Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaomba nichukue nafasi hii kukushukuru wewe mwenyewe kwa kuongoza Bunge hili siku hii ya leo na kuweza kufikia wakati huu wa kuhitimisha hoja ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee ninatumia fursa hii tena kuishukuru Kamati yako ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, chini ya uongozi wake Mheshimiwa Timotheo Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini. Kwa kweli, Kamati hii imekuwa ikitoa miongozo, ambayo imefanya leo tumefikia mafanikio makubwa sana katika utendaji kazi wa Wizara yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ninawashukuru wachangiaji wote waliochangia hoja yetu hii, jumla ya wachangiaji nane wamechangia hoja hii. Nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge, mawazo na ushauri wote walioutoa, sisi kama Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tunaenda kuufanyia kazi na kuhakikisha kwamba, tunaporejea hapa waone mambo yote waliyoyasema yamefanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezizungumzia. Suala la Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, miaka minne hii ya utawala wa Mheshimiwa Rais wetu kipenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan, tume hii imefanya kazi kubwa sana. Kwa sababu, tangu tupate uhuru katika vijiji 12,333 tulivyonavyo, amezungumza hapa Mheshimiwa Mnzava, vijiji vilivyokuwa vimewekewa matumizi bora havizidi 2,600, lakini katika kipindi cha miaka minne tumeona vijiji zaidi ya 4,000 vikiwa vimewekewa matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza, kwa ushauri wa Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge, tumefanikiwa kupokea shilingi bilioni tano kutoka Wizara ya Fedha, kwa ajili ya kwenda kuendeleza upimaji wa vijiji 333 na kuweka matumizi bora. Kazi hiyo imezinduliwa Wilayani Ikungi, Mkoani Singida, wiki kadhaa zilizopita na Kamati yako ya Bunge ilishiriki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawahakikishia kwamba, lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na sisi wasaidizi wake ni kuhakikisha mipango ya matumizi bora ya ardhi inakuwepo kwenye vijiji vyote 12,333. Hii ndiyo itakwenda kuondoa mzizi wa migogoro ya ardhi, hasa kati ya wakulima na wafugaji. Amezungumza hapa Mheshimiwa Lusinde, ipo migogoro kwa sababu ya maeneo kutokupangwa na kuwekwa, kwa ajili ya ufugaji na kilimo, ama maeneo mengine yanakuwa yamepangwa, ambayo hayako suitable, kwa ajili ya kimoja ama kingine. Kwa kupima vijiji vyote hivi, tutahakikisha tunaondokana na changamoto hiyo. Ninalihakikishia Bunge lako kwamba, tunakwenda kutekeleza hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Plot Development Revolving Fund, ambapo ndiyo Mradi wa KKK upo. Tangu Development Fund hii ianzishwe haikuwahi kuwekewa hata senti moja, lakini katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweza kuweka shilingi bilioni 50, ambayo fedha hii imekwenda kupima viwanja zaidi ya 12,303.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia Mheshimiwa Chege, amezungumza changamoto ya halmashauri kutorejesha fedha hizi. Tumekaa na wenzetu wa TAMISEMI, tumekaa na wenzetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambayo yeye, Mheshimiwa Chege, ni Makamu Mwenyekiti. Tumekubaliana ya kwamba, kuanzia sasa hakuna maombi yoyote ya halmashauri yataletwa moja kwa moja kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama halmashauri inaona ina uhitaji mkubwa wa kupima viwanja kupitia Mradi huu wa KKK ipitishe maombi yake TAMISEMI; TAMISEMI ione uwezo wa halmashauri ile kurudisha. Kwa sababu, wengine walichukua fedha, walienda kupima katika maeneo ambayo hayauziki na ndiyo maana fedha hii hairejei. Tumeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba, tunalinda fedha hizi shilingi bilioni 50 zilizotolewa na Dkt. Samia Suluhu Hassan na tunahakikisha viwanja zaidi vinaendelea kupimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumziwa kwa upana wake na Waheshimiwa Wabunge waliochangia; amezungumza Mheshimiwa Mnzava, Mheshimiwa Kunambi, Mheshimiwa Asenga na Waheshimiwa wengine waliopata nafasi ya kuzungumza wamegusia sana suala la