Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia afya na uhai na vilevile nichukue nafasi hii kabisa kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kiongozi wetu, mwenye maono na mwenye kusimamia vyema Serikali yake kiasi cha kutoa matumaini makubwa kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu pia nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Pofesa Makame Mnyaa Mbalawa, Waziri wa Uchukuzi, Naibu wake Mheshimiwa Kihenzile, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Uchukuzi kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya inayoleta matumaini kwa Watanzania kuongeza, na kuchechemua uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimepata bahati juzijuzi hapa ya kwenda kutembelea Bandari ya Kalema iliyoko katika Ziwa Tanganyika kwenye Mkoa wa Katavi na kule tumekwenda kuangalia sekta binafsi ambao wanajenga meli nne za mizigo ambapo kila meli moja itakuwa inachukua tanai elfu mbili, kwa hiyo, meli hizo nne zitakuwa zinachukua tani 8,000. Hawa wawekezaji wanaweka zile meli kwenye Ziwa Tanganyika kwa ajili ya kuchukua mzigo wao wa madini kutoka Congo, kuuleta kwetu kwenye bandari zetu na kuuleta Bandari ya Dar es Salaam na kusafirisha kwenda nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanachosema, wenyewe mzigo wao ni wa kutoka Congo tu, mzigo wa kupeleka Congo watachukua mizigo ya watanzania na wafanyabiasha wengine, iwe ni mahindi, iwe ni karanga, chochote kile watabeba kwa gharama nafuu kukipeleka Congo kwa sababu wao tayari gharama zao zitakuwa zimejilipa katika kuleta madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapongeza hatua hii kwa sababu siku zote tumekuwa tukisema hapa katika Bunge hili, Serikali haiwezi kufanya kila kitu, Serikali ni lazima ihusishe sekta binafsi katika kuhakikisha kwamba huduma kwa wananchi zinapatikana. Serikali inajenga barabara lakini haina mabasi, mabasi ni ya watu binafsi ndiyo yanapita kwenye barabara na hata hii SGR huko tunakokwenda itafika mahala miundombinu ni ya Serikali lakini itakuwa inapita Treni ya Kuchauka inapita hapo, Treni ya Prof. Manya inapita hapo, analipa miundombinu. (Na nyie hamumshukuru Mungu ninawaombea mambo mema hayo au mpaka niseme ya Mheshimiwa Bakhresa. (Kicheko&Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niunge mkono juhudi zinazoendelea za Bandari ya Dar es Salaam, watanzania mmeona. Tulisimama katika Bunge hili tukawatoa hofu tukawaambia kinachokwenda kufanyika ni kikubwa kutoka TICTS iliyokuwa inaendesha bandari kuja DP World tumeongeza shilingi trilioni moja, trilioni moja ni karibu asilimia nne hadi tano ya bajeti ya nchi yetu imeongezeka kutokana na uwekezaji mzuri uliyofanywa pale. Kwa hiyo, tunapongeza sana Serikali kwa hatua hii na hasa tunampongeza Rais wetu, aliziba masikio akasema mimi sitaki kusikia kelele, ninafanya mambo kwa manufaa ya watanzania, wakiyaona watanipongeza na leo tunampongeza Rais wetu kwa kazi kubwa na nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uchukuzi ni kazi ya chain, unatoka kwenye reli, reli ikifika kwenye bandari, bandari inachukua, bandari ikikoma inachukua barabara inapeleka mpaka inapokwenda, ni kazi ya chain. Sasa ni lazima tuongeze kasi ya ujenzi wa reli, hasa SGR.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivyo kwa nini? Kwenye SGR pesa mnazo; mbona tunasuasua? Hebu tuongeze kasi! Mheshimiwa Profesa Mbarawa wewe tunakuamini siyo Profesa wa maneno, wewe ni Profesa wa vitendo na umeonyesha kazi kubwa sana, ongeza kasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hii ikiweza kufika Kigoma mizigo inayotoka Kongo ya madini itakwenda kwenye Bandari ya Dar es Salaam; kwa hiyo tutakuwa na chain. Kwenye reli tutapata, kwenye meli tutapata, na Bandari ya Dar es Salaam tutapata, kwa hiyo ongezeni kasi. Hizi kilometa 506 za Tabora - Kigoma ambazo sasa hivi mmefikia 7.88%, mimi ninaamini katika kipindi kisichozidi miezi sita mkiamua tunaweza tukaenda mpaka 40%; hebu ongezeni kasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niwapongeze kwa hatua mliyoanza nayo ya kujenga kiwanda cha meli kule Kigoma. Nimesikia tayari mmempa advance yule mkandarasi na kazi imeanza pale eneo la Katabe katika ufukwe wa Ziwa Tanganyika. Hii nayo itatusaidia sana; meli zote za Zambia, Kongo, Burundi na Tanzania tukiwa na ship yard pale imekamilika watakuja kufanya ukarabati pale, tutapata fedha na hiyo itasaidia sana kuongeza mzunguko wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na suala la meli ya MV. Liemba na MV. Mwongozo. Mheshimiwa Waziri ninarudia kukupa maua yako. Uliahidi katika Bunge hili kwamba utafanya kila namna uwezavyo utoe fedha ili kazi ile ianze. Ninashukuru nimeona kazi ile imeanza. Sasa hivi meli ile imepandishwa kwenye cherezo na mpaka sasa kazi ninaambiwa iko kwenye asilimia karibu 24. Ninakupa hongera sana kwa kazi hiyo na nikuombe endelea na kazi ya Mwongozo kwa sababu kazi ya Mwongozo ni ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Mwongozo ni stability tu. Kila kitu kiko sawasawa; engine iko sawasawa na vitu vingine vyote viko sawasawa. Hebu anza na kazi ile ya Mwongozo, Mwongozo inaweza ikatoka haraka na wananchi wetu wakaweza kupata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninarudia tena kutoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa haya mambo ambayo wananchi wetu wameyaona wenyewe sasa. Ninarudia tena kutoa pongezi nyingi kwako Mheshimiwa Profesa Mbarawa na Naibu wako na Wizara nzima ya Uchukuzi; endeleeni kupiga kazi na sisi tunawaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi