Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ambaye ametujalia na kutuwezesha kuendelea kuwepo humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri lakini kwa kazi kubwa na nzuri inayofanyika kwenye sekta anayosimamia kwenye Wizara ya Uchukuzi. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wako mnafanya kazi nzuri pamoja na watendaji kule Wizarani, tunawapongeza sana tunaendelea kuwatakia kila lakheri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango kwenye maeneo machache. Eneo la kwanza, Mheshimiwa Rais alipokuwa kwenye ziara kwenye Mkoa wa Tanga, Tarehe 24 Februari alipokuwa Korogwe tulimuomba kwamba Serikali itukumbuke ujenzi wa Reli ya kisasa kwa upande wa kaskazini, lakini watu wa Korogwe tuliomba kwa namna jiografia ya Korogwe ilivyo tunafaa kuwa na logistics centre ya uhakika kwenye lile eneo kwa ajili ya kukuza biashara kwenye maeneo yale. Tunaomba Mheshimiwa Waziri maombi haya tuliyompa Mheshimiwa Rais muendelee kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili na la mwisho ninalotaka kuchangia ni kuhusu bandari, kwenye bandari nina maeneo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza Mheshimiwa Rais akiwa Tanga aliahidi kwamba barabara ya kutoka Handeni kwenda Kibirashi itakwenda kujengwa kwa ushirikiano kati ya Bandari na wenzetu wa TANROADS wakae waone namna ya kujenga barabara hii ili iweze kusaidia Bandari ya Tanga iweze kufanya kazi vizuri. Tunaiomba Bandari na TANROADS mkae pamoja timizeni ahadi aliyoitoa Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye upande wa bandari, kipekee ukichukua takwimu za mafanikio na ufanisi wa bandari yetu kwa sasa hasa bandari ya Dar es Salaam, tuna kila sababu ya kukiri kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakika ni mzalendo namba moja wa nchi yetu, lakini ni kiongozi mwenye maono makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa mchakato wa uwekezaji kwenye bandari kulikuwa na maneno mengi, mengine ya hovyo, mengine ya kusadikika, mengine ya kufikirika lakini ukisikiliza na ukipata takwimu ya mafanikio ya bandari yetu kwa sasa, Mheshimiwa Rais ni mzalendo wa kweli na ni kiongozi jasiri aliyesimamia maono haya, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zinaonesha mapato kwenye bandari yameongezeka kwa zaidi ya shilingi trilioni moja katika kipindi hiki cha mwaka mmoja tu huu, lakini siyo hivyo tu, muda wa meli kusubiri dangani umepungua kwa kiwango kikubwa sana, lakini muda wa kuhudumia meli kutoka wastani wa siku saba mpaka siku tatu, muda wa meli kupungua dangani umepungua kutoka wastani wa siku 46 mpaka leo tunavyozungumza tuko kwenye siku saba, haya ni mafanikio makubwa sana kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mafanikio haya na kwa uzoefu wa kazi hii kubwa ya kijasiri aliyoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mimi nakuja na ushauri mmoja leo kwenu, inawezekana muda wa mwaka mmoja usitoshe kuufanyia kazi lakini mna muda wa kuufanyia kazi. Tunaomba tuishauri, kwa kutumia uzoefu wa kazi hii aliyoifanya Mheshimiwa Rais, Wizara na Serikali anzeni kutafuta namna ya kuanzisha na kukuza biashara mpya kwenye bandari, biashara ya kufaulisha mizigo na ili biashara hiyo ifanyike vizuri tunawapa wito, tafuteni wawekezaji wengine tukajenge bandari mahsusi kwa ajili ya jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo eneo zuri sana kule Tanga. Tukishindwa kujenga kwenye Bandari ya Tanga ilipo sasa tuna eneo la Pangani Deep Sea zuri kabisa, tuna eneo la Mwambani, tutafute uwekezaji, tuanzishe ujenzi wa bandari nyingine kwa ajili ya biashara mahsusi ya kusafirisha mizigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua jiografia ya Bara la Afrika liko katikati ya Mabara hayo mengine yote