Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi ya kupata dakika hizi chache na mimi kuchangia katika Wizara yetu ya Uchukuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema wenzangu ni bahati iliyo njema kupata nafasi hii na mimi nataka kuanza kwa kutoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwanza kwa kuzigawa Wizara hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana leo tumesahau lakini nyuma Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi zilikuwa ni Wizara moja na hapo ndipo ninapomuonea huruma Mheshimiwa Profesa Mbarawa wakati ule alipokuwa Waziri alikuwa akibeba mzigo wote katika ujenzi na katika uchukuzi. Sisi ambao tuko katika Kamati ya Bunge ya Miundombinu tunajua mzigo mkubwa ambao walikuwa nao lakini kwa maoni ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezigawanya na leo tunapata matunda makubwa sana katika Wizara ya Uchukuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na Naibu Waziri wake hapa, ex - DAS kaka yetu mpole kabisa Mwakiposa na watumishi wote wa Wizara ninawapongeza sana. Pia, Wakurugenzi wote kuanzia LATRA, TASAC, TPA, TRC, ATCL, TASHICO, TMA, TCAA, TAA, TAZARA, DMI na Wakurugenzi wote kwa ujumla mnafanya kazi nzuri tumeiona kwenye Kamati na tunawapongeza sana katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utekelezaji huu mzuri wa Chama cha Mapinduzi na Ilani yake kwa hakika tutashinda mechi zote zilizobaki japokuwa ile mechi moja ya “no reform” hatutaicheza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera sana Mheshimiwa Waziri kwa kubadilisha Sera ya Uchukuzi. Tumeona kwenye Kamati na mlitupatia semina kuna Sera ya Uchukuzi ya mwaka 2003 kwamba mtaibadilisha sasa safari hii mifumo yote ya usafirishaji itasomana. Hili ni jambo kubwa sana ambalo kwa kweli tunawapongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza katika shilingi 2,746,485,000,000 mnazoziomba na ulizozisema hapa, 95% inaenda katika bajeti ya maendeleo na 4.5% peke yake ni matumizi ya kawaida. Mkifanya kazi hii vizuri na kwa bidi mtaunga mkono kauli ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kwamba tukiwekeza vizuri katika Uchukuzi, katika Bandari tutapata nusu ya bajeti ya nchi yetu na tutajikwamua sana kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema kidogo kwenye SGR, TRC na TAZARA. Nikwambie tu, nilikuwa ninarudia hotuba za nyuma za Wabunge kwenye Mabunge yaliyopita hapa. Nimeiangalia hotuba ya Mheshimiwa Heche akiwa Mbunge hapa, anaizodoa Serikali ya CCM kwamba, hiyo SGR hamtaijenga; rudieni hotuba zake mtasikia, anawaambia jengeni hiyo SGR muone. Ukiniruhusu nitakutumia video, nimesafiri kwenye SGR na Mheshimiwa Heche, alisinzia, na pembeni alikuwa na mtoto mzuri, mpaka tunashuka Dar es Salaam, anateremka kwenye belt zile mpaka chini. Ukiniruhusu nitakutumia hizo picha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninataka nimwambie Mheshimiwa Heche, anazunguka huko anatapika maneno, anamkebehi Rais, familia yake na uongozi huu, lakini SGR kapanda na alivyokuwa Mbunge hapa alikuwa anabeza. SGR sasa inapendeza, kama alivyosema Mheshimiwa Lusinde, ina maua mazuri siyo kama yale ya ATCL ya malalamiko zamani, maua yanapendeza, safari inakuwa fupi. Hata Mheshimiwa Musukuma alikuwa analalamikia kwamba, maua yale yako mengi, lakini maua yale yana faida zake, na sote tunayaunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini SGR imetusaidia kutoka saa tisa za Dar es Salaam – Dodoma kwa basi, sasahivi ni saa tatu; hilo ni jambo la msingi sana na halijawahi kutokea. Ushauri wangu kwa SGR, Dodoma, mnajaza foleni kwa kupeleka treni kule mwisho, Barabara ya Iringa, nimewaambia kuna mchakato wa kuweka kituo Stendi ya Mabasi ya Nanenane; wekeni na shusheni hata dakika tano pale kwa sababu, wananchi wengi wanatoka Dar e Salaam wanapanda mabasi ya kwenda mikoani hapa Dodoma. Unavyowapitisha unawapeleka Stendi ya Iringa inabidi warudi tena mjini, wanatengeneza foleni kubwa; shusha pale Nanenane dakika tano, lami imeshaungwa pale kwenda kwenye Kituo cha Mabasi cha Nanenane, halafu wengine wanaobaki kwenda njia ya Iringa huko, Singida, wanaweza wakaendelea. Kwa hiyo, nataka kutoa ushauri huo, ni muhimu mkalizingatia jambo hilo kwa haraka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo yanaletwa na mikakati na mipango. Nimeangalia hotuba za Wabunge wa CHADEMA wa nyuma, kaka yangu Nassari, ambaye sasahivi Mheshimiwa Rais kamteua kuwa, mkuu wa wilaya, nilikutananae juzi hapa akiwa DC. Nilimsalimia, “Kaka Nassari mambo vipi?” Akaniambia, “Salama ndugu yangu”; nikamwambia, “maendeleo vipi?”