukrani na hakika Mheshimiwa Rais amejivua gamba la business as usual, ameonesha ni Rais ambaye hakubali kucheza kama vile watu wa zamani walivyokuwa wakisema, tumewaona baba zetu, kama hivi, wanafanya na yeye kuji-limit na kuji-confine hapo. Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mbarawa hakika mmefanya mageuzi makubwa katika sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaizungumzia Bandari ya Tanga, ambayo ninakwenda kujengewa barabara ya lami kutoka Handeni – Kiberashi, kama toll road, kutokana na mapinduzi na mageuzi makubwa ya Mamlaka ya Bandari. Kwa kweli, moyo wangu umejawa na shukrani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka ya karibuni tu tulikuwa tunazungumzia ma-gati ya bandari zetu kuu yamejengwa kwa sheet piles ambazo zilikuwa ni lazima ufanye electrolysis uondoe hydroxyzine irons, ili kuzuia chumvi isiweze kuharibu sheet piles zile. Leo tunazungumzia miundombinu ambayo ma-gati yamejengwa kwa zege nzuri na zimeongezwa meta kumi ndani ya maji, hakika ni mageuzi makubwa katika sekta hii ya bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mwaka 2000 tu tulikuwa tunazungumzia wizi wa mafuta bandarini; tulikuwa tunazungumzia upotevu wa mafuta na mapato bandarini. Leo tunazungumzia bandari zetu zenye flow meter za kidijiti, hakika ni mapindduzi makubwa katika Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka hivi karibuni tulikuwa hatuna chelezo, tunabeba meli tunazipeleka Mombasa. Leo hii hiyo imekuwa historia, hakika ni mageuzi makubwa katika sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni juzi tu, ninakumbuka ambavyo tulikuwa tunahangaika na cranes zisizokuwa na uwezo wa upakuaji; tunatumia cranes ambazo mara kwa mara zinaharibika, tunapoteza fedha nyingi kwenye matengenezo. Leo hii tunazungumzia ship to shore gantry cranes ambazo zinaweza kuingia zenyewe mita 50 ndani ya maji kutokana na rail space yake. Hakika ni mageuzi makubwa kwenye sekta ya bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka vizuri tangu Awamu ya Kwanza ya Profesa Mbarawa katika sekta hii akiwa ni Waziri, enzi za Magufuli, alivyokuwa king’ang’anizi na mfuatiliaji wa karibu mpaka Mr. DK. Qube akawa anamuona nuksi pale bandarini, lakini leo tunayaona mageuzi makubwa kwenye Sekta hii ya Uchukuzi. Hakika moyo wangu umejawa na shukrani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi karibuni tulikuwa tunazungumza namna ambavyo tunaweza tukapunguza muda wa utekelezaji, ili mtu ambaye yuko kwenye hoteli anakunywa kikombe chake cha kahawa anaiona meli yake namna ambavyo inasogea kwenye gati na namna ambavyo inahudumiwa. Leo tumeingiza TEHAMA katika utekelezaji wa shughuli za kibandari na tunayaona mafanikio yake. Moyo wangu umejawa na shukrani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli ninaona fahari kubwa kwa mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika Sekta hii ya Bandari na kipekee, hili la kuhakikisha tumepata private sector kuweza kuiendesha bandari. Vijana wa bandari walikuwa wanabembelezwa kuingia DP World mpaka mkurugenzi mkuu anawaongezea mishahara, nendeni mkahudumu; kwa kweli, ni mapinduzi makubwa kwa sababu, mimi nimekuwa pale, nilikuwa ninaona treatment ya wafanyakazi ikoje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii bandari imetulia. Hakika ni mapinduzi makubwa na ni pongezi kwake kijana, ambaye yuko very well composed, Plasduce Mbossa. Anafanya kazi kubwa vizuri zaidi na niwaambie vijana wengine mlioaminiwa katika nafasi hizi, jitahidini kujifunza kupitia Mbossa, yuko very well composed na bandari imetulia; bandari ilivyokuwa juzi, sivyo ilivyo sasa hivi. Hakika mmeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikumbushe, nilisema haya wakati wa mchango wangu wa kwanza katika Sekta ya Bandari, leo ninakwenda kutimiza miaka mitano, mmefanya mengi makubwa ya kimapinduzi katika sekta hii. Ninaomba niikumbushe bandari, mengi mmefanya, lakini bado tusipotafuta mechanism na kufanya tafiti ya kujua namna ambavyo tunaweza ku-control sedimentation na kina cha bahari kupungua, bado kutakuwa na challenge mbele yetu. Niwaombe sana Mamlaka ya Bandari pamoja na Wizara husika kuwekeza katika kujua ni kwa nini kuna sedimentation rate kubwa na kwa nini kina kinapungua katika bandari zetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje na mechanism ambayo italinganisha dragging na kuchimba. Tuone ipi ina thamani ndogo, kuweza kuleta matumizi yaliyosahihi katika sekta ya bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa reli ya kisasa na kwa ujenzi mkubwa unaoendelea, ambao kidunia ni nchi mbili tu ndizo zinaweza kutekeleza mradi mkubwa kama huu wa reli wa nchini Tanzania, ni China na Saud Arabia pekee ndiyo zinaweza kutekeleza mradi huu ambao ukikamilika kilometa zake 4,700 hakika Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mama wa Kizimkazi, ambao walimchukulia poa, aisee wakae kisawasawa. Inabidi tu wazoee kwamba, Dkt. Samia Suluhu Hassan mambo yake siyo ya kitoto, anashindana na China na Saud Arabia kuwa na mradi mkubwa kama huu. Hakika ni mageuzi makubwa katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumalizia. Ninaomba nizungumzie viwanja vya ndege; ninaomba nikizungumzie Kiwanja cha Ndege cha Msalato. Kiwanja kinajengwa, ombi langu ni kuhakikisha hatukifanyi kikawa kama Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaam; hakiwi Vingungutilised, lazima tuweke miundombinu inayoendana na kiwanja cha ndege cha kimataifa. Ni lazima kuwe na land use plan nzuri kuzunguka Msalato Airport kwa maana ya hoteli, business centres na mambo mengi, ili kuendana na kiwanja cha ndege cha kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuhitaji Msalato Airport iwe Vingungutilised, tunahitaji Msalato Airport iwe airport ya Kimataifa, ya mfano. Tujifunze kutokana na makosa ya kiwanja cha ndege kingine cha kimataifa ambacho tunacho nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalize kwa kusema kwamba, design ya Kiwanja cha Ndege cha Msalato inazungumzia kubeba passengers milioni moja na laki tano kwa mwaka, wakati kiwanja ambacho kipo sasahivi tunazungumzia passengers laki moja na hamsini mpaka laki mbili na hamsini kwa mwaka. Maana yake ni lazima kuweka mikakati ya namna gani tutaongeza capacity ya passengers hao ku-attract more investors Mjini Dodoma kwa ku-attract vivutio zaidi Mjini Dodoma, ili kiwanja cha ndege kile kiweze kuingiza idadi hiyo ya passengers kwa ku-return mapato ambayo yatawekezwa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, moyo wangu umejawa na shukrani. Hongera sana Profesa Makame Mbarawa, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Kadogosa kwa kazi kubwa kwenye miundombinu yetu ya reli. Mnaupiga mwingi, big up sana. Ahsante sana.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja 105%.