Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kupata nafasi hii na mimi niweke mchango wangu mdogo kwenye Wizara nyeti kabisa Wizara ya Uchukuzi. Nikupongeze sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwa kazi nzuri, Katibu Mkuu, Naibu Waziri ndugu yetu Kihenzile kwa namna ambavyo mmekuwa mkichapa kazi bila kulala kuhakikisha kwamba nchi inakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisia miamba watatu hawa wawili walionitangulia kuzungumza wamesema maneno mazito sana kuhusu maono ya Mheshimiwa Rais wetu, msimamo wake kuhakikisha kwamba bandari inawekezwa na hii inatufanya Taifa letu liwe Taifa la kipekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wale waliokuwa wanabisha walikuwa sehemu ya kufanikisha jambo hili kwa sababu wakati mwingine ikitokea mtu akibisha mwingine ndiyo anafanya vizuri zaidi. Kama unavyoona hata kwenye michezo jamaa wakibisha sisi tunafanya vizuri zaidi, sisi tukibisha wanafanya vizuri zaidi, hivyo ndiyo inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alifumba macho akasema twende tuwekeze. Mabingwa wamezungumza kwa umakini sana namna ambavyo mapato yameongezeka lakini ninataka kusema nini kwako Mheshimiwa Waziri, Naibu wako pamoja na Katibu Mkuu? Namna mnavyosimamia utendaji wa kazi wa siku hadi siku kupunguza uzembe, uwajibikaji kuwa wa kiwango cha juu kumetufikisha kwenye mafanikio haya makubwa, tunawashukuruni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamezungumzwa hapa watu hawajui tu. Mapato haya ongezeko lake yametupa faida gani? Mpaka sasa hivi ndani ya mwaka mmoja Bandari ya Mbamba Bay inajengwa, ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta tulilisema sana kwenye Bunge hili; Serikali sikivu imeanza kujenga na speed yake ni kubwa na ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna ujenzi wa bandari ya mizigo michafu Mtwara inajengwa kwa nguvu kubwa sana. Ujenzi wa gati mbili za mita 500 Dar es Salaam unajengwa kutokana na mafanikio haya. Kwa hiyo mimi hapa ninataka kuunganisha tu watu wasiseme mbona kumeongezeka hatuoni kitu? Mapato yameongezeka na shughuli za ujenzi zimeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kazi inatakiwa kufanywa Mheshimiwa Waziri. Kweli Mheshimiwa Rais alisema aliwapa timeframe kwamba lazima treni ianze kazi na imeanza na tumeona namna ambavyo watu wanasafiri kwa haraka wanaboresha shughuli zao. Juzi mimi kuna mtu alikuwa na mgonjwa Muhimbili lakini uji ameupika Dodoma mgonjwa akaenda kunywa Muhimbili kitu ambacho zamani kisingewezekana. Zamani isingewezekana uji umepikwa Dodoma umenywewa Muhimbili - Dar es salaam halafu jioni karudi anasema nilikuwa Dar es Salaam kumwona mgonjwa. Yaani watu wanakwenda wanateleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna mambo ya kufanywa. Tunawapongeza sana kwenye reli Engineer Kadogosa, tunampongeza sana kwenye bandari Engineer Mbosa pamoja na Menejimenti yote wamefanya kazi kubwa sana watu wa manunuzi. Tumeona Engineering ikifanya kazi ya watoto wazalendo wazawa wa Taifa hili. Ndugu zangu tukiaminiana tunaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeona namna ambavyo treni yetu inasimamiwa kwa usafi mkubwa na mabinti zetu wako hapa juu. Wamefanya kazi nzuri, wanatunza mazingira, wana lugha nzuri, yaani ukisafiri ni kama unasafiri Ulaya, hili ndiyo tulikuwa tunalitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ya kufanya Mheshimiwa Waziri; kwanza elimu itolewe sehemu zote ambazo treni inapita. Kuna baadhi ya maeneo watu wanarusha mawe kwenye treni. Vitengo vyetu vya elimu, madiwani wa maeneo yale, wenyeviti wa Serikali za vijiji, sisi Waheshimiwa Wabunge tunayo training ya kutosha; kule ambako treni imeanza kazi na kule ambako itaenda kuanza kazi elimu itangulie kutolewa ili watu wajue hii treni ni mali yetu. Treni siyo ya kurushia mawe, mtu anataka kupima kasi ya treni na kasi ya jiwe, kidogo hivi vitu vinatuletea shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo mimi ningeomba nishauri kwenye reli yetu ya kati kumekuwa na hujuma nyingi sana. Watu wanang’oa vyuma chakavu sana, wanapeleka abiria kuchukua muda mrefu sana kusubiri chombo; hii inakuwa si sawa. Kwa hiyo tunawaomba sana Serikali muanzishe operation kwa watu wanaouza vyuma chakavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila muuzaji wa chuma chakavu aweke bango kwenye Ofisi yake kwamba vyuma vya reli vya aina hii marufuku kuvileta hapa ili watu waelewe kabisa kwamba chuma cha reli uuzwaji wake una taratibu, hakiwezi kuuzwa hovyohovyo na hivyo kusababisha watu ku-sabotage reli yetu. Hii itatupelekea watu tukiheshimu miundombinu, tukaheshimu utaratibu, Taifa letu litasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo mengine madogo madogo haya yasikuumizeni Waheshimiwa Wabunge. Mtu akisema “no reforms no election” wewe badilisha kidogo tu mwambie “no election no reforms” basi yaani inakuwa imekaa mahali pake. Hakuna uchaguzi hakuna mabadiliko. Uchaguzi ndiyo unaoleta nini mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko yatakujaje bila uchaguzi? Haiwezekani! Ni sawasawa unalazimisha umefunga jembe la kulimia na ng’ombe au umefunga mkokoteni na punda halafu unataka mkokoteni utangulie; mkokoteni utavuta punda? Haiwezekani. Ni lazima punda ndiyo atangulie kuvuta mkokoteni. Kwa hiyo lazima uchaguzi utangulie ili ulete mabadiliko. Jambo rahisi sana wala lisitupotezee muda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)