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akasema, “aah bwana, maendeleo ni mchakato. Sasahivi nimekuwa mkuu wa wilaya ndiyo ninajua kwamba, kupiga kelele peke yake bila mipango hakutoshelezi maendeleo”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasahivi yuko vijijini kule anahamasisha maendeleo na anaona ugumu wa maendeleo. Alitamani wagombea ubunge wote wa upinzani wawe ma-DC kwanza kabla ya kuanza kupiga kelele na kukosoa siku zote kwa sababu, kukosoa ni rahisi, lakini kujenga ni kugumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TRC wakamilishe kipande cha Mwanza – Tabora ambacho kiko 63% na Makutupora – Tabora kiko 14%; kamilisheni hivi, ili Watanzania wote waweze kupata raha. Nimeona kwenye taarifa yenu mnaboresha MGR na SGR na nimeona kwenye bajeti kuna kipande cha Kidatu – Kilosa, kilometa 108 kitaunganishwa na SGR. Hili ni jimbo langu, Kidatu imepooza, tunaamini mkiunganisha pale patakuwa na stendi nzuri na patachangamka sana. Kwa hiyo, tunawaomba sana mkamilishe jambo hili, ili tuendelee kukuza sekta ya uchukuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa Mkataba wa TAZARA. Septemba 2024, TAZARA sasa itafufuka na wananchi wetu watapata mafanikio makubwa. Katika hii TAZARA, na Katibu Mkuu ananisikiliza, ardhi ya TAZARA iko Tanzania japokuwa tuna ushirikiano na Zambia, nimeleta barua kwako kuomba temporary ekari moja ya ardhi katika eneo lenye ekari 20; kuna soko, zaidi ya miaka 30 halmashauri haiwezi kuendeleza soko lile kwa sababu, haijapata ruhusa ya kumiliki ardhi ile. Tumeomba kwa barua, tunaomba ekari moja katika soko la miaka mingi ambalo lipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri wapewe barua ya kutumia ekari moja, ili Mkurugenzi wa Halmashauri apate uhalali wa kutumia fedha za Serikali kujenga choo na mabanda. Hatutaki kujenga soko la ghorofa wala soko la nini, tunataka kujenga choo temporary na mabanda kwa sababu, ardhi ya TAZARA iko kwetu Tanzania tunaweza kuitumia, yatakapokuja mabadiliko baadae, mtabadilisha na mtatumia kwa vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bandari. Mmefanya uwezeshaji mkubwa wa bandari na Wabunge wengine wamesema hapa. Sasa ninajiuliza, mimi niko Kamati ya Bunge ya Miundombinu, hapa kuna taarifa kibao za kuboresha Bandari ya Nyasa, Dar es Salaam, Tanganyika, Ziwa Victoria, Mbegani Bagamoyo na Mtwara, sasa ule uongo ulikuwa unasemwa kwamba, bandari zimeuzwa katika nchi hii uko wapi? Mbona bandari zote ziko kwetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania ni lazima wawe makini na watu hawa. Nchi nzima walisema bandari zimeuzwa na kuna watu wamewaamini watu hawa, lakini Serikali inazimiliki bandari zote na inaendelea kuziboresha; za kuambiwa changanya na za kwako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika TPA ni vizuri sana mkakamilisha, nimesema mara kadhaa hapa kuhusu reli ndani ya bandari. Tunaboresha bandari kavu ya Kwala, lakini kama treni haitoi makontena pale ndani bandarini tutaendelea kupata hasara kubwa sana katika nchi yetu kwa maana ya kwamba, hakuna connection ya reli ndani ya bandari na Bandari Kavu ya Kwala na hii ya Ihumwa. Kamilisheni jambo hilo, ili muweze kuleta maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TASHIKO. Ninapenda kusema kwamba, mnafanya kazi nzuri, pamoja na TASAC kwa kumalizia… ninaomba dakika moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nisisitize, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba, hatujapata ajali za maji, lakini hii TASAC, tumeona katika bajeti na mipango ya Serikali, inatakiwa ijiongeze itumie mapato ya ndani kununua maboti ya uokozi; lolote likitokea, sasahivi wanaweza kutafuta miili? Wanaweza kufanya uokozi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona boti moja limenunuliwa Uturuki, la ambulance, ndiyo linafika sasahivi kwenda Mwanza; waongeze, wanunue mengi kwa sababu, yanachukua muda mrefu kuyajenga. TASAC ipewe uwezo, itumie mapato ya ndani iweze kujenga ofisi na uokozi, lolote likitokea tuokoe maisha ya watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ila no reforms, hatuchezi. Japokuwa mechi zilizobaki tutashinda.