Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Uchukuzi ambayo ni Wizara muhimu sana kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2020 tuliweza kuwasilisha kitabu kwa Watanzania kinachoitwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi. Ilani hii ilikuwa na kurasa zipatazo 303. Ilani hii pamoja na mambo mengi kwenye Sekta ya uchukuzi ilizungumza maneno mazito sana kwenye ibara ya 58 kwenye sehemu ile ya uchukuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ilieleza kwa uwazi kabisa kwamba Sekta ya Uchukuzi, Chama Cha Mapinduzi kinatambua kuwa uendelezaji wa miundombinu ni hitaji la msingi katika kuchochea na kuwezesha Uchumi na kuwezesha maendeleo ya Sekta ya kiuchumi na kijamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ni kitabu ambacho ni mwongozo wa maendeleo ilieleza waziwazi. Wanasema siku zote tembea kwenye maneno yako. Kwa hiyo kwenye hili ninaomba niseme wakati ninaenda kuchangia, Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake imetembea kwenye maneno yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetembea kwenye maneno yake kwamba itaboresha Sekta ya Uchukuzi na kweli imeboresha. Kwenye hili ninaomba niseme waziwazi kwa hakika Mheshimiwa Rais ameonekana wazi kwamba yeye anasimamia vizuri maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Sekta ya Uwekezaji mimi nitachangia kama maeneo matatu; nitachangia upande wa bandari, nitachangia reli lakini nitamalizia upande wa anga kwa maana ya Sekta ya Usafirishaji wa Anga ambayo nitaeleza kwa ufupi sana katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kama nilivyosema kwenye Sekta hii amefanya kazi kubwa, fedha nyingi zimetolewa na tunaona namna ambavyo Sekta hii inachochea Uchumi wa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Ibara ile ya 59 imesema chama kitaelekeza Serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati. Miundombinu hiyo inajumuisha reli, viwanja vya ndege pamoja na bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la bandari niseme kwa uwazi kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri ndugu yetu Mheshimiwa Profesa Mnyaa Mbarawa pamoja na Naibu Waziri na Katibu Mkuu na watendaji wote kwa namna walivyosimamia kwa dhati maono ya Mheshimiwa Rais. Kwa hakika Mheshimiwa Profesa Mbarawa hongera sana kazi umefanya nzuri ninajua kuna kipindi weight ilipungua lakini Mungu atakuongeza weight kwa kazi kubwa uliyofanya ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alisimama kidete katika kusimamia jambo hili lilikuwa na kelele nyingi lakini leo wanaona aibu kwa kazi kubwa aliyofanya. Leo ameeleza hapa kwamba katika kipindi cha mwaka huu tumeongeza zaidi ya bilioni 1.7 ambayo kimsingi haijawahi kupatikana katika eneo lolote. Hayo ni mafanikio makubwa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi tumeona uwekezaji mkubwa kwenye eneo hili. Bandari ya Dar es salaam ilikuwa na maneno mengi kwa miaka minne iliyopita. Ilikuwa na maneno mengine kwamba magari ambayo yanahifadhiwa pale sehemu haitoshi, kwenye ile row ambayo inapokea magari lakini kama haitoshi gati namba moja mpaka namba tatu imeboreshwa, gati namba nne na namba saba imeboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyoongea ushushaji wa shehena umeongezeka kwa kiwango kikubwa ambayo ni tofauti na huko nyuma ambayo ilikuwa ni kero kubwa kwa ajili ya Bandari yetu ya Dar es salaam na hata ilitishia baadhi ya wateja kutokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi tumeenda kukaribisha Sekta Binafsi. Kazi hii kama Kamati tumeiona ni kazi kubwa. Leo hii tunavyoongea tumepunguza gharama za uendeshaji kwa 30% ambazo zilikuwa zinafanyika wakati inaendeshwa na Serikali. Kwa hiyo maana yake ni kwamba mwekezaji amekuja kuwa ni sehemu ya uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo imekuwa ni kimbilio katika nchi zinazotuzunguka katika ukanda huu wa nchi nane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilitaka niseme nini? Niendelee kuwaomba sana Wizara endeleeni kusimamia mipango ambayo ipo kwa ajili ya gati namba 8 – 11 pamoja na 12 na 15 ikiwemo pale eneo la kupokelea mafuta matanki 15 yale ambayo