Kamisheni ya Ardhi na namna ambavyo inakwenda kutatua changamoto mbalimbali. Ninasema mbele ya Bunge lako Tukufu, tumechelewa sana kuwa na Kamisheni kama hii ya Ardhi na tumechelewa sana kuweka utaratibu madhubuti wa kuhakikisha nchi yetu inakuwa imepimwa na imepangwa vilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kuna mwingiliano mkubwa kati ya Mamlaka ya Upimaji na Mamlaka ya Halmashauri, kuna changamoto kubwa. Kwenye master plan unakuta kuna eneo, mfano Jimboni kwako pale Kariakoo, master plan huenda inasema mwisho ni ghorofa kadhaa, tano au sita, ama jengo lilijengwa kama apartment, tumeona changamoto zikijitokeza za maghorofa kudondoka, lakini mabadiliko ya matumizi yanapofanyika Wizara ya Ardhi haihusiki. Mabadiliko ya matumizi kwenda kwenye commercial hayapiti katika entity nyingine za Serikali kuhakikisha ya kwamba, jengo lile linaweza kuhimili mabadiliko hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwa Dar es Salaam, Masaki na Oyster Bay, mpango madhubuti wa maeneo yale uliopitishwa na Baraza la Mawaziri unasema ni ground plus five, maximum. Kuna watu wanaojenga ground plus nine, plus ten, ni kwa sababu ya mamlaka kuingiliana. Anapokwenda kuomba kibali cha ujenzi, mtu anaomba cha ghorofa 10 anapewa, hawajui master plan iko vipi! Suluhisho la hili na migongano hii inayojitokeza ni kuhakikisha tunakuwa tuna Land Commission.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawatoa mashaka Waheshimiwa Wabunge, kuwa na Land Commission hii haimaanishi kwamba, tunakwenda kutoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Bado Serikali za Mitaa itakuwa ni kiungo muhimu sana katika utekelezaji wa kazi za Kamisheni hii ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia ndugu yangu, Mheshimiwa Kunambi, amezungumzia suala la Tume na RERA kuwa, chini ya Commission hii. Sasa kwa sababu tuko katika initial stages za kuanzisha tume hii tunachukua mawazo hayo na kwenda kuyafanyia kazi. Nimemsikia Mheshimiwa Mnzava akisema isiathiri D by D; haitoathiri D by D, tutahakikisha tunaboresha yale malengo ya D by D yaweze kuendelea kuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye suala la kuanzisha Real Estate Regulator Authority (RERA), kwenye masuala ya miliki, na lenyewe tumechelewa sana. Kumekuwa kuna uholela mwingi katika Sekta ya Real Estate.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mwananchi wa kawaida anayetaka kununua kiwanja ili aweze kujenga kwa kipato chake anachokipata anaweza akatafuta dalali A akamwonyesha kiwanja, dalali B, akamwonyesha kiwanja kile kile, dalali C, akamwonyesha kile kile; lakini si ajabu hawa watu wote mwenye kiwanja hawafahamu, mwenye kiwanja hawajui, ama hata nyumba ambayo inauzwa; ni kwa sababu kuna uholela mwingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kuweka utaratibu ambao utamlinda Mtanzania katika kuhakikisha tunawafahamu wenye nyumba, tunawafahamu wanaofanya kazi katika sekta ya milki ili mwananchi awe salama, lakini hata mwenye nyumba na yeye awe salama. Kwa hiyo ni jambo ambalo nalo lilichelewa na niwahakikishie tutalileta hapa Bungeni kwa ajili ya kupitisha sheria zake tuweze kuanza kulitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa hapa suala la migogoro ya ardhi. Ni kweli kwamba kuna changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi na migogoro hii ipo ya aina mbalimbali. Kuna migogoro ambayo ni administrative ambayo ni jukumu letu kama Wizara, kuna migogoro ambayo ni ya kifamilia, lakini tafsiri ya jamii inaona kama ni wajibu wa sekta ya ardhi kutatua administratively; labda mirathi na kadhalika na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna migogoro ambayo imeshatolewa maamuzi na Mahakama. Katika maamuzi hayo sisi kama administrators hatuwezi kuingilia Mhimili mwingine; wajibu wa ku-counter maamuzi yale ya Mahakamani kukata rufaa katika chombo cha Mahakama ili uamuzi unapotoka, sisi kama administrators tuweze kutekeleza wajibu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mengine lazima nikiri ni migogoro iliyotengenezwa na watumishi wetu wenyewe katika sekta ya ardhi. Mheshimiwa Msambatavangu amezungumzia kuhusu masuala la