kwa maana ya Asia, Amerika, lakini ukichukua Tanzania ambayo iko katikati ya Bara la Afrika Pwani ya Mashariki, huu uzuri wa jiografia yetu unazifanya bandari zetu kuwa sehemu na kitovu muhimu sana kwenye biashara ya kufaulisha mizigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujatumia vizuri uzuri wa jiografia tulionao, tunazo nchi ambazo hazina uzuri wa jiografia kama Tanzania lakini zimetumia mbinu hii ya biashara na zinafanya vizuri na nitakupa mfano wa nchi mbili. Nchi ya kwanza ni Singapore, wakati Singapore inapata uhuru mwaka 1964, GDP ya Singapore ilikuwa ndogo kuliko GDP ya Tanzania. Singapore imepata uhuru GDP yake ni dollar milioni 894.15 wakati huo GDP ya Tanzania ilikuwa dollar bilioni 3.75, lakini mpaka mwaka 1979 GDP ya Tanzania ilikuwa kubwa kuliko Singapore, lakini leo Singapore GDP yake ni mara sita ya GDP ya Tanzania, na sekta zinazokuza uchumi wa Singapore ni tatu tu, kwanza ni bandari, pili ni utalii na ya tatu ni huduma za kifedha. Kwa sasa bandari ya Singapore ni bandari ya pili kwa ukubwa duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu za mwaka 2023 bandari ya Singapore, imehudumia meli 193,016, lakini bandari ya Singapore imehudumia shehena milioni 41.12 katika shehena milioni 41.12 asilimia 90 ya shehena hizi ni transshipment ni kufaulisha tu. Ukiacha hiyo tunayo bandari ya Salalah iko Oman imeanzishwa mwaka 1998 kwa mkataba wa PPP kati ya Serikali ya Oman na Shirika la AP Terminals, Kampuni ya Meli. Kwa mwaka 2023, Bandari ya Salalah imehudumia meli milioni 3.8 katika meli milioni 3.8 asilimia 98 ya mizigo iliyohudumiwa, shehena zilizohudumiwa na bandari hii ni za kufaulisha, sisi tunakwama wapi kufanya jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara tuanze kubuni namna ya kupata mwekezaji, very strategic investor tukajenge bandari Tanga mahsusi kwa ajili ya biashara ya kufaulisha mizigo na tukijenga hii bandari, bandari yetu hii itakumbana na ushindani wa maeneo mawili tu, kwanza itakuwa ni bandari hii ya Salalah lakini ya pili itakuwa ni Bandari ya Djibout. Ukienda kwenye ushindani Bandari ya Salalah haitatusumbua sana pamoja na kwamba ina advantage nyingi, ikiwemo advantage ya kuwa karibu na Bahari ya Sham kwa hiyo kuwa karibu na masoko ya Amerika na Ulaya lakini wako mbali sana na Route ya Cap of Good Hope ambapo sisi bandari zetu kwa jiografia yetu ziko karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushindani ya pili inawezekana ukawa Bandari ya Djibout, hauwezi kuwa mkubwa kwa sababu Bandari ya Djibout sasa hivi haina mwekezaji baada ya DP World kuondoka, lakini pia ina hudumia meli chache, wastani wake ni meli 350,000 kwa mwaka. Mtu pekee ambaye ni tishio kwetu kwenye jambo hili ni nchi moja jirani ambayo siitaji, bandari yao iko karibu na sisi jiografia yetu ni moja, location yetu ni moja. Wakituwahi kwenye jambo hili wenzetu watafanya biashara nzuri zaidi kuliko sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sisi tuanze kutafuta wawekezaji, na kwenye kutafuta wawekezaji kwenye miradi mikubwa kama ilivyokuwa kwenye DP World huwezi kuanza kutangaza, ukitangaza huwezi kupata strategic investor unachotakiwa kufanya ni kutafuta makampuni makubwa duniani, tunakaa nayo, tunazungumza nayo, tuna negotiate terms, kwa sababu haya makampuni makubwa mengi yao yenyewe yana miliki meli kwa hiyo yatakuwa na uhakika wa kuleta meli, yana uhakika wa mizigo. Niombe sana Serikali ni wakati sahihi tuanze kuwaza jambo hili na mimi naona eneo sahihi sana kwenye jambo hili ni eneo la Tanga, tuna eneo la Pangani na tunalo eneo la Mwambani, maeneo yote mawili haya yanafaa kwa ajili ya ujenzi wa bandari hii kwa ajili ya kufanya kazi ya kufaulisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)