yatasaidia kuwa na hifadhi ya mafuta nchini hata likiyumba soko la mafuta duniani bei itabakia palepale na itaendelea kuongeza uchumi wa nchi. Kazi hii endeleeni kuifanya kwenye lile eneo la single receiving terminal iendelee kwa kasi ambayo imeanza na kwa hakika najua Mheshimiwa Waziri utaendelea kusimamia jambo hili. Hongera sana kwa kazi nzuri ya Bandari ya Dar es salaam lakini tunaona Bandari ya Tanga na Mtwara kazi nzuri inafanyika. Endeleeni kufanya hivyohivyo ili kuongeza uchumi wa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la pili tumekuwa na gharama za uendeshaji zilizopungua. Tumeweza kuongeza bakaa la mapato. Bakaa la mapato lilikuwa shilingi bilioni 45 lakini leo bakaa la mapato limekuwa bilioni 142. Ni jambo kubwa ambalo halijawahi kutokea fedha hizi zitaenda kufanya kazi kubwa ya kujenga hospitali, kujenga shule, kujenga barabara ambazo Wabunge wote wamekuwa wakisema hapa kwa sababu mapato yatapatikana kwa wingi katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunaposikia watu wanasema “no reforms no election” si kwa bahati mbaya. Hata wewe huogopi kwa maendeleo haya? Lazima useme “no reforms no election” kwa sababu ukiingia uwanjani unapigwa asubuhi bado kweupe. Hauna sababu ya kupata aibu bora uweke mpira kwapani ondoka usije ukapatwa na aibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningekuwa hata mimi ningesema “no reforms” kwa hali iliyofanywa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtaturu kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kingu.
TAARIFA
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaomba nimpe taarifa mchangiaji anayechangia kwa uzalendo mkubwa sana Mbunge pacha na jirani yangu kwamba kilio cha “no reforms no election” lazima kitaendelea kwa sababu kwa impact hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Shirika la Ndege peke yake sasa hivi linaingiza jumla ya mapato ya dola milioni 354 kwa miaka minne, Sekta ambayo inaelekea kuwa Sekta ya tatu katika kuleta forex za nchi. Nani atakuja kwenye uchaguzi kushindana na CCM? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninampa mchangiaji taarifa ya kwamba kwa namna ambavyo uchukuzi wameupiga mwingi, kwa kweli “no reforms no elections” wataendelea kuisema kwa sababu hakuna wa kuja ku-compete na Chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi ujao. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtaturu unaipokea hiyo taarifa ya Mheshimiwa Kingu?
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapokea taarifa kwa heshima ya pacha wangu Mheshimiwa Elibariki Kingu lakini ninaomba niseme tu kwamba hata wale wanaosema kwamba “Hatuchezi” nao pia naona ni haohao. Wanafanana na hao ambao wanasema “no reforms no election” kwa sababu hali ya mziki wa Mpanzu na wengine ni mkubwa sana pale watakapoona tunaenda kubeba kombe. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtaturu malizia nusu dakika.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie eneo la reli. Reli imefanyika vizuri sana na uwekezaji mkubwa tumepata zaidi ya shilingi bilioni 60 katika muda mfupi. Hili ni jambo kubwa lakini hata Balozi wa Marekani alipopanda kwenye ile treni aliona ni bora kuliko ya Marekani maana yake ni kazi kubwa iliyofanywa na Serikali yetu. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja. Niombe sana eneo moja tu la viwanja vya ndege. Viwanja vya ndege vilisemwa vitajengwa katika viwanja 11 vya Songea, Iringa, Musoma, Tanga, Dodoma pamoja na Singida lakini naona viwanja vingine vinajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe na kiwanja cha Singida kiko karibu na Makao Makuu ya nchi na chenyewe kiangaliwe. Nitaomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu nimechangia kwa uzalendo kwenye eneo hili, nikuombe unaposimama uwaambie watu wa Singida kiwanja cha Singida kimekwama nini ili na sisi wale watoto wa Dar es Salaam ambao hawajawahi kuja Singida warudi nyumbani waje wapande ndege kwa sababu wengine wamesema bila ndege hawarudi nyumbani. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. Asilimia 100 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mitano tena. (Makofi)