double allocation ambayo yamekuwa kinara katika Jiji letu la Dodoma na maeneo mengine. Nitoe maelekezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hapa leo mbele ya Bunge lako Tukufu; ni marufuku kuendelea kutumia mfumo mwingine zaidi ya e-ardhi katika kutoa au kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, double allocation ilikuwa inatokeaje; unakuta mtumishi wetu kwa makusudi na kwa kufahamu anakwenda kwenye mfumo ambao hatuutumii tena wa MORIS anatoa hati. Anakuja Mheshimiwa Msambatavangu na yeye anataka hati ya kiwanja hicho hicho anaingia kwenye e-ardhi, kwa sababu mifumo ile ilikuwa haisomani. Kwa hiyo unakuta eneo moja lina hati mbili. Kuanzia leo ni marufuku kuendelea kutumia mfumo wa zamani. Tutahakikisha nchi nzima mpaka ifikapo mwaka 2027 tunaweka mfumo mzima wa e-ardhi ili kuondokana na changamoto hizi za migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Kunambi kuwa nitafika Jimboni kwake. Nimhakikishie Mheshimiwa Asenga kuwa mgogoro ule wa pale kwa Baba Askofu tayari fedha imekwishapelekwa kwa ajili ya kuanza upimaji na kwenda kutatua. Vile vile Mheshimiwa Halima juzi tumekaa na wazee wale; niwaahidi na Mheshimiwa Mbunge wa jimbo rafiki yangu Mheshimiwa Mtemvu, kuwa tutahakikisha kwamba tunafika kuweza kusikiliza pande zote mbili tuone tutatue changamoto ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, si tu kwa Mheshimiwa Mtemvu, hata kwa Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo ambapo maeneo haya yameingiliwa. Tayari kuna nyumba zaidi ya laki mbili katika eneo hilo; ninaamini tutapata ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza Mheshimiwa Naibu Waziri juu ya Shirika letu la Nyumba na wewe mwenyewe uliligusia wakati unamtambulisha DG. Ni kwamba tunaendelea na mradi wa Samia Scheme; na tunatafuta njia bora ya kuhakikisha kuwa tunapata nyumba za bei nafuu ambazo Watanzania wengi wataweza ku-afford kuzinunua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wanafahamu kuwa ililetwa Bungeni hapa kwa ajili ya kuondoa VAT katika nyumba ambazo zipo chini ya milioni 50; na sasa tunapoelekea ni kutafuta namna ya kuondoa VAT kwenye nyumba amhazo hazizidi milioni 100; na huku tunatafuta teknolojia mpya kwa kuangalia kwa wenzetu nchi mbalimbali wanajenga vipi katika kupunguza gharama ili tupate nyumba ambayo Mtanzania wa kawaida ataweza ku-afford. Hii ndiyo njia pekee pia ya kulinda ardhi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi tuliyokuwanayo wakati wa uhuru wetu mwaka 1961 tukiwa Watanzania milioni tisa ni ardhi ile ile na mipaka ile ile ambayo tunayo leo hii ambayo tuko Watanzania milioni 65. Tukiacha tusambae bila mipango, bila kwenda juu na kujenga nyumba za bei nafuu tutajikuta tunamaliza ardhi yote ambapo vizazi vijavyo vitakosa mahali pa kwenda. Ni lazima tujenge kwenda juu, lakini vile vile tuipendezeshe na miji yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, michango mingine ya Waheshimiwa Wabunge tumeipokea kwa maandishi; niwaahidi tunakwenda kuifanyia kazi. Tutahakikisha kwamba tunaibadili sekta ya ardhi kwa kuweka mifumo madhubuti ya kuhakikisha tunaondokana na migogoro. Niseme tu kwamba Mheshimiwa Rais katika kipindi changu cha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametupa support kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hivi majuzi tu ametupatia magari zaidi ya 50 ambayo yanakwenda kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli zetu katika sekta hii ya ardhi. Hata hili land commission ambalo tunalizungumzia ni jambo ambalo yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais alielekeza Siku ya Uzinduzi wa Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995, Toleo la 2003.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wizara ipo mbioni katika kuandaa sheria mbalimbali zinazotokana na sera ile ili tulete hapa Bungeni; na kanuni mbalimbali, ili tuanze kutekeleza sasa kama vile sera inavyotutaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, ninaomba sasa nitoe hoja mbele ya Bunge lako ili tuweze kupitishiwa bajeti yetu. Ninashukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
(Hoja ilitolewa iamuliwe)